WALIOLIPUA ARUSHA KUNASWA!
WATU waliohusika na kutega bomu linalohisiwa kuwa ni la kienyeji katika baa ya Arusha Night Park huenda wakanaswa kirahisi baada ya polisi kuchukua mitambo ya usalama (CCTV) iliyofungwa kwa ajili ya kufanya uchunguzi.
Katika tukio hilo lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita, jumla ya watu 17 walijeruhiwa, baadhi yao vibaya sana wakati wakinywa na kufuatilia katika televisheni michuano ya soka inayochezwa katika nchi mbalimbali barani Ulaya.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas aliyefika eneo la tukio haraka akiwa na kikosi cha ukaguzi wa mabomu, mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na wa wilaya ya Arusha, John Mongella walishuhudia majeruhi wakiondolewa na kupelekwa katika hospitali mbalimbali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Mmiliki wa baa hiyo, Joseph Karugendo alisema anaamini waliohusika na tukio hilo lililojeruhi wafanyakazi na wateja wao watapatikana kwani walifunga mitambo ya kufuatilia matukio ya CCTV.
“Baada ya tukio lile polisi walifika, wakazingira eneo lile hivyo leo
asubuhi (juzi) polisi wameondoka na ‘monitor’ ya CCTV pamoja na mfanyakazi wetu mmoja kwa lengo la kwenda kufanyia uchunguzi wa picha hizo,” alisema mkurugenzi huyo.
Mmoja wa wahudumu waliokuwepo wakati tukio hilo likitokea, Aneth Mushi, alisema alikuwa amebeba chakula cha wateja ndipo aliposikia kishindo kikubwa na kelele za watu zilizomfanya aangushe sahani za chakula na kukimbia.
“Kwa kweli nasikitika sana watu wameumia na mimi ni Mungu tu kaniokoa vinginevyo ningeweza kuwa mmoja wa majeruhi,” alisema Aneth.
Hili ni tukio la tatu la bomu kutokea kwenye Jiji la Arusha kwa kipindi cha
mwaka mmoja ambapo jumla ya watu saba wamepoteza maisha huku wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa.
Katika tukio la Mei 5, mwaka jana bomu lilirushwa kwenye Kanisa laKatoliki la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti ambapo jumlaya watu watatu walifariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Tukio la pili ni lile la Juni 15, mwaka jana ambapo bomu lilirushwa kwenye
mkutano wa kufunga kampeni wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) kwenye Viwanja vya Soweto ambapo jumla ya watu wanne walifariki dunia akiwemo mwanamke mmoja na watoto watatu.
Hata hivyo tayari mtu mmoja amefikishwa mahakamani kuhusiana na tukio la bomu kanisani.
-GPL
0 comments:
Post a Comment