Friday 2 May 2014

JK: MISHAHARA ITAPANDA, KODI ITAPUNGUZWA KATIKA BAJETI YA 2014/2015


 
Rais Jakaya Kikwete ametoa ahadi mbili za kuwafurahisha wafanyakazi. Kwanza ametangaza nia ya kuongeza mishahara yao na pili, kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara hiyo mambo ambayo ameahidi kutekelezwa katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni hivi karibuni.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema anatambua kuwa wafanyakazi wana hamu ya kujua Serikali itasema nini kuhusu masilahi yao.
Alisema malalamiko ya wafanyakazi wengi ni kutaka kuona kima cha chini cha mshahara kinaongezwa huku kodi kwenye mishahara (Paye), ikipungua.
“Mimi na wenzangu serikalini hatuna upungufu wa dhamira ya kufanya hivyo, tumethibitisha miaka iliyopita na tutaendelea kuwa hivyo,” alisema.
Huku akishangiliwa na wafanyakazi waliofurika katika Uwanja wa Uhuru, Rais Kikwete alisema: “Najua kuwa nyongeza tuliyotoa mwaka jana si kubwa kama wafanyakazi walivyotaka iwe... hata mimi nisingependa iwe hivyo.”
“Kwa nyongeza iliyofanywa mwaka jana, hivi sasa Serikali inatumia asilimia 44.9 ya Bajeti kulipa mishahara ambayo ni asilimia 10 ya Pato la Taifa.”
Akifafanua namna Serikali ilivyofikia uamuzi wa kuongeza mishahara kwa mwaka huu, Rais Kikwete alisema kulikuwa na mjadala mkali baina ya wafadhili waliodai nyongeza ni kubwa mno.

“Ni kweli mapato yetu ni madogo lakini kwa kuwa mishahara ni midogo, lazima tuendelee kuongeza, hata hicho kidogo lazima ukitoe ili uijenge ile nafuu, alisema bila kutaja kiwango kitakachoongezwa.
“Hata sasa kumekuwa na ubishi mkali kati ya Wizara ya Utumishi na Hazina kuhusu nyongeza ya mwaka huu iwe mpaka kiasi gani, nikaingilia kati nikakubaliana na utumishi, Hazina walikuwa wanataka ipungue kidogo,” alisema.
Walimu na shemeji yao
Suala la mshahara lilijitokeza kwa namna nyingine kwenye maandamano ya wafanyakazi pale walimu walipoamua kusimama mbele ya jukwaa kuu na kumweleza Rais Kikwete ambaye walimtaja kama shemeji yao, kwamba hawajapata mshahara wa Aprili wakimtaka aingilie kati.
“Shemeji, shemeji, shemeji, hatujapata mishahara yetu ya Aprili, tunaomba utusaidie,” walitoa ujumbe huo kwa njia ya wimbo.

Tofauti na wafanyakazi wengine ambao walipita mbele ya mgeni rasmi bila kusimama, walimu walisimama kwa dakika moja kuhakikisha ujumbe huo unamfikia.
Wakati hayo yakitokea, Rais Kikwete na viongozi wengine walikuwa wakicheka huku wakiwaangalia walimu hao waliokuwa wakiendelea kuimba wimbo huo.
Ajira kwa wageni
Rais Kikwete aliagiza yafanyike marekebisho kwenye sheria ya vibali vya ajira ili kudhibiti ongezeko la wafanyakazi wa kigeni nchini ambao wanafanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.
Aliagiza hatua hiyo itekelezwe haraka hata ikibidi kwa kupeleka bungeni hati ya dharura ili kuhakikisha jambo hilo linaanza mara moja.
Malalamiko ya Tucta
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya alisema pamoja na ongezeko la mishahara kufanyika kila mwaka, limekuwa dogo mno kiasi cha kushindwa kufikiwa kima cha chini ya mshahara kinachotakiwa.
Alisema kwa upande wa sekta binafsi, Serikali imeongeza mshahara kutoka Sh100,000 hadi Sh450,000 mwaka jana, huku sekta ya kilimo ikiwa ya mwisho kwa kuwa na kiwango cha chini zaidi.
“Hali hii imesababisha kuwapo kwa upungufu mkubwa wa wafanyakazi mashambani na hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao,” alisema na kuongeza:
“Tunapenda kuikumbusha Serikali kwamba kumlipa mfanyakazi mshahara unaokidhi mahitaji muhimu ya maisha siyo jambo la fadhila, bali ni mojawapo ya haki za msingi za binadamu zinazosisitizwa na jumuiya za kimataifa.”
Tanga
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Hafsa Mtassiwa alisema Serikali inatambua changamoto zinazowakabili wafanyakazi zikiwamo za kodi ya mishahara kuwa juu na kwamba inazifanyia kazi.

Mbeya
Mratibu wa maadhimisho hayo mkoani Mbeya, Joseph Sayo ameiomba Serikali iache kuwanyonya wafanyakazi na kuwa mwajiri msumbufu kuliko wengine nchini.
“Serikali inadaiwa na wafanyakazi fedha nyingi na pia inawakopa wafanyakazi kwa njia mbalimbali zikiwamo za kupitia kwenye mifuko ya hifadhi za jamii na kushindwa kurudisha kwa wakati,” alisema.
Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo amewataka waajiri kufuata sheria na taratibu za kazi katika kuhakikisha kuwa wanawalipa wafanyakazi wao stahili zao ikiwamo nyongeza ya mishahara, kupandishwa vyeo na motisha kwa wanaostahili.
Geita
Wafanyakazi mkoani Geita, wameilalamikia Serikali kwa kushindwa kutekeleza ahadi mbalimbali ilizotoa kuboresha maisha yao, hivyo kulazimika kufanya kazi kwenye mazingira magumu.
Morogoro
Mratibu wa Tucta Mkoa wa Morogoro, Charles Luvunzu amesema rushwa na ukosefu wa uadilifu ni miongoni mwa mambo yanayokiukwa na waajiri wengi licha ya vyama vya wafanyakazi kuyapigia kelele.
Shinyanga
Tucta imewataka waajiri kuacha tabia ya kuwafukuza wafanyakazi kama kuku. Imeshauri wakae meza moja kujadiliana ili kutatua matatizo yanayowakabili sehemu za kazi.
Mwanza
Mratibu wa Tucta Mwanza, Evarist Mwalongo ameutaka uongozi wa mkoa kuwachukulia hatua za kisheria waajiri wasiofuata sheria za kazi huku akiitaka Serikali kubadilisha sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii, ili itoe mafao mazuri kwa wastaafu na kiwango cha kodi kwenye mshahara kipungue hadi asilimia moja.
Mara
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Henjewelle amewaagiza waajiri kuwalipa wafanyakazi masilahi yao kwa wakati ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara kazini.

Chanzo: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA