Kisanga cha mahabusu kuvua nguo mjini ARUSHA ,TANZANIA
Mahabusu wa Gereza Kuu la Mkoa wa Arusha, kaskazini
mwa Tanzania, Jumanne walisababisha vurugu katika viwanja vya Mahakama
ya Hakimu Mkazi mjini humo baada ya kuvua nguo na kugoma kushuka kwenye
basi lililowachukua kwenda mahakamani wakipinga kitendo cha watuhumiwa
wawili wa dawa za kulevya kuachiwa huru.
Watuhumiwa wanaolalamikiwa ambao mashtaka yao
yalibadilishwa mara mbili ili wapewe dhamana ni Dharam Patel na Nivan
Patel wanaodaiwa kukamatwa na kete 173 za heroini na misokoto 300 ya
bangi, Aprili,2014.
Kwa mujibu wa watu waliokuwa katika
eneo la mahakama hayo, mahabusu hao walikuwa wakipaza sauti kupinga
madaraja(ubaguzi) miongoni mwa watuhumiwa, wenye uwezo kifedha na wasio
nacho, hali ambayo imesababisha wengine kuachiwa na wengine kuendelea
kusota magerezani kwa kisingizio cha "upelelezi haujakamilika"
Mahabusu hao walisikika wakipaza sauti kutoka
ndani ya basi: "Wenzetu hata mwezi haujaisha wanafutiwa kesi, jamani
sisi tumekosa nini? Tunataka haki itendeke kwa wote" walisema.
Kuachiwa kwa watuhumiwa wanaolalamikiwa na
mahabusu wenzao kunasemekana kumetokana na hatua ya Ofisi ya Mkurugenzi
wa Mashtaka Arusha kubadilisha hati ya mashitaka na hivyo kuwawezesha
kupata dhamana.
Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Kuzuia Dawa za
Kulevya, Godfrey Nzowa ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa ofisi yake
haina taarifa za watuhumiwa hao kupewa dhamana lakini alisema kulikuwa
na jaribio la kufanya hivyo.
Bwana Nzowa amesema baada ya kubainika njama
hizo, ofisi yake ilipinga, akisema kuwa kosa la watuhumiwa lilikuwa wazi
na hivyo kuonyesha hali ya kutoamini kuwa watuhumiwa wanaweza kupata
dhamana kwa kosa hilo!
Hata hivyo Ofisi ya Mwendesha Mashitaka, DPP
haijaweza kulitolea maelezo suala la mahabusu hao kulalamikia mahabusu
wenzao kupendelewa katika utoaji wa haki kwa makosa wanayotuhumiwa.
NA BBC
0 comments:
Post a Comment