Tuesday, 6 May 2014

Mbowe: Mrema,Cheyo nje Baraza la Mawaziri


Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema ni vyama vitatu pekee vya upinzani ndivyo atakavyoviingiza kuunda baraza jipya la mawaziri kivuli.
Mbowe alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na NIPASHE lililotaka kujua muda wa kuunda baraza hilo na idadi ya vyama atakavyoviingiza baada ya kulivunja baraza la sasa wiki hii.
Alivitaja vyama hivyo kuwa ni Chadema, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).
Kwa mujibu wa Mbowe, sababu kubwa ya kuviingiza vyama hivyo kwenye baraza hilo ni kutokana na msimamo wao wa kushiriki vyema katika mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya na kujadili Rasimu ya Katiba sura ya kwanza na ya sita ya kwenye Mkutano wa Bunge Maalum la Katiba ulioahirishwa Aprili 25, mwaka huu hadi ngwe ya pili kuanzia Agosti 5, mwaka huu.

“Ni vyama vitatu tu ambavyo vipo kikamilifu katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), yaani Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi. Mrema (Augustine- TLP) yupo CCM na Cheyo (John-UDP) yupo nusu nusu, hivyo ni vyama hivyo vitatu tu ambavyo vipo Ukawa ndivyo vitakavyounda hili baraza jipya la mawaziri kivuli,” alifafanua Mbowe.

Kuhusu muda wa kuunda baraza hilo, Mbowe, alisema, yeye ndiye mwenye kuliunda na kwamba baada ya kulivunja la sasa, atatangaza wakati wa kupatikana kwa baraza jipya kwa kuwa la sasa bado lipo.

Kabla ya Mbowe ambaye ni mjumbe wa Bunge la Katiba na Mbunge wa Jimbo la Hai kutangaza maamuzi ya kufanya mabadiliko hayo, awali baraza hilo lilikuwa likiundwa na wabunge wa Chadema pekee. Baraza hilo liliundwa mwaka 2011 baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kuwashirikisha Chadema peke yao.

Mbowe alipounda baraza hilo alisema kuwa asingevihusisha vyama vingine vya upinzani kwa kuwa wakati huo havikuwa na mwafaka wala maslahi yanayofanana.

Hata hivyo, aliahidi kuwa angewateua wabunge wa vyama vingine baada ya kuridhika kwamba kambi ya upinzani ina mwafaka na msimamo wa pamoja katika masuala mbalimbali muhimu kwa nchi.

Mbowe alitangaza uamuzi wa kuundwa baraza jipya kivuli litakalovishirikisha vyama vingine Aprili 30, mwaka huu baada ya yeye pamoja na wajumbe wenzake wanaounda Ukawa, kufanya mkutano wa pamoja kwa lengo la kusisitiza msimamo wa muundo wa serikali tatu na kupinga wa serikali mbili unaoungwa mkono na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Viongozi wote wa kitaifa wa vyama hivyo vinavyounda Ukawa walihudhuria Mbowe alisema katika mkutano huo kuwa kulivunja baraza la sasa la mawaziri kivuli ili kuwaingiza pia wajumbe kutoka vyama vingine vya upinzani na kwamba ushirika uliopo baina vyama vyao hivyo hautaishia tu katika kudai katiba ya wananchi, bali utaendelea hadi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.

Kutokana na hilo, Mbowe, aliongeza kuwa wiki hii anatarajia kuvunja baraza la mawaziri kivuli na kuliunda upya ili kuhakikisha Ukawa inasambaa siyo katika Bunge Maalum la Katiba tu, bali katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika Uchaguzi Mkuu mwakani.

MREMA AZUNGUMZA
Alipoulizwa jana na NIPASHE kuhusiana na kauli ya Mbowe, Mrema alihoji kwamba wanaposema yeye ni CCM kwa nini hawazungumzii ndoa ya CCM na CUF ambao waliunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

“Mbona hiyo ndoa hawaisemi, badala yake wananisema mimi. Upinzani wa kusaliti nchi, sitaufanya na yale ya kubomoa nchi sitayakubali,” alisema.

“Nimewahi kushika Uwaziri wa Mambo ya Ndani, Kazi na Vijana pamoja na unaibu Waziri Mkuu hivyo kuwa waziri kivuli ni maigizo,” alisema Mrema.

Mrema pia alihoji ni kwanini baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanamuita kuwa ni CCM wakati wao wanapoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM hawakatai uteuzi huo.

Cheyo alipotafutwa jana simu yake ilikuwa inaita bila majibu.

Mrema ni Mbunge pekee anayetoka Tanzania Labour (TLP) na Cheyo ni Mbunge pekee kutoka United Democratic (UDP).

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA