JE WAJUA:::Watumiaji wa simu nchini wafikia milioni 27, Internet milioni 9
IDADI ya watumiaji wa huduma za simu nchini imeongezeka kutoka laini za simu za kiganjani milioni 2.96 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 27.45 Desemba mwaka jana.
Hayo yamebainishwa jana bungeni na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, wakati akisoma hotuba ya makadirio
ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Licha ya kuongezeka kwa watumiaji wa simu za kiganjani, lakini pia
watumiaji wa mfumo wa mawasiliano ya Intaneti, nao wameongezeka kutoka
milioni 3.56 mwaka 2008 hadi kufikia milioni 9.3 Desemba mwaka jana.
Waziri Mbarawa, alisema kuna ongezeko kubwa la huduma kupitia
mawasiliano ya simu ya kiganjani ambapo huduma hizo ni pamoja na
miamala ya kifedha ambayo ina watumiaji wapatao 12,330,962 na ununuzi
wa huduma na bidhaa kwa kutumia miamala ya kibenki.
“Hivi sasa, wananchi wanaweza kufanya malipo ya huduma mbalimbali
wanazozitumia kupitia simu za kiganjani ambapo katika kipindi cha Julai
2013 hadi 2014 jumla ya miamala 972,641,605 yenye thamani inayofikia
sh trilioni 28.3 imefanyika,” alisema Mbarawa.
Alibainisha kuwa maendeleo hayo yamesaidia kuokoa muda na kupunguza msongamano sehemu za kupatia huduma za kifedha.
Aliongeza kuwa kuongezeka kwa watumiaji wa mitandao kunaifanya wizara
hiyo iendelee kushawishi sekta binafsi kufikisha mawasiliano kwenye
maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Mbarawa alisema kutokana na juhudi hizo, kampuni za simu zimeridhia
kwa hiari kupeleka mawasiliano kwenye kata 163 kwa awamu ya kwanza “A”
na awamu ya kwanza “B”.
Alibainisha kuwa katika awamu ya kwanza “A” kampuni za simu
zitapeleka mawasiliano kwenye kata 44 na gharama zao na kata 33 kwa
ruzuku ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Alisema kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano
(TEHAMA), serikali inakamilisha utaratibu wa kuwezesha kufanya mikutano
kwa kutumia TEHAMA.
Chini ya mfumo huo, mikutano kutoka mkoa mmoja hadi mwingine itakuwa
ikifanyika kwa njia ya mtandao bila wahusika kuwapo ndani ya ukumbi
mmoja.
“Wizara inaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa matumizi ya TEHAMA
katika ofisi za serikali yanaongezeka, kwa sasa wizara imefunga mitambo
ya video 26 kwa ajili ya kuendesha vikao kwa njia ya mtandao. Hadi
kufikia Novemba mwaka 2013, mitambo 25 ilikuwa imefungwa katika makao
makuu ya mikoa 21,” alisema.
Alitaja ofisi zilizokwishafungwa mitambo hiyo kuwa ni Ofisi ya Waziri
Mkuu, Wizara ya Fedha na Uchumi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na TAMISEMI.
Alisema kuwa taratibu za kufunga mitambo hiyo katika makao makuu ya
mikoa mitano ya Zanzibar zimekamilika na inatarajiwa kufungwa mwishoni
mwa Juni 2014.
Hata hivyo, Mbarawa alisema pamoja na kuwepo kwa mafanikio ya TEHAMA,
wizara imeweka utaratibu wa usalama katika mitandao ya mawasiliano.
“Kutokana na mafanikio makubwa, hasa kufuatia kuongezeka kwa matumizi
ya TEHAMA ulimwenguni na kasi kubwa ya mabadiliko na matumizi ya
teknolojia ya mawasiliano, imeleta hofu kwa watumiaji kutokana na
kuongezeka kwa uharifu wa mitandao na uvunjifu wa maadili katika jamii.
Alisema kwa kutambua changamoto hizo, serikali inatarajia kutunga
sheria na kuanzisha kikosi maalumu cha kupambana na wahalifu katika
mtandao na kutoa elimu kwa wananchi.
NATanzania Daima
NATanzania Daima
0 comments:
Post a Comment