Saturday 2 August 2014

UKITAKA USALAMA KWENYE MAPENZI BASI USIFANYE HAYA MAKOSA


TUNAPENDA kuongozwa na fikra zetu. Kila mmoja anataka mwongozo wa maisha yake uendane na halmashauri ya ubongo wake. Hufanya hivyo, bila kujua kuwa kuna kikomo fulani ndani yake. Akili na matakwa ya moyo, wakati mwingine vinaweza kukupoteza.
Moyo unaweza kumpenda mchawi na ukawa huelewi kitu kwa chochote utakachoambiwa. Penzi la jambazi likikuingia, serikali ndiyo utaiona ni katili kwa sababu inamsaka mwenzi wako usiku na mchana. Hii ina maana kuwa mapenzi ni zaidi ya fikra za kila mtu.
Hutokea watu kuachana wakati bado wanapendana. Migogoro midogo inawafanya watengane, matokeo yake kila mmoja anabaki akiumia kivyake. Huo ni mfano mmoja kati ya mingi inayoonesha kwamba mapenzi yapo juu ya fikra za kawaida. Inahitaji utulivu wenye mashiko ya sayansi ya saikolojia.
Kuna ambao waliishi kwa mategemeo ya kuachana. Wakiamini wamechokana, matokeo yake kwenye ubongo wao wakatengeneza maneno: “Ipo siku.” Hata hivyo, miezi na miaka ikakatika mpaka wakazikana. Kumbe Mungu aliwaandikia wawe pamoja mpaka kifo ila wao hawakujua.
Dosari ya aina hiyo inatokana na wawili wanaopendana lakini upendo wao ukapofushwa na migogoro ya hapa na pale. Nasisitiza kuwa watu ni lazima wagundue mapema matatizo yao kabla ya kuhisi kwamba kati yao hakuna mapenzi. Vilevile, kila mmoja amuelewe mwenzi wake ni binadamu na siyo malaika.
Ana mapenzi naye, tena mapenzi makubwa. Hata hivyo, hiyo haimfanyi awe malaika. Ni binadamu, kwa hiyo wakati anadumisha mapenzi yake, anaweza kufanya makosa mengi. Jaribu kumvumilia kwa sababu ameumbwa na udhaifu, hajakamilika.
Baada ya utangulizi huo, ni vizuri kujua kuwa yapo makosa ambayo wengi huyafanya, tena mara nyingi bila kujua. Tunaishi nayo, matokeo yanakuwa ni mazoea. Hata hivyo, mara nyingi hutokea yanaharibu uhusiano ndiyo maana nimechagua tuyajadili. Yafuatayo ndiyo makosa yenyewe:

KULICHEZEA KAMARI PENZI LAKO NA MAISHA YAKO
Hapo ulipo hujawahi kuona mtu anapambana kuhakikisha mwenzi wake anabadilika tabia? Bila shaka tayari ulishajionea. Je, umejifunza nini kutoka kwao? Ni kweli kabisa kwamba mwenzi wako si malaika, kwa hiyo mnapokutana lazima mtatofautiana, je, ikitokea hamuendani kabisa?
Umejitahidi kumuweka kwenye mstari unaotaka lakini mwenzako haendi. Unasubiri nini? Kung’ang’ania penzi la mtu ambaye huendani naye, ni sawa na kuuchezea kamari moyo wako, vilevile ni sawa na kuyachezea karata tatu maisha yako.
Upo na mwenzi wako ambaye hakutoshelezi. Mnakutana mara nyingi lakini hakufikishi pale unapotaka upelekwe na mwandani wako. Unanyamaza tu kwa imani kuwa ipo siku ataweza, siku zinakwenda na mabadiliko hayaonekani. Unajipa matumaini kedekede kwamba kuna siku nyoka ataota miguu na jongoo atakuwa na macho.
Unakuwa na mpenzi ambaye kila siku anakupa visingizio ili msikutane faragha. Je, kwa nini usijiongeze kwamba mtu huyo hana hisia na wewe? Au, kwa nini usijiulize kama pengine mtu wako yupo kwenye uhusiano wa pembeni ambako anatoshelezewa mahitaji yake?
Tatizo kubwa ambalo inatakiwa lijulikane ni kwamba wengi wanapoingia kwenye uhusiano, hawapimi watu wao ni wazuri kwao kiasi gani. Wanavutwa na matamanio ya juu. Mvuto wa juu, huipumbaza akili na kudhani moyo unapenda kumbe ni uongo mtupu.
Mtu anaweza kudumu na mwenzi wake ambaye hamtoshelezi kwa miaka mingi. Anapumbazwa na mvuto wa juu, kwa hiyo anashindwa kuelewa mantiki ya muungano wa nyoyo. Zingatia kwamba mwenzi wako ambaye nyoyo zenu zimeungana, lazima atakuridhisha, naye ataridhika kwa huduma unayompa.
MFANO: Jayden Brown anatoa ushuhuda: “Nikifikiria uhusiano wangu uliopita nabaki najishangaa. Nilikuwa mbinafsi, nilikuwa naoneshwa upendo na wapenzi wangu lakini nilikuwa sitoi ukilinganisha na wao. Nilishangazwa na wanawake waliojitoa kwangu, wao waliamini kuna siku ningebadilika.
“Wanawake niliokuwa nao, walijipa matumaini kuwa ni muda tu, kipo kipindi ambacho kingefika na maisha yetu yangekuwa salama. Kumbe walichowaza wao, hakikuwa ndani ya akili yangu.
“Wao waliamini kwamba upo muda wa mabadiliko ya mimi kuwa mtu bora, ningebadilika kuwa mwema kwenye mapenzi, ningekuwa mpenzi bora. Kitu mapenzi juu yao hakikuwa ndani yangu kabisa.” 

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA