Wednesday 26 November 2014

JAJI WARIOBA AFUNGUKA,"KATIBA ILIYOPENDEKEZWA HAIFAI"



Baadhi ya wajumbe wa iliyokuwa tume ya mabadiliko ya katiba wameitaka serikali ichapishe kwa wingi na kuzisambaza kwa wananchi nakala za katiba pendekezwa, ili wananchi waisome, waitafakari na kuielewa kabla ya kuipigia kura ya maoni huku wakitahadharisha uwezekano wa nchi kuwa na katiba isiyokidhi matarajio na maslahi ya wananchi endapo wataipigia kura kabla ya kuisoma na kuiielewa.
 
Wakizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na mfuko wa Mwalimu Nyerere uliofanyika jijini Dar es Salaam, wajumbe hao akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo jaji mstaafu Joseph Warioba, wameelezea kutoridhishwa na tunu za taifa, haki za makundi mbalimbali kama vile watu wenye ulemavu, wanawake na watoto na baadhi ya vipengele kuondolewa.
 
Akizungumza katika mdahalo huo, aliyekuwa mjumbe wa tume Bw Hamfrey Polepole ametaka kuwepo maridhiano ya kikatiba kati ya pande mbili za muungano ili uwepo muungano unaokubaliwa, unaodumishwa na kulindwa kikatiba huku akieleza kusikitishwa na kitendo cha kufutwa kwa ibara muhimu zilizokuwa katika rasimu ya katiba na kushauri ibara hizo zirejeshwe kwani ndiyo msingi wa katiba inayozingatia maslahi ya wananchi na taifa imara.
 
Baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa waliohudhuria mdahalo huo na kupata fursa ya kuuliza maswali akiwemo Prof Ibrahimu Lipumba amesema katiba isiyozingatia maadili na kuweka bayana tunu za taifa haiwezi kuwa katiba bora itakayodumu kwa miaka mingi ijayo huku baadhi ya wananchi wakiomba ufafanuzi kwa baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye rasimu ya pili hasa kile kinachohusu madaraka ya rais.
 
Hata hivyo mdahalo huo umekuwa na ulinzi mkali wa polisi tofauti na midahalo mingine ambapo mwandishi  alishuhudia wahudhuriaji wakiwa wanakaguliwa na vifaa maalum kabla ya kuingia ndani.

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA