MBUNGE WA MUSOMA ,NIMROD MKONO ALISHWA SUMU
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono amelishwa sumu wakati akiwa kwenye safari ya kikazi jijini London nchini Uingereza, imeelezwa.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Citizen, Mkono ambaye pia ni mwanasheria maarufu, aliugua ghafla alipokuwa jijini humo.
Madaktari wake walisema kuwa alikuwa amelishwa sumu iliyokuwa imekusudiwa kuharibu figo zake ndani ya saa 72.
Madaktari wake walisema kuwa alikuwa amelishwa sumu iliyokuwa imekusudiwa kuharibu figo zake ndani ya saa 72.
“Ilikuwa siku mbili tangu niwasili London, nilianguka wakati nikifanya shughuli zilizonileta huku,” alisema na kuongeza:
“Nilijisikia vibaya na kupoteza kumbukumbu kwa takriban saa sita.”
Imeelezwa kuwa mbunge huyo alianza kutokwa jasho jingi ghafla kabla hajaanguka.
“Baada ya kuhudumiwa, madaktari wa London walisema sumu ilikuwa inaharibu figo yangu,” alisema.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, alikuwa ameonywa mapema kuwa muda mfupi kabla hajasafiri kwenda London anapaswa awe mwangalifu, pia asifikie kwenye hoteli zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kundi kutoka Tanzania, hivyo aliamua kufikia kwenye makazi yake jijini humo.
“Nilipokea meseji mbili kutoka kwa baadhi ya marafiki zangu wakinionya kuwa mwangalifu wakati wote,” alisema na kuongeza kuwa: “Nilikuwa nimeongozana na baadhi ya wabunge katika safari hiyo. Taarifa zinaeleza kuwa maofisa usalama wa kikosi cha upelelezi nchini Uingereza wameanza kulichunguza suala hilo.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema kuwa taarifa kuhusu tukio hilo zilishafikishwa ofisi za Bunge ingawa hakuna maelezo ya kutosha.
“Ninafahamu kuwa Mbunge Mkono alipata matatizo ya kiafya wakati akiwa London, lakini anaendelea vizuri…maelezo kuhusu ugonjwa wake unabaki siri kati ya Mkono na madaktari wake,” alisema.
Mkono alikuwa mshauri mkuu wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na Serikali dhidi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL na kwamba aliwahi kuziwakilisha kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) kabla ya mkataba wake kumalizika mwanzoni mwa mwaka huu.
Tanesco walikataa kusaini upya mkataba wa Mkono. Mbunge huyo anatajwa kuwa nyuma ya kuvuja kwa kashfa ya Escrow, kutokana na taarifa nyingi anazoweza kuwa anazifahamu kuhusu sakata hilo.
Julai mwaka huu, Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo alimtuhumu Mkono kutumia kashfa ya Escrow kumchafua, tuhuma ambazo Mkono anazikana.
Wiki chache baadaye, Spika alimtaka Mkono kueleza namna ambavyo aliishughulikia kesi ya IPTL na Standard Chartered Bank Hong Kong iliyokuwa imefunguliwa dhidi ya Tanesco na Serikali.
Mkono aliwasilisha taarifa kuhusu kuchotwa kwa Sh207 bilioni kwenye akaunti ya Escrow kutoka Benki Kuu ya Tanzania wakati ambapo kulikuwa kuna kesi nyingine inaendelea kwenye mahakama ya kimataifa.
Hatuwezi kuthibitisha kama kuna uhusiano wowote kati ya kulishwa sumu na kashfa ya Escrow. Mkono amekuwa akisema kuwa uchunguzi pekee ndiyo utakaoeleza ukweli.