WANACHUO WATELEKEZWA,WAZIRAI KWA NJAA,MMILIKI WAKE ATUMIA JUMA LA SUMAYE KUTAPELI
WANAFUNZI 46 wa chuo kipya cha kilimo na mifugo cha Nice Dream kilichopo Mtaa wa Mapelele, Kata ya Ilemi jijini Mbeya wamejikuta wakiwa katika wakati mgumu, baada ya kutelekezwa na uongozi wa chuo hicho, kiasi cha kushindwa kupata chakula kwa siku tano mfululizo, hali iliyosababisha baadhi yao kuzirai.
Hayo yameibuka baada ya uongozi wa chuo kudaiwa kuchukua ada za wanafunzi hao, wengi wakiwa kutoka mikoa ya Kagera na Mara ambao inaelezwa walitumiwa barua za kujiunga na chuo wakielezwa kuwa ni cha Serikali, ilhali sivyo.
Aidha, mmiliki wake ametajwa kujaribu kukipa hadhi chuo kwa kutangaza kuwa kimezinduliwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye naye amekana kukitambua chuo hicho.
Hayo yamebainishwa na Diwani wa Kata ya Ilemi, Furaha Mwandalima aliyesema alipokea malalamiko kutoka kwa wanachuo hao, naye kwenda kujionea hali halisi katika chuo hicho alichosema hakuwahi kukisikia.
Baada ya kuiona hali ilivyokuwa, alilazimika kumtafuta Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga aliyemshauri kutoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Norman Sigalla ili kupata mustakabali wa suala hilo.
Mwandishi wettu alifika chuoni hapo jana na kukuta baadhi ya wanafunzi wakiwa wamedhoofu, huku mmoja wao akiripotiwa kuzirai kwa kile kinachotajwa kuwa ni sababu ya njaa.
Hata hivyo, tatizo la njaa lilipata ufumbuzi wa muda baada ya wakazi wa maeneo ya jirani na chuo kuchanga fedha na kuanza kuwapikia wanafunzi hao.
Baadhi ya wananchi pia walionekana chuoni hapo wakiangua kilio kwa kuwahurumia wanafunzi hao walioonekana dhahiri kuchanganyikiwa na tukio la kutelekezwa kwao.
Mmoja wa wanafunzi hao, Joanes Renatus anayetoka mkoani Kagera, alisema alipokea barua na fomu ya kutaarifiwa kujiunga na chuo hicho baada ya matokeo ya kidato cha nne mwaka jana ikiambatanishwa na gharama za michango yenye jumla ya Sh 860,000.
Alisema barua hiyo ilikuwa ikisisitiza mwanafunzi anatakiwa kuripoti akiwa na karo ya muhula wa kwanza ambayo ni Sh 550,000 jambo ambalo alilitekeleza kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wenzake waliofika chuoni hapo Septemba mwaka huu.
Aliongeza kuwa, licha ya kutoka kwao akiwa na matumaini ya kupata chuo kizuri, alipofika chuoni baada ya safari ya zaidi ya kilometa 1,200 kutoka Kagera hadi Mbeya, alishangazwa kuona mazingira yasiyoashiria kuwa ni chuo alichopangiwa.
Na hata baada ya kutaka kujiridhisha, walibaini hakikuwa na usajili kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Wanafunzi wengine, Annaf Habibu kutoka Kagera na Mtani Ndelekule kutoka Mara, wakifafanua zaidi walisema baada ya kuripoti chuoni hapo, hawakukuta wanafunzi wengine na walipoulizia walijibiwa wamekwenda katika mafunzo ya vitendo, kumbe sivyo, lakini kadri muda ulivyozidi ikabainika kuwa wao walikuwa wanafunzi wa kwanza.
“Hatujui hatima yetu na tumetoka mbali kufuata elimu, lakini kumbe sivyo…inauma zaidi kwa sababu wazazi wetu wamelazimika kuuza mifugo na mashamba ili tusome, kumbe tunaishia katika mazingira haya…,” alisema Ndelekule huku akilengwalengwa machozi.
Aliongeza kuwa, kwa kuwa imeshajionesha hakuna dalili za wao kusoma chuoni hapo, ni vyema kama Serikali ikawasaidia kupata vyuo vingine ili watimize ndoto zao na pia kuwafuta `machozi’ wazazi wao.
Kutokana na adha hiyo, Diwani Mwandalimi alisema mwafaka uliofikiwa ni kutolewa kwa agizo la kuorodheshwa kwa majina ya wanafunzi na mahali wanakotoka ili kuwarudisha makwao na chuo kifungwe kutokana na kutosajiliwa rasmi na kwamba kilikuwa kinaendeshwa kijanja.
Balozi wa Mtaa wa Mapelele, Geophrey Mwalupindi na mkazi mwenzake Fanuel Kisanga walipoulizwa juu ya chuo hicho, walionesha kushangazwa na taarifa hizo, huku wakisema awali kilikuwa ni kituo cha kufundishia masomo ya ziada (twisheni) na shule ya chekechea.
Kati ya wanafunzi waliotapeliwa, 41 wanatokea Mkoa wa Kagera, wawili mkoani Mara, wawili wilayani Kyela mkoani Mbeya na mmoja akitokea Dar es Salaam.
Juhudi za kuupata uongozi wa chuo hicho haukufanikiwa kupitia namba za simu za mkononi walizoandika kwenye bango la chuo ambazo ni 0765659079 na 0684423849, kwani hazikupatikana hewani.
Uchunguzi pia umebaini malipo ya karo chuoni hapo yalikuwa yakipokelewa kwa ujanjaujanja na mtu aliyefahamika kama Samwel Daudi ambaye ni mmiliki wa chuo hicho na njia anazotumia kukusanyia ada kutoka kwa wanafunzi ambao hupeleka kwa Katibu Muhtasi wake na kutoa stakabadhi isiyokuwa na namba za usajili wa chuo wala namba za TRA.
Njia nyingine ambayo wanafunzi waliambiwa walipie ada zao ni kupitia njia ya M-Pesa ambapo mzazi alilazimika kutuma kwa wakala mwenye namba 98369 tofauti na kupokelewa kwa njia ya benki au simu ya uongozi.
Kama vile haitoshi, mmiliki wa chuo hicho alitumia mbinu zaidi ili kuwaaminisha wanafunzi na wazazi kuwa chuo hicho kimesajiliwa baada ya kuchora kibao kikionesha chuo hicho kilifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu mstaafu, Sumaye.
Hata hivyo, Mwandishi alipomtafuta Sumaye kuzungumzia anavyokifahamu chuo hicho kinachojinadi kimezinduliwa naye Oktoba 24, mwaka huu, alikana kuhusika nacho.
“Sijafika chuoni hapo na wala sikijui. Huyo aliyefanya hivyo ni tapeli, anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema akionekana kuguswa na tukio hilo.
Aliongeza kuwa, alialikwa kwa shughuli ya kanisa mjini Mbeya na akiwa huko alifuatwa na mmiliki wa chuo akimwomba kufungua chuo chake, lakini akakataa kwa kuwa alishapata taarifa za awali, hivyo kumshauri mmiliki huyo kukamilisha taratibu zinazotakiwa ndipo amwite kwa uzinduzi rasmi.