HIZI NDIZO MBINU ZA JINSI YA KUISHI NA MPENZI ANAEPENDA PESA.
Hapa tunazungumza kuhusu
mapenzi kama kawaida yetu. Leo nimekuja na mada ambayo naamini itawagusa wengi.
Marafiki zangu, kusaidia katika mapenzi ni jambo zuri tena lenye mantiki sana.
Suala la kusaidiana si la
upande mmoja. Linaweza kuwa kwa wote, kwa mwanaume au mwanamke. Ni kati ya
nguzo muhimu katika mapenzi, lakini kwa bahati mbaya kuna wale ambao wamekuwa
na tabia ya kupenda sana fedha!
Unajua wenzi wanajuana
kulingana na wanavyoishi, hivyo ni rahisi sana kumgundua mwenzako kama anapenda
sana fedha au ni kweli ana tatizo linalohitaji msaada wako. Hii ni kasoro,
lakini haimaanishi kwamba ndiyo sababu ya kuachana.
Katika mada hii ipo dawa ya
namna ya kudumu katika mapenzi motomoto na mwenzi wa aina hii. Imekuwa ni
kawaida kumsikia msichana akitamba mbele ya wasichana wenzake kwa kusema: “Mimi
nina kibuzi changu bwana kila ninachotaka kinanipa, kinajua kisiponipa nakitosa
tu, yaani nakichuna kama sina akili nzuri.”
Umewahi kukutana na maneno
ya aina hii? Bila shaka jibu ni ndiyo. Si hivyo tu, wapo wanaume pia ambao ni
kero kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea
kupewa kila kitu na wapenzi wao hata kama wanao uwezo wa kuvipata vitu hivyo
kama watajishughulisha.
Ninachotaka kusema leo ni
kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na fedha, ukiona mpenzi wako
anaweka fedha mbele na ukishindwa kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua
penzi lake lina walakini, hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.
Katika mapenzi hatukatai
suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida fulani akaomba umsaidie, kama
unao uwezo msaidie na kama huna mueleze ukweli kisha muangalie namna nyingine
ya kumsaidia.
Itakuwa siyo busara kama
utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba ukimweleza mpenzi wako ataona unamchuna.
Wapenzi wanaopendana kwa dhati hawachunani bali wanasaidiana na hili ni kwa
pande zote mbili.
Kinachokera ni kutoishiwa
na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna kwingine ni kwa mambo ya
starehe. Yaani sasa hivi umemuomba mpenzi wako vocha, hajakaa vizuri umemtaka
akija akuletee chipsi mayai, baadaye unataka akutoe ‘out’, bila kujali kwamba
wakati huo mpenzi wako ana fedha au laah.
Katika mazingira hayo
unadhani mpenzi wako atashindwa kukuchoka? Akikuacha kwa sababu hiyo utamlaumu?
Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya kutaka kukuomba fedha kila wakati tena
katika matumizi mengine ambayo siyo ya msingi, mbinu zifuatazo ni muhimu
kuzifuata. Twende tukaone.
MWELEZE UKWELI
Kama huna fedha wakati
mpenzi wako anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na kamwe usijaribu kutoa ahadi
ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza. Usiwe mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara
nitakununulia hiki na kile.
Mwanaume hatakiwi afahamike
siku ana fedha au hana. Maana kuna wenzangu ambao siku za mishahara
wanabadilisha hadi kutembea! Mwanamke akijua hilo naye ataongeza ‘mizinga’ ili
afaidi.
JENGENI KUSAIDIANA
Jambo la muhimu ambalo
wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa.
Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli ya basi analipa, wakati mpenzi wake
ana kazi yake.
Ifike wakati kwa makusudi,
mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua
namna fedha zinavyokuwa hazitoshi na ataweza kubana matumizi.
ACHA UFUJALI
Kuna wanaume wengine tangu
wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa fedha kwa kutoa ofa na zawadi
kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi wako kuwa unazo!
Unachotakiwa ni kudhibiti
mapema matumizi yako hata kama fedha itakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa
hakushibishi uhitaji, kadiri unavyotoa ndivyo unavyoongeza mahitaji. Weka maisha
yako katikati usijidai tajiri kumbe ni kapuku tu.
BAKI NA HILI
Katika kumalizia niseme tu
kwamba, mapenzi si kukomoana, bali kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia
mwenzako ili siku na wewe ukiwa na tatizo akusaidie.
Kitu unachotakiwa kukiepuka
ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga mizinga mpenzi wako kila
mara kunapunguza mapenzi hivyo epukana na tabia hiyo.
Niseme nini tena marafiki
zangu. Kwa leo hebu bakini na hili, uhakikishe unasoma ukurasa huu kila
siku, nitakuja na mada moja nzuri sana.
0 comments:
Post a Comment