Wanaume Wadaiwa Kuwa Chanzo cha Mmomonyoko wa Maadili
.
TATIZO la kuporomoka kwa maadili ndani ya jamii ni kutokana na wanaume wengi kushindwa kutimiza wajibu wao ndani ya familia na jamii.
Kauli
hiyo ilitolewa juzi na Dk Chris Mauki, Mshauri wa Saikolojia na
Mahusiano, ambaye pia ni Mhadhiri wa somo la Saikolojia Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, wakati wa semina ya kinababa iliyofanyika katika Ukumbi
wa Makane uliopo Mkuranga, Mkoa wa Pwani.
Dk
Mauki alisema mmomonyoko wa maadili unaotokea katika jamii yetu
unasababishwa na wanaume kushindwa kutimiza wajibu wao kama wazazi na
kuwaachia wanawake majukumu yote ambayo mengine yalipaswa yatimizwe na
wanaume.
“Mmomonyoko
wa maadili katika jamii ni matokeo ya wanaume kutowajibika kama wazazi
na badala yake majukumu yao wameyatelekeza kwa wanawake.
“Wanawake
wamekuwa na kazi nyingi kiasi kwamba wanazidiwa na hivyo kushindwa
kudhibiti mwenendo wa maadili ya watoto wao ipasavyo,” alisema Dk Mauki.
Aliendelea
kusema wanaume wengi wamekuwa na tabia ya kutelekeza familia zao na
kutokomea pasipojulikana na kuwaachia wanawake mzigo mkubwa wa kutunza
na kulea familia peke yao.
“Familia
nyingi zinapokumbana na matatizo ambayo ni ya kawaida katika maisha ya
binadamu kama maradhi, ulemavu au ugumu wa maisha, wanaume hushindwa
kuwa wastahimilivu na hivyo huamua kutelekeza familia zao na kutokomea
kusikojulikana,” alisema Dk Mauki.
Akirejea
majukumu ya wanaume katika jamii, alisema wanaume ndio wasimamizi wa
kila kitu katika familia, walezi, washauri, walinzi na watoaji wa
mahitaji muhimu katika familia zao.
“Siku
hizi wanawake wamekuwa ndio walezi wakubwa wa familia, kazi ambayo
ilipaswa ifanywe na wanaume. Wanawake walipaswa kuwa walezi wa
kisaikolojia na sio wahangaikaji wa kutafuta na kutunza familia, hii
ilikuwa ni kazi ya wanaume,” alisema Dk Mauki.
Akifungua
semina hiyo, Mchungaji Debora Lusambi wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kongowe, alisema kanisa liliamua
kuandaa semina hiyo kwa wanaume kwani wanaume wameonekana kushindwa
kutimiza wajibu wao ukilinganisha na wanawake.
“Kanisa
limeona wanaume huingia kwenye ndoa bila ya kuwa na mafunzo yoyote
ukilinganisha na wanawake ambao kabla ya ndoa hupata kufundwa maarufu
kama ‘kitchen party’ na kumuaga binti yao ambayo hujulikana kama ‘send
off’, vitu ambavyo huwasaidia kuwa walezi na wavumilivu katika ndoa
zao.
“Hivyo
tumeona ili kupunguza kuporomoka kwa maadili, ni lazima wanaume nao
wapate mafunzo, watambue wajibu wao katika familia na jamii kwa ujumla,”
alisema Mchungaji Lusambi.
--MPEKUZI
0 comments:
Post a Comment