Monday, 3 June 2024

MPANGILIO WA MLO NA MAZOEZI KATIKA KUPUNGUZA UZITO WA MWILI



Na Dkt. Ngaillah

 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania hivi karibuni imeeleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanasababisha vifo kati ya asilimia 40 hadi 45 ya vifo vyote vinavyotokea hospitalini, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 33 miaka mitano iliyopita.

Kutokana na hali hiyo, wizara imeshauri hatua mbalimbali za kuchukuliwa ili kukabiliana na kasi ya ongezeko la vifo hivyo ambapo miongoni mwa hatua hizo ni kupunguza ulaji wa vyakula vya mafuta, chumvi nyingi, unywaji wa pombe na kufanya mazoezi.

Kutokana na msingi huo, tumefanya mahojiano na Dkt. Hussein Ngaillah kutoka Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma kuhusu nafasi ya diet (ulaji chakula) na ufanyaji mazoezi katika kuwezesha watu kupunguza uzito.

Mambo tuliyozungumza ni pamoja na;

Nafasi ya Diet katika kupunguza uzito

Kwa lugha nyepesi Dkt. Ngailllah amesema kuwa diet ni namna fulani ya ulaji wa vyakula ikiwa lengo kuu ni kupunguza uzito. Ameeleza kuwa diet ina nafasi kwenye kupunguza uzito kwa sababu msingi mkubwa ni kupunguza kiwango cha vyakula hasa vya wanga na kuruhusu mwili kutumia mafuta kama chanzo cha nishati. Kwa mantiki hiyo, mafuta ambayo ndiyo yanasababisha uzito mwilini yanapungua.

Je diet inafanya kazi? Jibu ni ndio, inafanya kazi. ndani ya miezi 3-6, unakuwa umepungua uzito.

Kuna mmoja katika wazungumzaji aliwahi kusema kwama “hatuli hadi tuwe na njaa na tukila hatushibi.” Maana yake wanakula kiwango cha chakula kile tu ambacho kinahitajika ili kuupa mwili nguvu. Wajuzi wa mambo wanashauri kuwe na ratiba ya kula, kwa siku isizidi milo mitano, kwa asubuhi, mchana na jioni na inayokuwa ya kutafuna vyakula vyepesi baina ya milo hiyo na hupaswi kula chochote katikati ya hiyo.

Pia hupaswi kuvukisha kifungua kinywa (breakfast) na hupaswi kula usiku sana muda wa mwili kulala. Mlo wako wa asubuhi uwe unaeleweka, wenyewe huita chai nzito, halafu mchana unakula kawaida na jioni chakula chepesi.

Vyakula vya kupunguza uzito

Dkt. Ngailllah ameelekeza kuwa vyakula vinavyopaswa kuliwa na mtu unayetaka kupungua uzito ni, 1). vyakula vya protini, matunda, mboga za majani, vyakula vya jamii ya kunde, karanga na mbegu, 2). Nafaka ambazo hazijakobolewa, kupunguza matumizi ya sukari na soda, 3). Kula mafuta ya mimea na kupunguza mafuta ya wanyama, 4.) Kula vyakula ambavyo huchelewa kumeng’enywa na kukufanya ukae kwa mda mrefu bila kusikia njaa na 5). Maji safi na salama.

Mazoezi ya kupunguza uzito

Wataalamu wanashauri kwa uchache mtu atumie dakika 150 kwa wiki kwa mazoezi mepesi na dakika 75 kwa mazoezi magumu. Na haya yanaweza kuwa kukimbia, kutembea mwendo wa haraka, kucheza muziki, kuruka kamba, kuogelea, kuendesha baiskeli au kuinua vitu vizito. Lengo ni jasho litoke, na mtu afanye mazoezi yale anayoyaweza kila siku kwa dakika 15 hadi dakika 30, afurahie mazoezi na asione kama adhabu.

Diet na mazoezi, ipi njia bora kupunguza uzito?

Kulijibu hili swali, nitakupa mfano, amesema Ngaillah, ukiacha hawa Wamasai waliopo mijini, ukienda kule umasaini hauwezi kukuta Mmasai anakitambi au bwanyenye, au kuna kabila fulani hivi dogo liko Pakistani milimani kule, hutawakuta wamenenepeana.

Siku zote wana miili fulani hivi, tunaiita mti mkavu. Kwanini? Kwa sababu muda mwingi wanatumia kikimbizana na wanyama, kupandisha milima kwa wale wa Pakistani kule, hayo ni mazoezi. Kila siku wanachoma mafuta mwilini na hakuna ziada inayobaki kuwafanya wanenepe kiholela, na hiyo ni kutokana na kuwa hawapati mafuta ya ziada jambo linalochangiwa na vyakula pamoja na ratiba za kula.

Watu hao wanakula vyakula vya kambakamba, vyakula asili na bila mafuta. Kwa hiyo, diet na mazoezi yanaenda bega kwa bega linapokuja suala la kupungua uzito hasa mazoezi.

Aidha, amesema kuwa diet pekee siyo njia bora sana kwa sababu, unaunyima mwili chakula ambacho kinaufanya ufanye kazi, pamoja baadhi ya madini na vitamini na kusababisha baadhi ya seli kuharibika. Ameongeza kuwa diet siyo njia endelevu kwani pindi mtu akisitisha anaweza kurudi kwenye kunenepa tena.

Kutokana na hayo ameshauri kuwa mtu anayetaka kupungua uzito abadili namna ya ulaji wake, ale vyakula asili, apunguze vyakula vya mafuta, afanye mazoezi, apate usingizi bora wa saa zisizopungua saba. Pia ameshauri mhusika aboreshe afya ya akili, aweze kudhibiti hofu na msongo wa mawazo.

  1 comment:

  1. Tunahitaji food schedule kabisa kuweza kufanya hili

    ReplyDelete

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA