Sunday 17 July 2016

UTUNZAJI BORA WA TAKA NGUMU MAJUMBANI UNA FAIDA ZAKE



Na Rose Riwa
Habari wasomaji wa tovuti hii, natumai hamjambo na ni wazima wa afya. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutupa uzima  na afya mpaka muda huu. Taka/ uchafu zimekuwa  zikizagaa katika maeneo mbalimbali  katika mazingira yetu  na kuchafua mazingira  pia kusababisha milipuko ya magonjwa ya kuambukizwa husasani katika kipindi cha mvua, pia uchafu umekuwa ni chanzo cha ugonjwa wa malaria ambao umekuwa ukihatarisha afya za  watanzania hususani watoto wadogo na mama wajawazito. 

Kutokana na hali hiyo serikali kwa kushirikina na wadau  mbalimbali wamekuwa wakitenga bajeti kubwa  na kujikita katika kuzuia magonjwa  mbalimbali yatokanayo na uchafuzi wa mazingira na pia kutenga mafungu kwenye halmashauri ili kusafisha miji na kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama.

 Lakini leo napenda tuangalie takataka kwa jicho la pili, tusiishie tu  kuuona uchafu na kuuchukia bila kuchukua hatua stahiki katika utunzaji wa taka katika ngazi ya familia. Na mada ya leo itajikita katika njia mbalimbali za kupunguza, kutumia na kutunza uchafu katika mazingira ya majumbani kwetu.

Kuna aina kuu tatu za taka na mada hii itazungumzia  aina  mojawapo inayoitwa taka ngumu (solid waste) zinazozalishwa kutokana na shughuli mbalimbali za majumbani. Taka ngumu majumbani ni sehemu ya maisha yetu, hatuwezi kuishi bila kutengeneza taka katika maisha ya kila siku. Hivyo basi ni muhimu kutumia na kutunza taka hizo vizuri ili kuepuka uchafuzi wa mazigira, milipuko ya magonjwa mbalimbali na kufanya mazingira ya nyumba  na mitaa yetu kupendeza na kuvutia. Lakini pia taka hazina tu hasara kama wengi tunavyozifikiria,  kama zitatunzwa na kutumiwa kwa usahihi zinaweza kuwa ni suluhisho la nishati katika nyumba zetu hivyo kuongeza kipato cha familia, kupunguza gharama za kununua nishati  na gharama za utapaji wa taka hizo .Katika nchi zilizoendelea taka ni moja wapo ya malighafi kama malighafi nyingine ambazo zinaingizia mataifa hayo kipato kikubwa  kinachotumika katika shughuli za maendeleo. Kwa hiyo hata Tanzania tunaweza kupata faida mbalimbali za taka kama tutafanya yafuatayo:-

1. Kutunza  vizuri taka ambazo zinaweza kutumiwa kama malighafi kutengeneza bidhaa nyingine kama vile chupa ya plastics na vyuma chakavu aina mbalimbali na unaweza kuviuza au kugawa kwa watu waliojiajiri/walioajiriwa (scavengers) kwa ajili ya kukusanya malighafi hii na kutegeneza bidhaa mbalimbali hii pia huongeza kipato kwa watu waliojiajiri au waliojiriwa katika sekta hiyo,kukupatia kipato wewe mwenyewe kama utaziuza na vilevile hupunguza kwa kiwango kikubwa kiwango cha uchafu  kinachozalishwa nyumbani.

2. Kutumia uchafu unaowahi kuharibika (decomposable waste) mfano mabaki ya chakula kuzalisha gesi asilia kwa matumizi ya nishati ya nyumbani ,kupunguza taka zinazozalishwa nyumbani na kutumia kama mbadala wa nishati nyumbani hivyo kuokoa kiwango cha pesa nyingi ambazo tunazitumia kila siku kwa ajili ya matumizi ya nishati  mkaa, kuni  na umeme. 

3. Tumia vihifadhio(packaging material) imara pale unapoenda sokoni au kununua mahitaji mbalimbali ya nyumbani, vihifadhio hivyo maalumu kama vile vikapu vimetengenezwa kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu na vinadumu hivyo kupunguza uchafu wa mifuko inayotumika kwa mara moja.

4.  Ikiwa utamudu,  ni vizuri pia ukanunua bidhaa kubwa itakayotumika kwa muda mrefu kulingana na matumizi yako kama vile dumu kubwa la sabuni za maji ili kuepuka kununua madumu madogodogo   mara kwa mara hivyo kupunguza uchafu katika nyumba yako.

5. kupika chakula nyumbani kunapunguza kiwango cha mabaki ya vifungashio vya chakula kinachonunuliwa kwenye  karatasi maalum maarufu kama aluminium (foil papers)  au mifuko ya plastiki maarufu inayotumika kufungia chips na vyakula vingine hivyo kupunguza kiwango cha uchafu nyumbani kwako.

6. Kuchemsha maji ya kunywa nyumbani kunatukupunguzia  uchafu wa makopo/chupa za plastiki za maji zinazonunuliwa kila siku hivyo kutupunguza mlundikano wa uchafu nyumbani kwako.

7. Nunua bidhaa zenye uwezo wa kukaa muda mrefu (durable products) ili kuepuka kununua bidhaa hizo mara kwa mara na kwa kufanya hivyo utapunguza gharama za maisha na kupunguza uchafu utokanao na mabaki ya bidhaa hizo mara baada ya matumizi.

8. Kutengeneza(repair) vifaa mbalimbali vinavyotumika nyumbani kama kunauwekano wa kufanya hivyo na kama hautaathiri usalama wa matumizi wa kifaa hicho ili kitumike kwa muda mrefu na kuepuka kununua vifaa vingine ili kudhibiti ongezeko la uchafu katika nyumba yako.

9. Unaweza kutumia tena mabaki ya bidhaa zilizochakaa kwa kazi nyingine badala ya kutupa kama vile kutumia ndoo iliyopasuka kupandia maua na kupendezesha nyumba yako badala ya kuitupa na kuwa kuongeza uchafu.

10. Kama utatumia mifuko kubeba au kuhifadhia bidhaa mbalimbali , nunua mifuko migumu ambayo inaweza kutumika zaidi ya mara moja ili kuepuka mlundikano wa mifuko inayotupwa kila siku baada ya matumizi ya mara moja.

11. Karatasi zilizochapishwa upande mmoja zinaweza pia kutumika upande wa pili kwa watoto wadogo kuchora au kufanyia shughuli nyingine zenye uwezo wa kuchangamsha akili zao kabla hazijatupwa  na hivyo kufanya zitumike muda mrefu  na kupunguza uwezekano wa kununua mpya kwa matumizi hayo.

Hivyo taka ngumu ikiwa zitatunzwa na kuhifadhiwa vizuri zinaweza kuleta faida  za kiuchumi na  kiafya katika jamii husika, ni jukumu la kila mmjoja kuhakikisha anaishi katika mazingira safi na salama kwa mustakabari wa  afya  zetu .

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA