Wednesday, 15 June 2016

HUMPENDI? KWA NINI UZAE NAYE?



Katika jamii tunayoishi kuna mambo mengi yanayoendelea ambayo huonyesha jinsi gani wawili walivyohusiana kimapenzi, lakini hujitokeza baada ya mapenzi yao kuharibika. Utamaduni au mazoea ya uhusiano wa kimapenzi kwa jamii yetu yanaonyesha kuwa wawili wanapotofautiana, huanza kutoleana maneno yasiyostahili.

Watu kuzaa bila ndoa siku hizi linaonekana kuwa ni jambo la kawaida na hii inatokana na mfumo wetu wa maisha, kwani wapo ambao walijaribu maisha ya ndoa, lakini mambo yakawa magumu kutokana na vipigo, manyanyaso na mateso mengine mengi.Cha ajabu asilimia kubwa ya wazazi hawa, wamekuwa wakitoa kauli kwamba hawawapendi wenza wao japokuwa walizaa, kauli ambazo naamini siyo sawa.
Utakuta mwanamke akisema; “Ohoo! Simpendi yule mwanaume kama nini, basi tu ilitokea nikazaa naye.” Sidhani kama maneno haya yana mbolea kwa sababu ni jambo la kawaida mtu kuridhika urafiki unapovunjika kwa sababu ni jambo la kawaida. Hata wanawake hawatakiwi kueleza kwa staili hiyo kwa sababu wakati wakiwa kwenye uhusiano, kila kitu kilikwenda sawa.
Suala la kuzaa hakuna bahati  mbaya, watu huwa wanajifariji tu lakini cha msingi ni kwamba mpaka unaamua kuzaa na mtu tambua kwamba ulimpenda na umekubaliana na hali yoyote itakayojitokeza katika maisha ya kumlea mtoto wenu.
Ninavyojua, kama mtu anashiriki mapenzi na mtu asiyempenda, huchukua tahadhari nyingi ili kuhakikisha suala la ujauzito halitokei. Maana wengine hujikuta wakishiriki na mtu kwa sababu tu ya shida ya wakati huo, kama vile ugumu wa maisha, shinikizo la kazi, kesi au vingine.
Kama unashiriki na mtu kwa staili hii, zipo njia za kujihami kuhakikisha ujauzito hautokei, kama vile kutumia kinga na mara nyingi mapenzi ya namna hii huwa ya muda mfupi, labda kama ni kubakwa.Kwa maana hiyo, suala la kuzaa na mtu usiyempenda halipo. Kutoa maneno hayo ni kama kuwapa mkosi watoto au mtoto mliyezaa ambaye anatambua kuwa wazazi wake ni watu waliopendana.
Kitu cha msingi ni kwa wapenzi ni kutambua kuwa katika mapenzi, kutengana ni jambo la kawaida kabisa katika jamii zote duniani. Hakuna ajabu yoyote kwa jambo hili na kwa sababu hiyo, ni jambo la kushangaza kumkuta mmoja wa wapenzi waliopendana hadi kuzaa, eti leo akilalamika kuwa hakumpenda mwenzake!

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA