Tuesday, 4 August 2015

BURUNDI: HALI YA WASIWASI YATANDA BUJUMBURA

Pierre-Claver Mbonimpa, mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Burundi, alizuiliwa jela kwa zaidi ya miezi minne. Hapa ni wakati alipokua Mahakamani akisubiri kusikilizwa, Julai 4 mwaka 2014.

Mwanaharakati wa haki za binadamu akiwa pia kiongozi wa shirika linalotetea haki za binadamu na za wafungwa APRODH, Pierre-Claver Mbonimpa ameponea kuuawa baada ya kujeruhiwa kwa risasi alizovyatuliwa na mtu aliyekuwa kwenye pikipiki katika kata ya Kanga wilayani Kinama, Kaskazini mwa jiji la Bujumbura.
Hali ya wasiwasi imetanda katika mji wa Bujumbura na wakaazi wa mji huo wameingiliwa na hofu baada ya kusikia tukio hilo.
Uvumi wa kuuawa kwa Pierre-Claver Mbonimpa ulianza kuzagaa tangu Jumapili Agost 2 nchini Burundi. Lakini Jumatatu mchana wiki hii, mwanaharakati huyo amekanusha taarifa hiyo.
Saa zisiozidi nne baadae, yaani saa 12 na robo, mtu aliye kuwa kwenye pikipiki amemfyatulia risasi Pierre-Claver Mbonimpa wakati alipokua akirudi nyubani katika kata ya Carama wilayani Kinama, Kaskazini mwa jiji la Bujumbura.
Pacifique Nininahazwe, mmoja kati ya wanaharakati wa mashirika ya kiraia akiwa pia kiongozi wa muungano wa mashirika ya kiraia FOCODE, yanayopinga muhula wa tatu wa Pierre Nkurunziza, ametoa wito wa kuzidisha ulinza katika hospitali ya Polyclinique Centrale de Bujumbura anakolazwa Pierre-Claver Mbonimpa, akisema anahofu huenda mwanaharakati huyo akamaliziwa maisha.
Balozi wa Marekani amewasili katika hospitali anakolazwa Pierre-Claver Mbonimpa, huku akielezea masikitiko yake kuona mauaji yamekua sugu nchini Burundi, hususan katika mji mkuu wa Bujumbura.
Hayo yanajiri wakati hali ya wasiwasi imetanda mjini Bujumbura na katika vitongoji vyake. Hali hii inatokea wakati katika hotuba yake Jumapili jioni baada ya kifo cha mkuu wa zamani wa Idara ya Ujasusi, jenerali Adolphe Nshimirimana mapema jumapili asubuhi, rais wa Burundi Pierre Nkurunziza aliwatolea wito raia kuwa watulivu na kujizuia na chochote kile ambacho kinaweza kuchochea chuki na machafuko.
Hata hivyo milio ya risasi imeendelea kusikika Jumatatu jioni wiki hii katika wilaya ziliyokuwa za waandamanaji hususan Nyakabiga, Cibitoke na Bwiza. Mpaka sasa haijajulikana hasara iliotokea.
Jumapili asubuhi afisa mwengine wa Idara ya Ujasusi wilayani Musaga, aliuawa nyumbani kwake na watu wasiojulikana. Mauaji yamekithiri nchini Burundi, ambapo mauaji yamekua yakishuhudiwa kila kukicha.
Na RFI

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA