TAIFA STARS YAANZA KUJINOA KWA AJILI YA NIGERIA
Na Saleh Ally, Kartepe
KIKOSI cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars kimesafiri kwa zaidi ya saa 10 hadi katika mji mdogo kabisa wa Kartepe hapa nchini Uturuki kwa ajili ya kuweka kambi.
Kambi hiyo ni kwa ajili ya kujiwinda ili kuwa fiti kabla ya mechi ya kuwania kucheza Kombe la Mataifa aAfrika dhidi ya Nigeria, mechi itakayopigwa Septemba 5 jijini Dar es Salaam.
Kabla haitakuwa mechi ndogo na Stars ambayo kwa mara ya kwanza, mara nyingine timu hiyo inanilewa na makocha wote wazalendo.
Safari:
Safari ya Stars kuja hapa Uturuki ilianzia Dar es Salaam na ndege iliondoka saa 9:45 usiku na kuwasili Istanbul Uturuki saa 4:45 asubuhi ikiwa ni saa saba bila ya kupumzika angani.
Safari hiyo ndeefu iliwafanya wachezaji wa Stars kuonekana wakiwa wamechoka sana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ataturk na baada ya hapo safari ya kwenda kambini iliyochukua saa tatu na shee ilianza kwa basi.
Awali ilionekana ni kama safari fupi tu, lakini haikuwa hivyo baada ya wachezaji kujikuta wakisafiri kwa saa tatu kutoka Istanbul hadi katika mji wa Izmil ambao ni wa tatu kwa ukubwa hapa Uturuki baada ya Istanbul na Ankara.
Kambi:
Bado Stars hawahaweka kambi mjini, badala yake wamepanda katika milima iliyo nje ya mji huo katika eneo linalojulikana kama Kartepe ambako kambi hiyo iko katika Hoteli kubwa ya The Green Park.
Kwa Dar es Salaam, The Green Park Hotel ni mfano wa Serena Hoteli, lakini hii ya hapa Uturuki ni kubwa mara tatu ya Serena.
Ina uwezo wa kupokea timu 11 hadi 14 kwa wakati mmoja. Ni hoteli ya kisasa ambayo inajumuisha nyumba maalum za kupanga maarufu kama apartment.
Hoteli hiyo inamiliki viwanja vitano vya kisasa vya mazoezi ambavyo timu mbalimbali zinazifokia hapa zinavitumia kwa ajili ya kujiweka sawa.
Wakati Stars inawasili katika kambi hiyo, timu ya taifa ya Bahrain ndiyo ilikuwa inaondoka. Lakini timu ya taifa ya Jordan na Libya zilikuwa ni kati ya timu zilizoweka kambi pia kulikuwa na klabu ya Al Ana’aa ya Libya ambayo pia ilikuwa hapa kwa ajili ya kujiandaa.
Kila wakati wa mazoezi uliopangwa na mwalimu, mabasi yamekuwa yakifika kuwachukua wachezaji na makocha pia kuwarudisha.
Kinachovutia zaidi, viwanja hivyo vimekuwa vikitumiwa kwa muda. Mfano kama umepangiwa kuanza saa 5 asubuhi, basi hadi saa 6:30 utatakiwa kung’oa virago na kuwapisha wengine.
Hali ya Hewa:
Hali ya hewa ya hapa ni kiboko, baridi ni kali kwa kuwa ni kuanzia nyuzi joto 12 hadi 14. Siku moja kabla ya Stars kuwasili, mvua zilinyesha mfululizo kwa saa 72.
Lakini tokea timu imewasili hali ya hewa si ya mvua tena, lakini baridi na hasa unapowadia usiku, inakuwa kali zaidi.
Kocha Charles Boniface Mkwasa na msaidizi wake, Hemed Morocco pamoja na mshauri wa masuala ya ufundi, Abdallah ‘King’ Kibadeni wanaonekana kuifurahia hali hiyo huku kila mmoja akisema wana imani mambi yatakuwa mazuri zaidi.
Benchi la ufundi la Stars linaamini mazoezi kwenye baridi ni bora kuliko kwenye joto ingaw atimu italazimika kurejea Septemba Mosi ili kuzoea tena hali ya hewa ya Dar es Salaam.
Jana, Stars ilijifua mara mbili, lakini leo itajifua mara moja tu asubuhi, jioni wachezaji watapumzika kwa ajili ya mechi ya kesho dhidi ya Libya ambayo itachezwa saa tano asubuhi.
Mkwasa amesema anapambana kuhakikisha wanaitumia mechi hiyo kama faida kwa Libya wana kikosi bora pia na watatoa msaada yeye na wenzake kujua wapi pa kufanyia kazi.
0 comments:
Post a Comment