MAGUFULI NA KAMPENI ZA KUJIKOSOA, NAMFANANISHA NA MWALIMU NYERERE NA KAULI YA TUJISAHIHISHE
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Tiketi ya CCM Dkt John Pombe Magufuli |
Na Humphrey Pole Pole
Kumekuwa na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu mgombea Urais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia CCM, Dr. John Pombe
Magufuli, kuibua na kuzungumzia mapungufu ya serikali ambayo yeye ni
waziri. Baadhi ya watu wanaofuatilia kampeni zake wameenda mbali zaidi
na kuhisi kuwa kwa kufanya hivyo, Magufuli anawafanyia kampeni labda
bila yeye kujua wapinzani wake katika kinyang’anyiro cha Urais.
Bila shaka, kwa watu wenye mtizamo huo, kampeni za Magufuli zingekuwa
zinatawaliwa na maneno yaliyoyajaa sifa nzuri za utendaji wa serikali
na chama tawala. Kwa hiyo, kwa mtizamo huo, ni jambo la kushangaza kuona
kuwa Magufuli anakosoa serikali aliyomo badala ya kuisifia na kuipamba
majukwani. Kwa sababu hiyo, baadhi ya watu wanasema kuwa Magufuli
anazungumza kama vile anagombea kupitia vyama vya upinzani.
Maoni ya namna hii pia yamekuwa yakielekezwa kwa katibu mkuu wa CCM,
Ndg. Abdulrahaman Kinana, ambaye katika shughuli zake za kisiasa za
chama chake katika maeneo mbalimbali hapa nchini amesikika mara nyingi
akiikosoa serikali ya chama ambacho yeye ni katibu mkuu. Watanzania
watakumbuka kuwa Ndg. Kinana aliwahi kuwaita baadhi ya mawaziri wa
serikali hii 'mizigo' na kutaka wawajibishwe kwa kushindwa kutimiza
wajibu wao kwa ufanisi. Kwa baadhi ya watu Ndg. Kinana hakufanya vizuri
kuikosoa serikali yake hadharani na hasa kwa kuongea kama mpinzani.
Kitendo cha Magufuli na viongozi wa chama chake kuibua mapungufu na
kuikosoa serikali yao hadharani inaonekana kama ni lugha ya wapinzani wa
kisiasa. Hakika utamaduni huo ni sawa na kujikosoa mwenyewe. Hata
hivyo, ili tuweze kuelewa kama kujikosoa ni jukumu pekee la vyama vya
upinzani na wagombea wao, inabidi tujiruhusu kuelimishwa na maneno ya
hekima aliyekuwa Rais na mpigania uhuru wa Guinea Bissau, kamarade,
Amilcar Cabral ambaye alishawahi kusema kuwa kwa kiongozi au anayetaka
kuwa kiongozi wa umma sharti awe na mwenendo wa kutoficha ukweli: Kwa
maneno yake;
"Hide nothing from the masses of our people.Tell no
lies.Expose lies whenever they are told. Mask no difficulties, mistakes,
failures. Claim no easy victories."
Tafsiri yake ni kuwa,
kiongozi asifiche chochote kwa wananchi. asiseme uongo, afichue uongo
kila unapoibuka. Asifiche matatizo, makosa, mapungufu na kushindwa.
Asijipe sifa nyepesi nyepesi.” Kutokana na hekima ya Amilcar Cabral
ilivyoelezwa hapo juu, ni wazi kuwa anachofanya Magufuli ndicho haswa
kinachotakiwa kufanyika. Kwa kufanya hivyo, Magufuli anaonyesha wazi
kuwa anajua matatizo na mapungufu yaliyopo na badala ya kuyafunika na
kuyapaka rangi anayaweka wazi. Bahati nzuri Magufuli amekuwa akielezea
namna atakavyoshughulikia hayo matatizo na mapungufu. Bahati nzuri
tabia hii ya Magufuli siyo mpya. Watanzania watakumbuka kuwa hulka hii
ya Magufuli ilijionyesha wakati hata alipokuwa waziri chini ya Rais
Benjamin Mkapa alipoikosoa Ofisi yake hadharani kwa baadhi ya watumishi
wa ofisi hiyo kujimilikishia magari ya umma isivyo halali. Katika
kipindi hiki cha kampeni, Magufuli amekuwa akitoa mapungufu ya serikali
hata pale ambapo Rais Kikwete yupo.
Sambamba na Amilcar Cabral,
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuandika kitabu mwaka
1962 kiitwacho "Tujisahihishe" akitaka Watanzania na hasa viongozi wawe
tayari muda wote kujisahihisha. Katika kitabu hicho Baba wa Taifa,
alisema kuwa “makosa ni makosa bila kujali ni nani ameyafanya. Muhimu ni
kuyajua makosa hayo na kujisahihisha.” Katika kitabu hicho, Mwalimu
Nyerere aliendelea kusema;
“Kujielimisha ni kujua ukweli wa
mambo na kuwa na ujuzi wa sababu mbalimbali za mambo; na kama mambo hayo
ni mabaya ni kujua jinsi ya kuyaondoa; na kama ni mema, jinsi ya
kuyadumisha. Mpumbavu ni yule anayeyapa mambo sababu zisizo za kweli na
kushauri dawa isiyo ya kweli katika kutafuta sababu za matatizo na
jinsi ya kuyaondoa(Nyerere, 1962, 5).”
Kwa maelezo hayo ya Baba
wa Taifa, ni wazi kuwa Magufuli ameamua kuwa mkweli katika kampeni zake
na ameepuka kuwa mpumbavu kama alivyobainisha Baba wa Taifa.
Kujikosoa anakofanya Magufuli kunadhihirisha aina ya Rais
tunayemhitaji. Itakuwa ni hatari kubwa kuwa na Rais asiyetayari
kujikosoa au kukosolewa. Ni janga kubwa kwa nchi kuwa na Rais ambaye
anaamini kuwa yeye ni mtakatifu asiyekosea. Rais wa namna hiyo ni lazima
atakuwa ni dikteta na watakodhubutu kumkosoa na kuibua makosa yake
watakiona cha moto. Kama historia za nchi mbalimbali inavyoonyesha, hili
likitokea, Tanzania itakuwa katika dhahama kubwa.
Maandiko ya
vitabu vitakatifu yanatuelekeza kuwa ukamilifu wa binadamu huja kwa
kusimama katika ukweli, kujikosoa na kukubali kukosolewa na kuepuka
hadaa. Vivyo hivyo, ukamilifu na uhai wa taasisi zinazoundwa na binadamu
kama vile vyama vya siasa na serikali lazima viwe na uthubutu wa
kujikosoa na kukubali kukosolewa kama anavyofanya Magufuli.
Kwa
maelezo hayo hapo juu, ni ni wazi kuwa ukosoaji siyo jukumu pekee la
vyama vya upinzani bali ni jukumu la kila mmoja hasa wale wanaotaka kuwa
viongozi wetu. Hivyo, badala ya kumshangaa Magufuli kwa kubainisha
makosa na mapungufu ya serikali ambayo yeye ni sehemu yake, tujielekeze
katika kuwataka wagombea wengine katika nafasi mbalimbali waepuke hadaa
na badala yake wafanye kampeni zao kwa kueleza ukweli.
Hadaa
katika kampeni zitatupatia viongozi matapeli ambao bila shaka uongozi
wao utakuwa wa hadaa kwa wananchi. Kinyume chake kiongozi mkweli na
aliye na uthubutu wa kujikosoa anaonyesha kuwa ana uwezo wa kutafuta
suluhisho la kweli la matatizo yaliyopo.
Kwa kuitimisha,
Magufuli hajachemka katika kuikosoa serikali aliyomo bali, kwa kufanya
hivyo, anaonyesha ufahamu wake wa hali halisi ilivyo. Zaidi, anaonyesha
kuwa yeye ni mtu aliyetayari kusimamia ukweli jinsi ulivyo na hivyo
ndivyo inapaswa kuwa.
0 comments:
Post a Comment