Sunday 25 October 2015

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KABLA YA KUINGIA KATIKA BIASHARA

Finance 6
Kuingia katika Biashara yoyote ile si jambo dogo sana kama wengi wetu tunavyofikiri, hasa kama unataka biashara yako idumu katika soko na kuwa sehemu ya biashara inayokua kila siku kwa kasi zaidi ya biashara nyingine sokoni.
Hivyo basi katika suala la ukuaji na uendelezi wa biashara unahitaji umakini na uangalifu mkubwa hasa katika uanzilishi wake na hata kuindeleza biashara yenyewe.
Wakati mwingine watu wengi wameona kuanzisha biashara ni suala dogo sana, na ndivyo ilivyo ila si dogo zaidi kama tunavyofikiri. Kuanzisha biashara linaweza kuwa suala dogo kama tunavyofikiri lakini kuiendeleza biashara hiyo likawa ni suala gumu zaidi kwa mtu mwenyewe.
Na kama unahitaji kufikia mahali pazuri pa kuendeleza biashara yako na kufanikiwa, ni vyema uzingatie vitu hivi kama msingi wa kwanza wa biashara yako kabla ya kuanzisha biashara yenyewe husika.
Jambo la Kwanza:
Wazo la Biashara.
Kuwa na wazo la biashara (Business Idea) ndio jambo la kwanza na la pekee kabisa unalotakiwa uwe nalo kabla ya kutafuta mambo mengine yote kama vile mtaji, eneo la biashara nakadhalika.
Watu wengi wanakimbilia kutafuta mitaji ya kuanzisha biashara, pasipo kuwa na wazo timilifu na lenye uhakika la biashara. Wazo ndio msingi wa kwanza wa uanzilishi wa biashara yoyote ile duniani.
Huwezi kukurupuka kutafuta mtaji wa kuanzisha biashara tu pasipo kwanza kuwa na wazo pekee la biashara unayotaka kufanya au kuanzisha. Tafuta wazo zuri la biashara kulingana na fursa zilizopo mahali ulipo ili uweze kufikia lengo na kusudi la kuanza biashara.
Kumbuka: Wazo ndio jambo la kwanza kabisa katika uanzilishi wa biashara yoyote ile hapa duniani.
Jambo la Pili:
Utafiti wa Wazo lako.
Kumbuka siku zote wazo la biashara ndio biashara yenyewe unayotaka kuianzisha na kuifanya katika maisha yako yote ya biashara. Hivyo unapaswa kuwa mwangalifu katika kulitafiti kabla ya kuanza kulifanyia kazi wazo lako husika.
Ni vyema ufanye utafiti wa kutosha kwa ajili ya wazo lako husika la biashara, hasa kwa ajili ya kulifahamu kiundani, kuliboresha na kuliendeleza wazo lako kwa makusudi ya kulifanya kuwa halisi.
Unaweza ukafanya utafiti wako kwa njia ya kuwauliza watu mbali mbali wenye biashara kama unayotaka kuanzisha, kuwauliza wataalamu tofauti wa biashara wanaoelewa biashara hiyo kiundani, kutembelea mitandao mbali mbali nakadhalika.
Jambo la Tatu:
Tafuta Mshauri (Mentor).
Pamoja na kuwa na wazo lako zuri la biashara na tayari umelifanyia utafiti wa kutosha kupitia njia mbali mbali kama nilizotangulia kuzitaja katika jambo la pili hapo juu. Ni vyema sasa utafute mshauri wako mkuu (mentor) wa kudumu, kwa ajili ya kukusaidia kukushauri siku zote katika masuala ya biashara yako.
Suala la kuwa na mshauri wa biashara yako ni la muhimu sana kwa dunia ya leo, hasa kama unataka biashara yako ikue na kufanya vizuri zaidi sokoni. Kama utahitaji niwe sehemu ya kukushauri zaidi kama mshauri wako wa biashara (mentor) utawasiliana nami zaidi kwa mawasiliano yetu yaliyo mwisho wa makala hii.
Jambo la Nne:
Mtaji wa Kuanzia.
Hili ndio suala ambalo kila mtu ambae utamuuliza kwa nini hadi sasa ameshindwa kuingia kwenye biashara, huwa analitumia na kulitaja kama sehemu ya kisingizio cha kutokuanza biashara.
Suala la Mtaji ni suala rahisi na jepesi sana kulifanikisha tofauti na wengi wanavyozani, hasa kama utakuwa umekamilisha mambo mengine yote niliyotangulia kusema na kukueleza hapo juu likiwemo wazo la biashara.
Ni vyema uwe na wazo la biashara kama nilivyotangulia kusema; kisha hatua hii ya mtaji inakua ni sehemu ndogo sana ya wewe kwenda kuingia katika biashara. Kuna vyanzo vingi sana unavyoweza kutumia kwa ajili ya kupata mtaji wa kuanza biashara.
Mojawapo ya vyanzo vya kukupatia mtaji wa kuanzia biashara ni “wewe binafsi.” Wewe ni mtaji tosha na wa kwanza wa kukusaidia kuanza biashara, kwa kupitia uwezo wako, ubunifu, maarifa, vipaji vyako na nguvu ulizonazo.
Njia nyingine za kukusaidia kupata mtaji wa biashara ni zile njia zilizopo nje ya wewe binafsi (nje yako), ambazo njia hizo yawezekana ni kwa njia ya wazazi, mashirika ya ukopeshaji, benki na taasisi za mikopo nchini.
Tambua njia hizi ni nzuri na zinaweza pia kukusaidia kupata mtaji wa kufanyia biashara, lakini kwa wakati mwingine zina mfumo husio mzuri na mrefu hadi kufikia kukusaidia, na tena zinahitaji kwanza juhudi zako zaidi za mwanzo ulizozionesha.
Kwa suala hili zaidi la mtaji nitakuletea makala pekee inayozungumzia zaidi juu ya mtaji wa kuanzia biashara.
Jambo la Tano:
Mtandao/Mahusiano (Network).
Nataka nikuambie kuwa dunia ya leo ili ufanikiwe kibiashara na uchumi na katika eneo lolote lile katika maisha, unahitaji kufahamiana na kujuana na watu tofauti tofauti, ambao wana uelewa tofauti, elimu tofauti na uwezo tofauti.
Watu hawa ni muhimu katika kukusaidia binafsi kufanikisha maono yako yoyote katika maisha. Hivyo basi hata katika uhitaji wako wa kuanzisha biashara unahitaji watu mbali mbali  ili kukusaidia katika kuwa bora zaidi katika biashara au kazi unayoifanya.Unahitaji kutengeneza mahusiano na watu wenye nia dhabiti ya kutaka kufanikiwa kama wewe, kujiendeleza na kukua zaidi katika maendeleo binafsi na ya kibiashara.
Tengeneza Mahusiano na watu wenye kufanya biashara kama yako au unayotaka kuanzisha. Hasa kwa lengo la kupata uzoefu, umakini na uongozi bora wa biashara yako. Watu ni muhimu sana katika kuchangia maendeleo ya maisha yako.
Kumbuka: Angalizo ni kwamba uwe makini sana katika kutambua mtu unayeweza kumshirikisha mambo yako ya kimaendeleo. Kwani si kila mtu unayeweza kumshirikisha mambo yako ya ndani zaidi.
Mambo mengine zaidi ya kuzingatia kabla ya kuingia katika biashara, iwe ni biashara ya duka la mtaani, sokoni au kampuni na kiwanda cha uzalishaji.
Unahitaji kufahamu ni aina gani ya biashara yako unayoanzisha; kama ni biashara binafsi (sole trader), biashara ya mahusiano (partnership), biashara ya ushirika (co-operation); na pia zaidi mamlaka husika zinazoshughulika na usajiri wa biashara yako nakadhalika.
Hadi kufikia hapo sina la ziada tukutane tena kesho katika makala ya “maendeleo ya mtu binafsi.” Nikutakie Mafanikio mema katika maisha yako.
-cicbat

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA