MILIPUKO YAUWA WATU SITA NAIROBI
Milipuko mitatu katika mji mkuu wa Kenya wa Nairobi imesababisha vifo vya watu 6 na karibu darzeni mbili kujeruhiwa jumatatu usiku katika mtaa mkubwa wenye wakazi wengi wa asili ya Kisomali wa Eastleigh.
Mkuu wa polisi wa County ya Nairobi Benson Kibue anasema milipuko hiyo ilitokea takriban saa moja na nusu usiku na kwa karibu wakati mmoja katika migahawa ya Sheraton Café na The New Kwa muzairua Grill.
Kufuatana na mmiliki wa Sheraton Café Bw. Patrick Gakuyu watu walikuwa wanatizama taarifa ya habari ya saa moja kwenye televisheni wakati aliposikia milipuko miwili na umeme kuzimika na kuwa katika kiza. Anasema anadhani ni grunetti mbili zilizorushwa ndani ya mgahawa wake.
Jumapili usiku karibu na mtaa huo mtu anayedhaniwa ni gaidi aliuwawa alipokuwa anatengeneza milipuko yake pamoja na wenzake watatu. Na gruneti moja ilipatikana siku hiyo hiyo ya jumapili katika mji wa pwani wa Lamu ndani ya kanisa moja.
Usalama umeimarishwa katika miji mikuu ya Kenya na hadi hivi sasa haijulikani aliyehusika na mashambulio ya jumatatu.
0 comments:
Post a Comment