Sunday, 29 November 2015

Maelfu wauaga mwili wa Mawazo Mwanza


3
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Mhe. Freeman Mbowe akiaga mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo.
4
Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Mh. Edward Lowassa akitoa heshima zake kwa mwili wa Mawazo.
2
Mawazo enzi za uhai wake.
1
Baadhi ya makamanda wa Chadema wakishiriki zoezi la kumuaga Mawazo leo.(P.T)
MAELFU ya wananchi wa mkoa wa Mwanza wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Mhe. Freeman Mbowe wameuaga mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, huku baadhi ya viongozi wa chama hicho, wakiwemo mawaziri wakuu wastaafu wakilitaka Jeshi la Polisi mkoani Geita kuhakikisha watu waliohusika na mauaji ya kiongozi huyo wanakamatwa na kufikishwa mahakamani mara moja.
Tukio la kuuaga mwili wa marehemu Alphonce Mawazo katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza limetanguliwa na ibada iliyoongozwa na Mchungaji Bernard Swai wa Kanisa la Winners.
Waziri Mkuu Mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu, Fredrick Sumaye pamoja na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Mh. Edward Lowassa wakatoa angalizo kwa Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha linatenda haki katika kushughulikia kifo cha marehemu Alphonce Mawazo.
Mtoto wa marehemu Alphonce Mawazo, Precious Mawazo mwenye umri wa miaka tisa naye ametokea mbele ya halaiki kuelezea majonzi ya kufiwa na baba yake mzazi.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe naye akatoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Alphonce Mawazo, aliyeuawa kikatili kwa kukatwa na mapanga na watu wasiojulikana Novemba 14 mwaka huu katika Kijiji cha Katoro wilayani Geita.
Mwili wa marehemu Alphonce Mawazo tayari umewasili mjini Geita ambako utalala usiku huu ili kutoa nafasi kwa wananchi wa mkoa huo kutoa heshima zao za mwisho kesho Jumapili asubuhi ya Novemba 29, kabla ya kupelekwa nyumbani kwao katika Kijiji cha Chikobe kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika siku ya Jumatatu Novemba 30.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA