UMOJA WA MATAIFA WATAKIWA KUCHUKUA HATUA KUWALINDA WAANDISHI HABARI
Picha ikionyesha ukatili dhidi ya waandishi wa habari
Jumla ya
waandishi wa habari 110, waliuawa duniani kote katika kipindi cha mwaka
2015, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la maripota wasio na
mipaka (RSF) .
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo ya RSF waandishi wa habari 67 waliuawa wakati
wakitekeleza wajibu wao wa kazi katika kipindi cha mwaka huu, na wengine
43 waliuawa katika mazingira ambayo hayajaeleweka. Waandishi wengine wa
habari 27 wasio na taaluma kamili ya uandishi wa habari na wafanyakazi
wengine 7 kutoka katika vyombo vya habari nao pia waliuawa.
Idadi
hiyo kubwa ya vifo vya waandishi wa habari imeelezwa kuchangiwa zaidi na
ukatili unaofanywa dhidi ya waandishi hao wa habari wakati wanapokuwa
wakitekeleza wajibu wao wa kazi. Hali hii inaashiria kushindwa kuchukua
hatua za kuwalinda waandishi wa habari imesema ripoti hiyo na kuutaka
Umoja wa Mataifa kuchukua hatua. Ripoti hiyo inazidi kutoa mwanga juu ya
kuongezeka kwa matukio ya mauaji dhidi ya waandishi wa habari
yanayofanywa na makundi yasiyokuwa na mahusiano na serikali kama vile
makundi ya itikadi kali mfano kundi la Dola la Kiisilamu.
"Kuna
umuhimu sasa wa kuandaliwa utaratibu wa kuwa na sheria ya kimataifa
itakayowalinda waandishi wa habari" alisema Christophe Deloire ambaye ni
katibu mkuu wa shirika la maripota wasio na mipaka. Idadi ya waandishi
wa habari 110 waliouawa mwaka huu inaashiria kuwa kuna haja ya kuchukua
hatua za haraka za kukabiliana na vitendo hivyo. Mwakilishi maalumu kwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atakaye shughulikia kulindwa kwa
waandishi wa habari wanapokuwa wanatekeleza wajibu wao anapaswa ateuliwe
bila kuchelewa," ameongeza kusema Deloire.
Kwa
mujibu wa shirika hilo la maripota wasio na mipaka lenye makao yake
jijini Paris Ufaransa idadi ya vifo 67 inafanya idadi ya waandishi wa
habari 787 waliouawa katika mauaji ya kupangwa au wakati wakitekeleza
wajibu wao tangu mwaka 2005. Kwa mwaka 2014, kulikuwa na mauaji ya aina
hiyo 66 dhidi ya waandishi wa habari.
Mataifa yenye migogoro ni kitisho kwa waandishi wa habari.
Mataifa
yanayokabiliwa na migogoro kama vile Iraq na Syria yameonekanakuwa ni
mataifa yaliyokuwa ya hatari zaidi kwa waandishi wa habari kwa mwaka
huu. Ufaransa imechukua nafasi ya tatu katika orodha hiyo kufuatia tukio
la kuuawa waandishi wa habari wanane wa jarida la tashtit la Charlie
Hebdo nchini humo mwezi January mwaka huu.
Tukio la
mauaji ya waandishi hao wa habari lilikuwa ni tukio ambalo halijawahi
kutokea katika taifa hilo katika kipindi cha nyuma na waandishi wa
habari wa jarida hilo tangu hapo wamekuwa wakiishi chini ya uangalizi na
baadhi yao wamekuwa wakibadilisha maeneo yao ya makazi.
Nchini
Syria mji wa kasikazini wa Allepo nao pia umetajwa kuwa miongoni mwa
miji ambayo imekuwa kitisho kwa maisha ya waandishi wa habari.
Hali hii
inaashiria kuwa waandishi wa habari wako katika hatari ya kupoteza
maisha wanapokuwa wanatekeleza wajibu wao wa kazi kutokana na matukio ya
kukamatwa na kufanywa mateka na makundi ya itikadi kali kama vile kundi
la dola la kiisilamu .
Miongoni
mwa waliouawa nchini Syria ni mwandishi wahabari wa kujitegemea kutoka
nchini Japan, Kenji Goto ambaye aliuawa na kundi la dola la Kiislamu.
Ripoti ya
shirika hilo la maripota wasio na mipaka imeitaja pia India ambako
waandishi wa habari tisa waliuawa tangu mwanzoni mwaka 2015, baadhi yao
kwa kufichua taarifa za mauaji yaliyopangwa na kuhusihwa kwa mauaji hayo
na wanasiasa.DW
0 comments:
Post a Comment