Serikali ya mpito Sudan Kusini kutoanza kama ilivyopangwa
Serikali ya mpito ya Sudan Kusini iliyotarajiwa kuanza rasmi shughuli zake hii leo imetangaza kuakhirisha mpango huo.
Msemaji
wa serikali Atenya Wek Ateny, amethibitisha hayo na ameweka wazi kwamba
takriban thuluthi mbili ya masuala ya kiserikali yataendeshwa kama
ilivyokuwa huko nyuma. Serikali hiyo ya mpito ya Umoja wa Kitaifa
ilitarajiwa kuundwa leo (22.01.2016) ili kumaliza mgogoro wa miaka
miwili uliosababisha zaidi ya watu 15,000 kuuwawa kwa mujibu wa Umoja wa
Mataifa. Serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa ikitarajiwa
kuundwa na kuanza kazi leo ikihusisha mawaziri 30.
Kuundwa
kwa serikali hiyo ni mchakato uliokwenda sambamba na makubaliano ya
amani yaliyotiwa saini na viongozi wawili wanaozozana Rais Salva Kiir na
makamu wake wa zamani Riek Machar kufuatia shinikizo la kimataifa mnamo
mwezi Agosti mwaka jana.
Vita vya
wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha watu zaidi ya milioni mbili
kuachawa bila makaazi vilihusisha mapambano kati ya wanajeshi wa
serikali ya Rais Kiir na waasi wanaomuunga mkono mpinzani wake kisiasa
Riek Machar.
Siku ya kihistoria
Kimsingi
leo ilikuwa siku muhimu iliyotarajiwa kuweka msingi wa kupigwa hatua
katika historia ya taifa hilo la Sudan Kusini ambalo limeshuhudia miaka
miwili ya mapigano kati ya pande hizo mbili hasimu.
Raia
zaidi ya milioni 12 wa nchi hiyo walitarajia kuiona serikali mpya ya
mpito itakayozijumuisha pande zote huku Salva Kiir akiendelea kushikilia
nafasi yake kama rais na Machar kurudishwa katika nafasi yake ya
zamani, yaani makamu wa rais.
Serikali
hiyo ya mawaziri 30 ikitarajiwa kwamba itajumuisha watu sita
walioteuliwa na Rais Kiir huku wengine 10 wakiteuliwa na Machar na
wawili wakiteuliwa kutoka upande wa wale waliokuwa wamezuiliwa jela na
wengine wawili wakiteuliwa na muungano wa vyama vidogo vya kisiasa
nchini Sudan Kusini.
Baadhi ya viongozi wanachama wa IGAD
Ama kwa
upande mwingine, ikitazamiwa kwamba baada ya mchakato mwishoni mwa miezi
30 jeshi la Sudan Kusini ambalo kwa hivi sasa limegawikaa pande mbili,
upande mmoja ukiegemea kambi ya Rais Kiir na upande wa pili wakiwa
watiifu wa Machar, walitarajiwa kuunganishwa hatua ambayo itafuatiwa na
mchakato wa kuitishwa uchaguzi wa rais na Bunge.
Awali
Rais Kiir akizungumza kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, aliwataka
wananchi wa taifa hilo kumpokea Riek Machar na wenzake 600 kwa mikono
miwili wakati wakiwasili nchini humo.
''Nawatolea
mwito nyote kuwakaribisha kaka zenu na dada zenu, watoto wenu wa kike
kwa wa kiuume pindi wakirejea nchini. Wakaribisheni kwa mikono mwili,
mridhiane na kusameheeana, msahau yaliyopita na kuanzisha ukurasa mpya,
mjenge hali ya kuaminiana na imani miongoni mwenu na muishi kwa amani na
upendo,'' alisema Rais Kiir.
Rais Kiir azungumzia vipaumbele
Kiongozi
huyo aliendelea kusisitiza, ''Tunapojiandaa kuzindua serikali ya mpito
ya Umoja wa Kitaifa vipaumbele vyetu vya mwanzo vitakuwa ni kutafuta
utekelezaji wa kudumu wa kusitisha mapigano pamoja na kujenga amani na
kurekebisha shule zilizoharibiwa kwa vita pamoja na mahospitali.
Kuhakikisha upatikanaji wa huduma za maji safi ya kunywa na kurudisha
katika hali ya kawaida maeneo yaliyoathiriwa na vita.''
Ikumbukwe
kwamba yote hayo yanafuatia makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na
Jumuiya ya ushirikiano katika kanda ya Afrika Mashariki-IGAD na ambayo
yaliridhiwa na kutiwa saini na Rais Kiir na makamu wake wa zamani Riek
Machar, Agosti mwaka jana hatua iliyofungua njia ya kupatikana mwafaka
wa kuundwa serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa. Utekelezwaji wa
makubaliano huo unafuatiliwa na aliyekuwa Rais wa Botswana, Festus
Mogae.
Hayo
yanajiri wakati ambapo ripoti ya Umoja wa Mataifa imeleeza kuwa majeshi
ya serikali ya Sudan Kusini yaliwashikilia wanawake kama watumwa wa
ngono, huku yakivamia raia nje ya kambi za Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu
wa ripoti hiyo, mamia ya watu, wakiwemo wanawake wajawazito na wasichana
wadogo walibakwa kwenye jimbo la Unity na wanajeshi wa ama pande zote
mbili. Hata hivyo, serikali ya Sudan Kusini imekanusha taarifa hizo za
ubakaji na uhalifu mwingine.
Chanzo:DW
0 comments:
Post a Comment