SYMPHOROSE MHANZA-MWANAMKE FUNDI NA MWENDESHA MITAMBO PEKEE KIWANDA CHA KONYAGI
Bi Symphrose akiwa kazini katika kiwanda cha Konyagi jijini Dar es Salaam |
Ukifika katika kiwada cha
Konyangi kilichopo eneo la Chang’ombe jijini Dar es Salaam na kumkuta
Bi.Symphorose Mhanza akiwa mitamboni huwezi kuamini kama ni mwanamke kutokana na
anavyomudu kazi yake ya ufundi na uendeshaji mitambo.
Symphorose anasema kuwa japo
kazi hii inaonekana kuwa ngumu kwa kuwa kuna wakati inabidi kutumia nguvu
nyingi kama ilivyo desturi ya kazi za ufundi lakini ameizoea na anaipenda.
“Naipenda sana kazi yangu na
nimeizoea japo inaonekana kuwa ni ngumu
na inafanywa zaidi na wanaume lakini mimi naona kawaida japo sijaona mwanamke
mwingine anayethubutu kuifanya kiwandani hapa”.Anasema.
Bi.Symphorose anasema jambo linalompa faraja kubwa na kuipenda zaidi kazi yake ni kutokana na jinsi anavyoaminiwa na mabosi
wake kiasi kwamba japo ni mwanamke peke yake katika kiwanda hicho anayefanya
kazi hii lakini anathaminiwa na kuaminiwa kama wanavyoaminiwa wafanyakazi
wenzake wanaume.
Akieleza historia yake ya
kazi alisema mwanzoni mwa miaka ya tisini ndipo alipojiunga na kiwada cha
Konyagi ambacho hivi sasa kiko chini ya kampuni ya TBL “Wakati huo ulipokuwa
unaajiriwa ulikuwa kwanza unapata mafunzo ya ndani yaliyokuwa yanatolewa kweye
fani mbalimbali ambapo mimi nilijifunza ufundi na uendeshaji mashine (Machine
Operator) kwa kipindi cha mwaka mmoja na nilipofuzu ndipo nikaanza kuifanya
kazi hii”.Anasema.
Bi.Symphorose aliendelea
kueleza kuwa baada ya kiwanda hicho kubinafsishwa kuna mifumo mingi mipya
imeanzishwa ikiwemo mafunzo ya mara kwa mara ambayo anadai yamesaidia kumpatia
ujuzi mkubwa katika fani ya ufundi na uendeshaji mashine na kumjengea uwezo wa
kujiamini zaidi.
Alisema anajivunia kufanya
kazi katika kampuni hii hasa kwa jinsi alivyoweza kupata ujuzi mkubwa ambao
unamuwezesha kumudu maisha popote atakapokwenda hata baada ya kustaafu kazi na
kuamua kuendesha shughuli zake.
Kuhusiana na changamoto
zilizopo katika kazi yake alisema ni za kawaida kama zilivyo katika kazi
nyingine “Changamoto kubwa ni mabadiliko ya kiteknolojia ambayo ili kwenda nayo sambamba inabidi uwe na ufuatiliaji wa
mambo mbalimbali katika fani ya ufundi bila hivyo unaweza kuachwa nyuma kwa
kuwa kila kukicha inabuniwa mitambo ya kisasa zaidi”.Alisema.
Kuhusiana na mafanikio
ambayo ameyapata kutokana na kazi yake Bi.Symphorose
ambaye ni mama wa familia mwenye watoto anasema yapo mafanikio kwa kuwa anaweza
kuchangia katika pato la familia katika kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo
kusomesha watoto wake.
Mafanikio mengine ni
kufundishwa na mwajiri wake mambo
mbalimbali ambayo yanasaidia
katika maisha ya kawaida “Hapa tunajifunza usafi wa mazingira,nidhamu ya
kutunza fedha,kupanga bajeti,kuzingatia muda na mambo mengineyo mengi ambayo
yanaweza kukusaidia sehemu yoyote katika maisha na ndio maana najivunia kufanya
kazi kampuni kubwa kama TBL”.Alisema.
Bi Symphorose Mhanza akitoa mafunzo ya uzalishaji kwa wafanyakazi wenzake katika kiwanda cha konyagi kilichopo jijini Dar es Salaam
Alimalizia kutoa ushauri kwa
watanzania wote kuwa tuachane na uzembe na tufanye kazi kwa bidii popote pale
tutakapokuwa tutafanikiwa na pia
alishauri wanawake wenzake kuchangamkia fursa za ajira zitazojitokeza ili
kuweza kupata kipato na kuwakwamua katika janga la umaskini.
0 comments:
Post a Comment