BESIGYE ASHIKILIWA NA POLISI TENA
Kiongozi
mkuu wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, amekamatwa kwa mara
nyengine baada ya kuchukuliwa nyumbani kwake alikokuwa kwenye kizuizi
cha nyumbani, hii ikiwa ni mara ya nne ndani ya wiki moja.
Besigye,
ambaye amekataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika siku ya
Alhamis (Februari 18) na ambayo yalimpa ushindi Rais Yoweri Museveni,
alichukuliwa na polisi siku ya Jumatatu (Februari 22), siku ambayo
alikuwa ametoa wito kwa wafuasi wake kuandamana nchi nzima.
Polisi
inasema maandamano hayo ni haramu, wakiongeza kwamba kwa kuwa muhula
mpya wa masomo unaanza, "basi maandamano hayo yangeliingilia haki za
wazazi na watoto wao wanaokwenda skuli."
Besigye
aliwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani siku ya Ijumaa baada ya polisi
kuyavamia makao makuu ya chama chake, Forum for Democratic Change (FDC),
wakiwatuhumu maafisa wa chama hicho "kutaka kutoa matokeo yao ya kura
kinyume cha sheria."
Polisi
walimchukuwa Besigye kutoka nyumbani kwake Kasangati, kaskazini mwa mji
mkuu Kampala na kumpeleka kwenye kituo cha polisi cha Nagalama, kwa
mujibu wa msemaji wa polisi, Patrick Onyango.
Besigye
hakusema kitu wakati akitupwa kwenye gari lenye vioo vya giza na
kuondolewa nyumbani kwake na Onyango hakutoa ufafanuzi zaidi.
'Nyumba imekuwa kambi ya kijeshi'.
Mke wa
Besigye, Winnie Byanyima, ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa shirika
la misaada la Oxfam International, alituma picha kwenye mtandao wa
Twitter ikiwaonesha polisi wa kuzuia fujo nje ya nyumba yao, akisema:
"Nyumba imekuwa kama kambi ya kijeshi. Tunataka amani."
Matokeo
yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi siku ya Jumamosi yalimpa Museveni
asilimia 70 ya kura dhidi ya asilimia 30 za Besigye, ambaye hadi matokeo
hayo yanatangazwa alishakamatwa mara tatu, kabla, wakati na baada ya
uchaguzi.
Hadi
sasa, Besigye ameshindwa mara ya nne kwenye uchaguzi wa urais na kila
mara amekuwa akilalamikia wizi wa kura na kila mara maandamano ya
wafuasi wake yamekuwa yakikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa vyombo vya
dola.
Museveni,
ambaye ameitawala Uganda tangu mwaka 1986, aliusifia ushindi wake na
akayatupilia mbali malalamiko ya Besigye na zile za waangalizi ambao
wameuita uchaguzi huo kuwa "haukuwa wa haki wala huru".
"Wapinzani
si viongozi. Ni watu domokaya, waongo, wanasemasema tu," alisema
kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 71 siku ya Jumapili.
"Na hao
Wazungu hawako makini," alisema akikusudia waangalizi wa Umoja wa Ulaya
waliosema kuwa Tume ya Uchaguzi ya Uganda haikuwa na uwazi na kwamba
polisi walitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya upinzani.
Chanzo:DW
0 comments:
Post a Comment