Monday, 22 February 2016

ULIMWENGU: NILICHEZA KIBISHI BISHI TU SUPER CUP, MGUU ULIKUWA UNAUMA ILE MBAYA

Na Mwandishi Wetu, LUBUMBASHI
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesema kwamba alicheza mechi ya kuwania Super Cup ya CAF Jumamosi akiwa ana maumivu makali ya mguu.
“Sikuwa katika nafasi ya kucheza kabisa siku ile, nilijilazimisha tu. Lakini namshukuru Mungu nimecheza Super Cup,”amesema Uli maarufu kwa jina la Rambo akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo mjini hapa.
Ulimwengu amesema kwamba aliumia mguu katika mechi ya ugenini wiki iliyopita dhidi ya St Eloi Lupopo wakitoa sare ya 0-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya DRC.

Ulimwengu amesema kwamba alicheza mechi ya kuwania Super Cup ya CAF Jumamosi akiwa ana maumivu makali ya mguu

Mabao mawili ya kipindi cha kwanza ya Daniel Nii Adjei yalitosha kuipa TP Mazembe ubingwa wa Super ya Afrika baada ya kuifunga 2-1 Etoile du Sahel ya Tunisia Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, DRC.
Mchezaji huyo wa Ghana alifunga bao la kwanza dakika ya 19 kabla ya kufunga la pili dakika ya 45, wakati Mohamed Msakni aliwafungia Watunisia dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza.
Hilo linakuwa taji la tatu kwa Mazembe la Super Cup, baada ya awali kutwaa Kombe hilo mwaka 2009 na 2010, sambamba na kuendeleza wimbi lake la ushindi tangu ilipotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Na siku hiyo, Ulimwengu aliingia akitokea benchi dakika ya 78 kuchukua nafasi ya Adama Traore – nas sasa Rambo anakuwa mwanasoka wa Tanzania aliyetwaa mataji mengi makubwa ya Afrika, baada ya mwishoni mwa mwaka kuiwezesha Mazembe pia kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika. 
Na ndiye mchezaji pekee wa Tanzania kutwaa Super Cup ya CAF, huku Mbwana Samatta aliyekuwa naye Mazembe kabla ya kuhamia KRC Genk ya Ubelgiji, akiwa mchezaji mwingine wa Tanzania aliyetwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika. 
Ulimwengu na Samatta pia ndiyo Watanzania pekee waliocheza Klabu Bingwa ya Dunia. Ulimwengu amesema anatarajiwa kuwa fiti mapema mwezi ujao baada ya kuanza matibabu leo. “Nitarejea nikiwa fiti kabisa mwezi ujao, nimeanza matibabu leo,”amesema.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA