MPANGO WA KUSAIDIA KAYA MASIKINI WANUFAISHA KAYA MILIONI 1.1 NCHINI
Mpango wa Kijamii wa Uzalishaji Salama ili kusaidia kaya masikini kupambana na umasikini (PSSN) umefanikiwa kuwa na matokeo mazuri kwa kusaidia kaya Milioni 1.1 nchini na kusaidia juhudi za serikali kupambana na umasikini.
Hayo yamefahamika wakati washirika wa maendeleo ambao ni Umoja wa Mataifa, Benki Kuu ya Dunia, Serikali ya Uingereza kupitia kitengo cha Maendeleo ya Kimataifa, Irish Aid, USAID, Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Sweden (SIDA) walipotembelea miradi ya maendeleo katika wilaya za Unguja, Chamwino, Babati, Sumbawanga (Manispaa na Wilaya), Singida na Hanang kwa kipindi cha siku tatu kuanzia Januari, 19 hadi 22.
Katika Mpango huo ambao utekelezwaji wake unasimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) unafanyika Tanzania Bara na Tanzania visiwani ukiwa na lengo la kuzisaidia kaya masikini pesa za matumizi ili kukidhi mahitaji ya kupata chakula pamoja na kuwawezesha kusaidia watoto wao kupata elimu jambo ambalo linaonekana kuzaa matunda kwa maeneo mengi ikiwepo Tanzania visiwani.
Serikali ya Tanzania imekuwa ikisaidia na washirika wa maendeleo ili kupunguza umaskini uliokithiri kwa wananchi wake na mwaka 2013 iliweka mpango wa kusaidia kaya masikini 275,000 kwa kipindi cha miaka mitano na tangu ianzishe mpango huo ilifanikiwa kusaidia kaya 275,000 kwa mwaka 2013 pekee katika wilaya nane nchini.
Na mpaka kufikia sasa mpango huo umeshatoa malipo mara 12 na jumla ya kaya masikini milioni 1.1 zimeshafaidika na mpango huo ikiwa ni kwa wilaya 161 na vijiji 9789 nchini.
Malengo ya serikali ya Tanzania na mashirika ya kimataifa ni kuhakikisha kufikia mwaka 2030 kunakuwa hakuna masikini hivyo ni wajibu wa kila nchi kuhakikisha inawasaidia wananchi wake ili wajijengee uwezo wa kujitegemea na kuondoka katika janga la umasikini.
0 comments:
Post a Comment