Thursday 4 February 2016

SIMBA YAANZA KUUWINDA UBINGWA LIGI KUU

Na Princess Asia, DAR ES SALAAM SIMBA SC imejiweka sawa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuifunga Mgambo JKT mabao 5-1 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 39 baada ya kucheza mechi 17, sasa ikiwa inazidiwa pointi moja tu na mabingwa watetezi, Yanga SC walio kileleni, wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 39 pia.

  Mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya tano akimalizia krosi ya mshambuliaji Ibrahim Hajib. Kiiza akakosa penalti dakika ya 14 iliyookolewa na kipa Mudathir Khamis, kufuatia Henry Chacha kuunawa mpira kwenye boksi. Lakini Mwinyi Kazimoto akafunga bao la pili dakika ya 28 kwa shuti kali kutoka nje ya boksi baada ya kugongeana vizuri na Hajib. Hajib akaenda kufunga mwenyewe bao la tatu dakika ya 42 baada ya kuwachambua mabeki watatu wa Mgambo na kipa wao Mudathir Khamis, kufuatia pasi ya Kazimoto.  

Daniel Lyanga aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Hajib kipindi cha pili, aliifungia Simba SC bao la nne kwa shuti kali kutoka nje ya boksi baada ya pasi ya kiungo Said Ndemla. Kiiza akahitimisha karamu ya mabao ya Simba SC kwa kufunga bao la tano dakika ya 82 akimalizia krosi ya Hassan Kessy, ambaye amecheza kwa kiwango cha juu leo.

Fuluzulu Maganga ‘akachafua gazeti’ kwa kuifungia Mgambo bao la kufutia machozi dakika ya 88 baada ya mabeki wa Simba SC kumuacha wakidhani ameotea. Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Kessy Ramadhani, Abdi Banda, Juuko Murshid, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamisi Kiiza, Ibrahim Hajib/Danny Lyanga dk72 na Hija Ugando/Said Ndemla dk62.  Mgambo JKT; Mudathir Khamis, Bakari Mtama/Bolly Shaibu dk44, Salim Mlima, Salim Kipaga, Ramadhani Malima/Mussa Ngunda dk44, Henry Chacha, Sunday Magoja, Mohammed Samatta, Fully Maganga, Ally Nassor na Aziz Gilla. 
MATOKEO NA RATIBA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA
  Febaruri 3, 2016 
Prisons 2-2 Yanga SC
Simba SC 5-1 Mgambo JKT
Kagera Sugar 2-1 Majimaji
African Sports 1-0 Mwadui FC
Mtibwa Sugar 2-2 Toto Africans
 Feburari 4, 2016
JKT Ruvu Vs Mbeya City
Coastal Union Vs Ndanda FC

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA