Friday 19 August 2016

MAJALIWA AZUNGUMZA NA WATUMISHI NA VIONGOZI WA MANISPAA YA ILALA, AWATAKA WAFANYENI UKAGUZI KUBAINI WANAFUNZI HEWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Manispaa ya Ilala jijini Dar es salam kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam Agosti 18, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya Viongozi na watumishi wa Manispaa ya Ilala wakisikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza nao kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam Agosti 18, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoka kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Julius Kambarage Nyerere baada ya kuzngumza na Viongozi na Watumishi wa Manispaa ya Ilala Agosti 18, 2016. Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda (kulia kwake), Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam, Teresia Mmbando (kushoto) , Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Dar es salaam, Ramadhani Madabida (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Sophia Mjema . (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu nchini wafanye ukaguzi katika shule ili kubaini wanafunzi hewa kwenye mpango wa elimu bure.

“Kila mwezi Serikali inapeleka shule zaidi ya shilingi bilioni 18 kugharamia elimu bure na sasa tumeanza kuona udanganyifu katika sekta ya elimu kwa kuwa na wanafunzi hewa. Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu nendeni mkafanye ukaguzi ili mpate takwimu sahihi,“ amesisitiza.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Agosti 18, 2016) alipokutana na watumishi na viongozi wa Manispaa ya Ilala katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu mkiona takwimu ziwachanganya, ni lazima mtoke maofisini na kwenda katika shule zilizo kwenye mpango wa elimu bure mkafanye uhakiki wa idadi ya wanafunzi,” ameonya.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema maamuzi yanayotolewa kwenye vikao vya madiwani lazima yawe na tija na ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatumika kuboresha shunghuli za maendeleo badala ya kujilipa posho.

“Lazima mjipange vizuri na kupunguza changamoto zinazoikabili wilaya yenu. Malipo yote ni lazima yawe yale yaliyoainishwa katika waraka na si vinginevyo.Mtu wa Ilala unadai nauli ya sh. 200,000; hivi unakuwa unatoka wapi hata mimi wa Lindi silipwi nauli hiyo,” amehoji.

Waziri Mkuu amesema ni lazima halmashauri zote nchini zizingatie sheria za Mamlaka ya Serikali za Mitaa na watendaji wake wajiulize kama mambo wanayoyafanya yana tija na wanawatendea haki watu wanaowatumikia.

Amesema Serikali inataka kuwa na watumishi wanaotambua nafasi zao na watakaofanya kazi kwa uadilifu, uaminifu pamoja na uwajibikaji mkubwa hivyo kila mtu ahakikishe anafanya kazi vizuri na yenye matokeo chanya.

“Kuna watu wanaona ukuu wa idara ndiyo kila kitu, hata yule anayekimbiza mafaili hathaminiwi, hili si jambo jema! Ninyi wote ni kitu kimoja, ni watumishi wa Serikali, hivyo kila mmoja amthamini mwenzake,” amesema.

Waziri Mkuu amesema: “Mkurugenzi yeyote asikubali kuwa na wakuu wa Idara wasiokuwa na ushirikiano na watumishi wengine kwa sababu hataweza kupata mafanikio ya kiutendaji ndani ya eneo lake,”.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, AGOSTI 18, 2016.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA