Showing posts with label MAJALIWA. Show all posts
Showing posts with label MAJALIWA. Show all posts

Sunday, 23 January 2022

WAZIRI MKUU MHE. KASSIM MAJALIWA AKABIDHI PIKIPIKI KWA VIJANA HANANG

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkpatia ufunguo wa pikipiki ya miguu mitatu (guta), Emmanuel John wakati alipokabidhi pikipiki na guta kwa kikundi cha vijana kilichonufaika na mkopo wa asilimia 10 kutoka halmashauri ya wilaya ya Hanang' akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Manyara.  Tukio hilo lilifanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Katesh  wilayani humo.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi ya Sh. 500,000/= mwanariadha wa zamani  Gidamis Shahanga ikiwa ni ishara ya kutambua heshima kubwa aliyolipatia  taifa letu kwa  kuwa mshindi pekee wa medali mbili za dhahabu katika  mashindano ya Jumuiya ya Madola(Commonwealth Games), mwaka 1978 na 1982  mita 10,000. Mheshimiwa Majaliwa alitoa zawadi hiyo baada ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Mogitu – Katesh wilayani Hanang na kuwasalimia wananchi katika viwanja vya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Katesh, Januari 23, 2022.  Kushoto ni Naibu Waziri wa Michezo na Utamaduni, Sanaa na Micheo, Pauline Gekul.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Tuesday, 22 August 2017

WAZIRI MKUU AKUTANA NA WANAFUNZI WA TANZANIA WANAOSOMA UDAKTARI CUBA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote wahakikishe wanaboresha mshikamano wao pamoja na kuimarisha uzalendo kwa Taifa lao.

Ametoa kauli hiyo Jumapili, Agosti 20, 2017 wakati akizungumza na wanafunzi wa Kitanzania wanaosomea udaktari nchini Cuba.

Waziri Mkuu yuko nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Alisema uzalendo kwa Taifa ni jambo muhimu.

“Uzalendo ni muhimu sana kwa sababu tumekosa fursa nyingi za kimaendeleo kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa wazalendo kwa Taifa lao.”

Kutokana na hali hiyo Serikali inawasisitiza Wananchi kuwa wazalendo na washirikiane kuhakikisha fursa za kimaendeleo zilizoko nchini zinaendelezwa.

Alisema Serikali inatekeleza miradi mingi kwa lengo la kukuza uchumi kutoka wa chini kwenda wa kati, ni vema wananchi wakashirikiana nayo ili kufanikisha adhma hiyo.

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi hao kuzingatia sheria za nchini waliyoko pamoja na kukumbuka kurudi nyumbani mara wamalizapo masomo yao.

Alisema Serikali inatambua uwepo wao wa kimasomo nchini Cuba na kwamba inatarajia kupata mchango mkubwa kutoka kwao punde wamalizapo masomo yao.

“Nawaomba msome kwa bidii na mfaulu mitihani yenu. Elimu yenu iwasaidie katika ajira na muweze kurejesha mikopo mliyopewa na Serikali ili iwanufaishe wengine.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka Mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii.

Alisema Tanzania imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, hivyo ni vema Mabalozi wakavitangaza jambo ambalo litasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Miongoni mwa vivutio vya utalii vilivyoko nchini ni pamoja na mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar, mbuga mbalimbali zenye wanyama wa aina tofauti tofauti.

Awali Mwenyekiti wa wanafunzi hao, Bw. Goodchance Tarimo alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watarejea nyumbani mara baada ya kumaliza masomo yao nchini humo.

Alisema wao wanaimani kubwa na Serikali na wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wa Taifa kwa lengo la kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.

“Tunapongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika  kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na ujenzi wa miundombinu ya kisasa.”

Friday, 18 August 2017

TUTAENDELEZA MAJALIWA::MAHUSIANO YA KIDIPLOMASIA YALIYOJENGWA NA AWAMU ZILIZOTANGULIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inayatambua na kuyathamini mahusiano mazuri ya kidiplomasia yaliyojengwa na awamu zilizotangulia baina ya Tanzania na mataifa mbalimbali ikiwemo Jamuhuri ya Cuba na kwamba itayaendelea. 

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Agosti 17, 2017), alipozungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Bi Anna Teressa mara baada ya kuwasili nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. 

“Tanzania na Cuba zina historia ya kutosha. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere.” 

Amesema katika ziara yake hiyo anatarajia kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali ya Cuba kwa lengo la kukuza ushirikiano katika sekta za Afya, Elimu, Utalii na Kilimo. 

Waziri Mkuu amesema Cuba ni mojawapo kati ya nchi zenye ushirikano wa muda mrefu na Tanzania kisiasa, kijamii, kiafya na kiuchumi.”Mfano katika Sekta ya Afya, madaktari wengi kutoka Cuba walikuwa wanakuja Tanzania kutibu wagonja waliokuwa na maradhi makubwa.” 

Pia Waziri Mkuu amesema katika ziara hiyo anatarajia kukutana na Jumuya ya Wafanyabiashara wa Cuba ili kuwaelezea fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania hususan katika Sekta ya Viwanda pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. 

Kwa upande wake Bi. Anna ambaye alimpokea Waziri Mkuu kwa niaba ya Serikali ya Cuba alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea ushirikiano mzuri baina ya nchi hizo mbili, hivyo alimuhakikishia kwamba wataendelea kuudumisha. 

Pia Bi. Anna ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa namna inavyopambana na rushwa, ufisadi, kuhimiza uwajibikaji pamoja na kutetea wanyonge. 

IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
IJUMAA, AGOSTI 18, 2017.

Saturday, 12 August 2017

MAJALIWA ::WANANCHI WALIOPEWA URAIA MUHESHIMU SHERIA ZA NCHI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa CUF Jimbo la Kaliua ,Magdalena Sakaya  Agosti 11.2017,Waziri Mkuu yupo wilayani Kaliua kwa ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo katika Mkoa wa Tabora
                                                                                       Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihotubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Veta Jimbo la Ulyankulu wilayani Kaliua Mkoani Tabora jana August 11.2017, ambapo amewataka wananchi waliopewa uraia kuheshimu sheria za nchi vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.  Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongea na wananchi wa kitongoji cha Mwamnange kilichopo Wilaya ya Kaliua jana Agosti 11 2017 .Wananchi hao walisimamisha msafara wake ili kumuomba serekali iwasaidie kupata Umeme. Waziri Mkuu yupo Mkoani Tabora kukagua shughuli za maendeleo.
                                                                        Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Thursday, 27 July 2017

PROGRAMU ZA ELIMU YA JUU ZIWEZESHE WAHITIMU KUJIAJIRI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha kwamba programu zote zinazotolewa na taasisi za elimu ya juu zinawawezesha wahitimu kujiajiri na kuwa na sifa za ushindani katika soko la ajira kimataifa. 


Amesema wakati umefika sasa kwa wasomi katika vyuo vyetu vikuu tujiridhisha kuwa mitaala inayotolewa kama inawaandaa wahitimu kupata taaluma na stadi za kuweza kujiajiri na kupambana na changamoto za kimaisha. 



Ametoa agizo hi lo jana(Jumatano, Julai 26, 2017) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 12 ya Elimu ya Juu, jijini Dar es Salaam. 



Amesema taasisi za elimu ya juu nchini ziangalie mitaala yake na kuimarisha mfumo wa ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ili kwenda sambamba na dunia ya kazi inayoendana na agenda ya maendeleo ya Taifa. 



Waziri Mkuu amesema maonesho hayo ni jukwaa la kipekee ambalo litaibua mjadala sahihi kuhusu uhalali wa kozi zinazotolewa na vyuo husika vya elimu ya juu. “Hivyo mnayo nafasi ya kuonesha kwa vitendo uwezo wenu katika utafiti, ubunifu na matumizi ya sayansi na teknolojia zinazotumika katika maendeleo ya viwanda.” 



Amesema ni vema mfumo wa ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ukaimarishwa ili kuhakikisha asilimia 60 ya wanafunzi wanahitimu shahada kwenye sekta ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi. 



Amesema taasisi za elimu ya juu ziweke mikakati ya kuinua na kuboresha taaluma wanayoitoa ili ilete tija kwa maendeleo ya Taifa na Dunia. Pia kuanzisha program za mafunzo zenye kukidhi mahitaji na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuzingatia mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa. 



Hata hivyo, Waziri Mkuu amezitaka taasisi hizo kuendelea kuimarisha mfumo wa udahili na kujipanga kutumia fursa za elimu na mafunzo ndani na nje ya nchi kwa makundi yote ya jamii kwa usawa katika ngazi zote hususan ufundi, hisabati, sayansi na teknolojia. 



Pia Waziri Mkuu amesema ni wakati muafaka kwa taasisi za elimu ya juu nchini kuandaa mikakati ya kuongeza udahili kwa kuzingatia mahitaji ya rasilimali watu na ujuzi unaohitajika katika sketa zinazokua haraka mfano mafuta, gesi na madini. 



IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
ALHAMISI, JULAI 26, 2017

Sunday, 2 July 2017

WAZIRI MKUU ATOA UFAFAZI SAKATA LA KUZUIA MAHINDI KUUZWA NJE YA NCHI

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amejibu hoja zinazosambazwa na wanasiasa wa kambi ya upinzani juu ya zuio la chakula nje ya nchi, akisema Serikali haizuii fursa ya wakulima kuuza mazao nje.

Bali, amesisitiza serikali inataka mazao hayo yatosheleze nchini na kama ni lazima, basi kwanza yasindikwe, yabanguliwe, yachakatwe kwa kuyakoboa ili kuyaongezea thamani. Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akijibu hoja ya wapinzani, walioitisha mkutano wa waandishi wa habari juzi na kuilaumu serikali.

Alhamisi wiki iliyopita, wakati Waziri Mkuu akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Viti Maalumu, Ritha Kabati aliyetaka kuruhusiwa kuuzwa mahindi nje ya nchi, alikataza kuuza mahindi nje ya nchi.

Alisema ni marufuku kuuza mahindi nje ya nchi; na kama ni muhimu lazima kibali kitoke kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kuuza nje ya nchi; na uuzwe unga uliosagwa na kamwe yasiuzwe mahindi.

Waziri Mkuu alitetea kauli hiyo ya serikali jana wakati akikagua banda la Ushirika wa Wakulima Wadogo wa Kilimo cha Umwagijiaji Dakawa (UWAWAKUDA) kabla ya kufunga Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD), yaliyofanyika katika Ukumbi wa CCM wa Jakaya Kikwete mjini hapa.

Alimpongeza na kumsifu mkulima Nassib Katoto kwa niaba ya wakulima wenzake wa Mpunga Dakawa mkoani Morogoro, kutokana na kulima kilimo cha umwagiliaji, lakini hasa kuvuna mpunga, kuukoboa na kuusindika ili kupata mchele na kuuweka katika mifuko na kuuza baada ya kuongeza thamani, badala ya mpunga.

Majaliwa alisema nia ya serikali si kuzuia fursa ya wakulima kuuza mahindi nje ya nchi, bali inataka kuhakikisha kila eneo nchini linakuwa na chakula, kwani baadhi ya maeneo nchini hayana chakula kutokana na kukosa mvua na hivyo kukumbwa na ukame.

Lakini, kama ni lazima kuuza chakula nje ya nchi, basi ni vema kibali kikatolewa na Waziri mwenye dhamana kwa kuuza unga badala ya mahindi. 

Alisema mazao yakisindikwa, yakichakatwa, yakabanguliwa na yakikobolewa kama vile mahindi, viwanda vya kukoboa na kusaga vitapata kipato, watu watapata ajira na mabaki yake yaani pumba yatatumika kulisha mifugo, kuliko kama yangeuzwa mahindi, kwani viwanda visingepata kazi, vijana wasingepata ajira na mifugo isingepata chakula.

Monday, 19 June 2017

WAZIRI MKUU::TAIFA LA WATU WAADILIFU HUANZIA KWENYE FAMILIA

Image result for majaliwa
Picha /Maktaba
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wazazi wana jukumu la kulea watoto kwenye misingi ya kumcha Mungu ili Taifa liweze kuwa na watu waadilifu na wachapakazi. 

“Taifa la watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia. Kama kaya zetu haziishi kwa uadilifu, ni vigumu sana kuwa na Taifa lenye wananchi waadilifu. Ni muhimu basi familia zetu zihakikishe kuwa tunakuwa na watoto wenye hofu ya Mungu na wenye kumcha Mungu,” alisema.

Alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Juni 17, 2017) wakati akizungumza na wageni waliohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na nyumba ya Paroko katika Parokia Teule ya Zuzu, nje kidogo ya mji wa Dodoma. 

Harambee hiyo ilitanguliwa na ibada ya misa ya shukrani kwa ajili ya marehemu Mzee Xavery Mizengo Pinda, ambaye ni baba yake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Peter Pinda. Mzee Xavery Pinda alifariki Novemba 27, mwaka jana katika hospitali ya mkoa wa Dodoma na kuzikwa kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele, Katavi.

Waziri Mkuu alisema wazazi wanapaswa kujitathmini juu ya malezi ya watoto wao na kujihoji kama wamepata malezi yanayostahili. “Kupitia funzo tulilolipata leo, tujitathmini kuhusu makuzi ya watoto wetu. Je watoto wetu wanapata malezi stahiki? Je tunawalea katika misingi ya kutoa kwa ajili ya Mungu au tunawafundisha wajilimbikizie mali? Je, tunawahoji watoto wetu kuhusu utajiri wanaoupata ghafla? Au tunawapongeza na kufurahia bila kujua wanapata wapi utajiri huo?,” alihoji.

“Nitumie nafasi hii kuwasihi wazazi wote kwamba tujitahidi kuwekeza katika malezi ya watoto wetu. Ili tuwe kioo cha aina ya Taifa tunalotaka kulijenga, hatuna budi kuwalea watoto wetu katika misingi ya imani, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa nchi yetu,” alisisitiza.

Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mke wake walichangia sh. milioni 10 ambapo jumla ya sh. milioni 160 zilikusanywa. Kati ya hizo, sh. 111,150,000 zilikuwa ni ahadi, sh. 38,447,000 zilikuwa ni fedha taslimu na sh. 10,403,000 zilikuwa ni vifaa vya ujenzi.
Mapema, akiongoza ibada ya shukrani, Makamu wa Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Padre Chesco Msaga alisema kila mtu anapaswa kumshukuru Mungu kwani hakuna mwanadamu anayeweza kudai kuwa yuko jinsi alivyo kwa sababu ya akili zake. 

“Hata sisi tunasahau kumshukuru Mungu hasa pale mambo yetu yanapotunyookea. Tunadhani ni kwa akili zetu ndiyo mambo yetu yananyooka. Tunapaswa tukumbuke kuwa maishayetu yapo mikononi mwa Mungu, na yeye ndiye anajua njia zetu,” alisema akirejea mfano wa wakoma 10 walioponywa na Bwana Yesu na mmoja tu ndiye alirudi kushukuru.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema harambee hiyo inafuatia uamuzi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya wa kuiteua Zuzu iwe parokia. 

“Sasa hivi tulikuwa na kigango. Kuteuliwa kuwa parokia maana yake tutakuwa na padre anakaa hapa Zuzu saa 24 na tutakuwa na ibada kila Jumapili, na katikati ya wiki kadri ratiba zitakavyoruhusu. 

“Kikubwa tunachopaswa kufanya kufuatia uamuzi huo, ni kuhakikisha kuwa mapadre wana nyumba ya kuishi. Sasa hivi, wa kwetu anakaa Dodoma mjini. Kwa hiyo tuna kazi ya kukarabati kanisa, lakini kwanza tukamilishe ujenzi wa nyumba ya mapadri,” alisema wakati akielezea madhumuni ya harambee hiyo. 

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA. 
JUMAPILI, JUNI 18, 2017.

Sunday, 18 June 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AONGOZA MAZISHI YA MARAYAPILI YA MZEE YUSTINO NDUGAI


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu CCM Abdalah Bulembo (Mbunge) akitoa salamu kwa niaba ya Wabunge wa CCM , Katika Tukio la Mazishi ya mara ya Pili ya Marehemu Yustino Ndugai Baba Mzazi wa Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai . Marehemu Yustino alifariki Mwaka 1992 na amezikwa mara ya Pili June 17 , 2017 katika makaburi ya familia ya Ndugai Kijij cha Chimoloto Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma
  Waiziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa Salamu za Serekali kwa Wananchi , Katika Tukio la Mazishi ya Mara ya Pili ya Marehemu Yustino Ndugai Baba Mzazi wa Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai . Marehemu Yustino alifariki Mwaka 1992 na amezikwa mara ya Pili June 17 , 2017 katika makaburi ya familia ya Ndugai Kijij cha Chimoloto Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Wziri Mkuu Kassim Majaliwa . akiweka Shada la Maua katika kaburi alipo Zikwa Kwamara ya Pili Marehemu Yustino Ndugai Baba Mzazi wa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Job Ndugai. Shughuli hiyo imefanyika June 17 , 2017 katika makaburi ya familia ya Ndugai Kijij cha Chimoloto Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

Tuesday, 6 June 2017

WAZIRI MKUU ATOA ONYO ZITO KWA WANAUME WANAOWAPA MIMBA WANAFUNZI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mtu yeyote atakayebainika amemkatisha mwanafunzi wa kike masomo kwa kumpa mimba au kumfanyia vitendo vya ukatili vitakavyopelekea kukatisha masomo yake ni lazima afungwe miaka 30 jela.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Lugalo jeshini Jijini Dar es Salaam wakati akizindua na kukabidhi vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu vyenye jumla ya thamani ya Shilingi Bilioni 16.9 kwa ajili ya shule 1696 kwa nchi nzima kwa lengo la kuhakikisha uboreshaji wa masomo ya sayansi.

Vilevile Majaliwa ameiagiza TAMISEMI kuhakikisha wanakamilisha maabara za shule zote nchini 4587 ambazo bado hazijakamilika ili vifaa hivyo vianze kusaidia wanafunzi kwa haraka na kufikia malengo ya nchi ya kuwa ya uchumi wa kati.

Pamoja na hayo, Majaliwa amesema watendaji watakaoenda kinyume na maadili ya kazi zao ni lazima mkono wa sheria uchukue nafasi yake.

BILIONI 16.9 KUNUFAISHA SEKONDARI 1696

 Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya walimu na wanafunzi wa shule za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (mwenye tai nyekundu) akipata maelekezo toka kwa moja ya mwalimu wa masomo ya sayansi wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (mwenye tai nyekundu) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
  Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (kulia) akikabidhi moja ya kifaa cha kufundishia masomo ya sayansi kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Juhudi wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya wanafunzi wa shule za Mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam. 

Picha zote na Eliphace Marwa - Maelezo
 
 
Frank Mvungi- Maelezo 
 
Serikali imetumia shilingi bilioni 16.9 kununua vifaa vya maabara na vile vya wanafunzi wenye mahitaji maalum vitakavyonufaisha shule za sekondari 1696 ambapo shule 1625 ni za Kata na 71 ni kongwe ambazo kwa sasa zipo katika ukarabati.

Akihutubia wakati wa hafla ya kuzindua mpango wa kusambaza vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum leo Jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa inaboresha sekta ya elimu ili azma ya ujenzi wa Tanzania ya Viwanda itimie kwa kuwa Taifa litaweza kuzalisha wanasayansi kulingana na mahitaji.

“Tunatoa vifaa hivi kwa awamu ya kwanza kwa shule zilizokamilisha ujenzi wa maabara, hivyo ni matumaini yangu kuwa wale ambao hawajakamilisha watafanya hivyo ili awamu ijayo nao wapate vifaa hivi.” Alisisistiza Majaliwa.

Aliongeza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha zaidi ya shule 4,000 nchini zinakuwa na vifaa vya maabara, walimu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia na mazingira rafiki ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora itakayowasaidia kushiriki katika ujenzi wa Taifa.

Pia Waziri Mkuu ameonya kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya mtu yoyote atakaye sababisha mwanafunzi wa kike kupata ujauzito na kushindwa kuendelea na masomo ambapo atakabiliwa na adhabu ya kwenda jela miaka thelathini.

“Awe baba au mama au mtu yoyote ambaye itathibitika kuwa amemsababishia ujauzito mwanafunzi, adahabu yake ni kifungo cha miaka thelathini jela.” Alisisitiza Majaliwa.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali imetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kuendelea kununua vifaa hivyo lengo likiwa kuendelea kuinua kiwango cha elimu kwa kushirikisha wadau wa maendeleo.

“Vifaa hivi vinakidhi mahitaji ya wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na upatikanaji wa vifaa hivi ni utekelezaji wa ahadi ya serikali ya Awamu ya Tano kwa wananchi katika kuboresha sekta ya elimu na vitawaongezea wanafunzi kasi ya kudadisi na kujifunza.” Alisisistiza Prof. Ndalichako.

Akifafanua kuhusu upatikanaji wa vifaa hivyo Prof. Ndalichako aliwashukuru wadau wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia, Uingereza, Denmark na wengine kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua kiwango cha elimu nchini ili kuchochea maendeleo kwa kuwa ufaulu wa masomo ya sayansi utaongezeka.

Kwa Upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa kazi ya kupokea vifaa hivyo imefanyika kwa ufanisi na kuahidi kuwa watatekeleza jukumu la kusambaza vifaa hivyo kama ilivyopangwa kupitia Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ).


Vifaa hivyo vya maabara na vile vya wanafunzi wenye mahitaji maalum vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9 vitasambzwa katika Kanda 11 na baadhi ya mikoa itakayonufaika katika Kanda hizo ni Dar es Salaam, Katavi, Kagera, Rukwa, Pwani, Tanga, Mwanza, Singida, Dodoma.

Tuesday, 28 February 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AFUNGUA MKUTANO WA WATENDAJI WAKUU WA MASHIRIKA YA UMMA,IKULU

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa  mapema leo 28 Februari 2017, ameongoza mkutano wa siku moja wa watendaji wakuu na wenyeviti wa bodi za mashirika ya umma, unaojadili nafasi za mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Mpango wa Pili ya Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21), Unaofanyika Ikulu Jijini Dar e Salaam.

Mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina,Waziri Majaliwa amewapongeza wakuu hao ambapo amewataka kuhakikisha wanaongeza juhudi na maarifa katika mashirika yao ili kusonga mbele.

Akisoma hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wakuu hao kuongeza ubunifu zaidi ili kuongeza maarifa katika mashirika yao hii ni pamoja na kujiendesha kwa faida ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kujiendesha.

Majaliwa amelipongeza Shirika la Nyumba NHC ambalo kwa miaka ya nyuma lilikuwa likiendeshwa kwa hasara, hata hivyo baada ya kuongeza ubunifu na kuingia kijana mzawa, wameweza kupiga hatua na sasa wamekuwa wa mfano wa kuigwa huku pia akipongeza baadhi ya mifuko ya Maendeleo ya Jamii pamoja na mabenki mengine kwa ikiongozwa na benki kuu, kutokana na kuwa na menejimenti nzuri, ubunifu na kutumia wataalamu waliobobea  katika fani zao, wameweza kufanya mambo makubwa.

“Kumekuwa na dhana potofu kwamba Mashirika ya Umma hayatakiwi kufanya biashara,  na kwamba yakifanya biashara lazima yapate hasara inaendelea kubaki kuwa ni dhana potofu. Ipo mifano mbalimbali” ameeleza Majaliwa huku akitolea mifano ya nchi zilizofanikiwa kwa mashirika ya Umma  kufanya vizuri  mfano

Mashirika kama Petrobras la Brazil, Statoil la Norway, CNOOC la China ambayo ni makubwa na yameweza kuwekeza nje  ya mipaka ya nchi zao.

Majaliwa amesema mpaka sasa Serikali imeweza kuwa na Mashirika ya umma 264 ambapo kati ya Mashirika hayo, Mashirika 65 ni Mashirika ya Kibiashara, Mashirika 187 ni mashirika ya  huduma wakati mashirika 12 ni udhibiti. Kati ya Mashirika 65 ya kibiashara, Mashirika 8 yanaendeshwa kwa ruzuku ya Serikali, wakati Mashirika 57 hayategemei ruzuku ya Serikali.

Awali akifungua mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja amesema malengo ya mkutano ni kukusanya maoni ya viongozi kuhusu nafasi ya mashirika ya umma katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, kuzungumzia changamoto tarajiwa katika utekelezaji wa majukumu haya na kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

“Mashirika ya Umma yana nafasi na uwezo mkubwa wa kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano, 2016/17–2020/21 wenye kaulimbiu ‘Maendeleo ya Viwanda kwa Mabadiliko ya Kiuchumi na Maendeleo ya Watu’,” amesema Profesa Semboja.

Profesa Semboja aliongeza, “Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais John Magufuli, mkutano huu umewezakutanisha viongozi kutoka serikalini na mashirika ya umma kwa lengo la kubadilishana maarifa na uzoefu wa jinsi mashirika haya yatakavyoiwezesha Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa maendeleo endelevu.”

Mkutano huo unajadili namna ya kuboresha mifumo ya kiutendaji ndani ya mashirika na uhusiano miongoni mwa mashirika na taasisi za serikali, kufungamanisha mipango ya mashirika ya umma na Mpango wa Pili wa Maendeleo, kutathmini kiwango na aina ya rasilimali zinazohitajika kuwezesha utekelezaji wa mipango na; kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mipango.

Jumla ya washiriki 100,  kutoka wizara, mashirika ya umma na mamlaka za udhibiti takribani 52 nchini.

Thursday, 19 January 2017

WAZIRI MKUU AMALIZA MGOGORO WA MPAKA KILINDI NA KITETO


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameumaliza mgogoro wa mpaka wa ardhi baina ya vijiji vya wilaya za Kiteto na Kilindi uliodumu kwa muda mrefu.

Mgogoro huo ambao ulianza kusuluhishwa tangu mwaka 1997, umepata suluhu kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu na kuwajumuisha Wakuu wa Mikoa hiyo miwili, Wabunge wa Kiteto na Kilindi, wenyeviti wa Halmashauri na madiwani wa kata mbili za mpakani pamoja na wananchi wa kata hizo.

Waziri Mkuu pia amewataka wanasiasa na viongozi wengine kutowavuruga wananchi na badala yake wawaongoze vizuri na kutoa maelekezo kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Januari 18, 2017) wakati akizungumza na wananchi wa wilaya za Kiteto na Kilindi katika kijiji cha Lembapili wilayani Kiteto, mkoani Manyara ambako ni kuna mpaka wa wilaya hizo mbili alipokwenda kutatua mgogoro huo.

Amesema viongozi wa wilaya hizo lazima wafuate sheria na wawaelekeze wananchi umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kuheshimu mipaka iliyowekwa kwa mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro.

Akizungumzia kuhusu mgogoro huo wa mpaka, Waziri Mkuu amesema nchi ilishaweka mipaka ya mikoa na wilaya zake yote tangu zamani na kumbukumbu zipo zikiwemo za mpaka wa wilaya hizo tangu mwaka 1961 kwa tangazo la Serikali namba 65 na hakuna mabadiliko. Hivyo, aliwasisitiza wauheshimu na kuufuata.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itakwenda kuweka alama vizuri na viongozi wa wilaya hizo watashirikishwa. Alama hizo zitawekwa na kifaa maalumu, hivyo amewataka wahusika watoe ushirikiano.

Waziri Mkuu amesema katika kipindi ambacho Serikali itakuwa ikiweka alama hizo, wananchi waendelee na shughuli zao hadi hapo zoezi litakapokamilika na wala wasibughudhiwe.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa siku nane kwa watu wote wanaomiliki silaha katika wilaya za Kilindi na Kiteto wazipeleke kwenye vituo vya Polisi ili zisajiliwe upya na kisha Wakuu wa Mikoa wafanye operesheni maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume cha sheria achukuliwe hatua.

“Wakuu wa Mikoa fanyeni ukaguzi maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume na utaratibu achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria. Pia kuna watu wana mitambo ya kutengenezea bunduki hapa, nao pia waisalimishe haraka,” amesisitiza. 

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi amesema mwanzoni mwa Februari wataalamu wake watakwenda katika mpaka huo ili kuanza kuweka alama vizuri.

Amesema baadhi ya viongozi huwa wana tabia ya kuzuia watendaji kutekeleza majukumu yao, hivyo ametumia gursa hiyo kuwaomba viongozi wa wilaya hizo watoe ushirikiano.

Amesema moja ya majukumu aliyopewa na Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha ndani ya miaka hii mitano anamaliza migogoro ya ardhi nchini ukiwemo huo wa Kilindi na Kiteto.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU

Wednesday, 18 January 2017

WAZIRI MKUU MAJALIWA AFUNGUA DUKA LA DAWA LA MSD KATIKA HOSPITALI YA MPANDA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda lililogharimu sh. milioni 55 litakalohudumia mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi na Tabora.

Pia duka hilo itatoa huduma kwa vituo vya kutolea huduma za afya 580 ikiwa ni pamoja na hospitali za rufaa za mikoa miwili ya Kigoma na Tabora, Hospitali za wilaya sita za Nzega, Igunga, Urambo, Kobondo, Kasulu na Mpanda Mji.

Waziri Mkuu amefungua duka hilo la dawa la MSD, lililoko  katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi jana (Jumanne, Januari 17, 2017) ikiwa ni utekelezaji wa agizo alilolitoa kwa MSD Agosti 20, 2016 alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Katavi. Aliuagiuza  uongozi MSD kujenga duka hilo ili kurahisisha upatikanaji wa dawa katika mkoa huo pamoja na mikoa jirani.

Aidha, Waziri Mkuu amesema baada ya kufunguliwa kwa duka hilo Serikali haitarajii kusikia tena katika vituo vya afya na Zahanati zilizoko mkoani Katavi na mikoa jirani  zinakosa dawa. Amewaagiza Wakurugenzi kusimamia suala hilo na kuhakikisha vituo vyote vya afya vinakuwa na dawa za kutosha.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kukutana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kutafuta namna bora ya kutumia fedha za huduma za afya zinazipatikana katika halmashauri nchini.
 
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Katavi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.

Amesema lengo la Serikali ni kuwa na Hospitali ya Rufaa kwa kila mkoa, hivyo, Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa mipya itakayojengwa Hospitali ya Mkoa ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Laurean Bwanakunu alisema ujenzi waduka hilo la Mpanda hadi kukamilika umegharimu sh. milioni 55, huku benki ya CRDB ikitoa sh. milioni 50 na MSD imeweka dawa na vifaa tiba vya sh. milioni 104.45 na vifaa vya TEHAMA vya sh. milioni tano.

Alisema kuanzishwa kwa duka hilo kutaongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wagonjwa hasa dawa ambazo hazimo katika orodha zilizoidhinishwa na Serikali kutumika katika vituo vyake vya kutolea huduma za afya ila zimeidhinishwa kutumika nchini na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Alisema dawa na vifaa tiba vilivyomo katika orodha ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zinapatikana katika duka hilo kwa bei nafuu, hivyo kuondoa usumbufu kwa wagonjwa kwenda kuzitafuta katika maduka ya mbali na kwa bei ghali.

“Nitoe mfano mdogo wa tofauti ya dawa katika ya maduka ya MSD na maduka ya mitaani, hapa dawa ya sindano ya kutibu fungus aina ya Fluconazole inauzwa sh. 2,300 na mitaani sh. 4,500 na dawa ya sindano kwa ajili ya kushusha kisukari (Insulin) chupa moja MSD ni sh. 8,500 na mitaani sh. 20,000,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA