Monday 31 October 2016

MALINZI ATEULIWA KAMATI YA MAGEUZI CAF


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika, Issa Hayatou ameteua Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kuwa miongoni mwa wajumbe 11 wa Kamati maalumu ya mageuzi ya muundo wa CAF itakayokuwa na jukumu la kufanya mabadiliko mapya ya shirikisho, imefahamika.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, katika Kamati hiyo ikayoongozwa na Rais Issa Hayatou mwenyewe, Malinzi ameteuliwa katika Kamati hiyo iliyotangazwa leo Oktoba 30, 2016 kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

Kamati hiyo imeundwa ikiwa ni sehemu ya maazimio ya mkutano uliopita wa kawaida wa CAF uliofanyika Septemba 29, mwaka huu ambako Rais Hayatou amezingatia mjadala uliolenga kufanya mabadiliko CAF kwa kufanyia kazi mara moja.

Hayatou si tu kwamba amejali mjadala wa mkutano ule, pia ameheshimu mawazo ya vyama wanachama vya nchi pamoja na wajumbe wa Kamati ya Utendaji na wataalamu mbalimbali ili kupata mustakabali wa muundo wa uongozi wa shirikisho hilo ili kukabiliana na changamoto dhidi ya mpira wa miguu barani Afrika.

Akizungumzia uteuzi huo, Malinzi kwanza alimshukuru Hayatou kwa uteuzi huo ambao umeonyesha moja kwa moja kuwa na imani naye katika kuleta maendeleo ya mpira wa miguu katika muundo mpya.

“Lakini sifa hii ya kuteuliwa ni yangu pekee kwani ni heshima kubwa ambayo imepewa nchi yetu pendwa ya Tanzania, kadhalika nchi zote za Afrika Mashariki na Kati,” alisema Malinzi alipozungumza namtandao wa TFF ambao ni www.tff.or.tz.

Kamati hiyo itawajibika kwa Kamati ya Utendaji ya CAF ili kupata mwongozo ingawa haibanwi zaidi na Katiba ya shirikisho.

Kamati inaundwa na:

1. Issa Hayatou (Cameroon), ambaye ni Rais CAF atakayekuwa Mwenyekiti.

2. Amadou Diakite (Mali), Makamu Rais wa CAF na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho.


3. Mohammed Raouraoua (Algeria), Mjumbe wa Kamati ya Utendaji CAF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Masuala ya Sheria. Pia ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Algeria (FAF).

4. Lydia Nsekera (Burundi) Mjumbe wa Baraza la Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

5. Raymond Hack (Afrika Kusini), Mwenyekiti wa Bodi ya Nidhamu ya CAF.

6. Me. Prosper Abega (Cameroon), Mwenyekiti wa Bodi ya Rufaa ya CAF.

7. Jamal Malinzi (Tanzania), Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

8. Me. Augustin Senghor (Senegal), Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Senegal (FSF)

9. Victor Adolfo Osorio (Cap Verde), Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Cap Verde (FCF)

10. Maclean Letshwti (Botswana), Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Botswana (BFA)

11. Hicham El Amrani (Morocco) ambaye ni Katibu Mkuu wa CAF.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA