Saturday, 12 August 2017

RAIS WA JAMHURI YA KIARABU YA MISRI,MHE. ABDEL FATTAH AL SISI ANATARAJIA KUFANYA ZIARA YA KITAIFA WIKI IJAYO

Kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Abdel Fattah Al Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri atafanya Ziara ya Kitaifa nchini Tanzania wiki ijayo. Hii itakuwa ni ziara ya kwanza ya Mheshimiwa Abdel Fattah Al Sisi nchini Tanzania tangu Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aingie madarakani.

Lengo la ziara hii ni kuimarisha na kukuza zaidi mahusiano mazuri yaliyopo ya kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizi mbili, ziara hii pia itatoa fursa kwa viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili, ya kikanda na kimataifa.

Mheshimiwa Rais Al Sisi atawasili nchini kupokelewa na mwenyeji wake, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, Mheshimiwa Rais Al Sisi mchana atakuwa na mazungumzo (tete-a-tete) na mwenyeji wake kabla ya kushiriki mazungumzo rasmi (official talks) na baadae jioni Mheshimiwa Rais Al Sisi atahudhuria dhifa ya kitaifa itakayoandaliwa na mwenyeji wake.

Tanzania na Misri zina mahusiano mazuri ya kidiplomasia ya muda mrefu ambayo yamezidi kuimarika hasa katika miaka ya karibuni. Ushirikiano huu unatokana na misingi ya mahusiano na mashirikiano ya karibu sana kati ya Marehemu Baba wa Taifa na muasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kiongozi mashuhuri wa Misri na muasisi wa Jamhuri ya Taifa la Kiarabu ya Misri, Marehemu Gamal Abdel Nasser.

Uhusiano wa nchi hizi mbili umejengwa katika misingi ya ushirikiano na maelewano katika Nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiulinzi na kiusalama pamoja na medani za siasa za ushirikiano kimataifa, kutetea haki za binadamu, kuimarisha umoja na maendeleo ya Afrika, ukombozi wa Bara la Afrika na kupinga ukoloni, dhuluma na aina zote za ukandamamizaji duniani. Uhusiano huu umejengwa katika Nyanja zote za uhusiano katika sekta za huduma za kijamii na kiuchumi zikiwemo elimu, afya, kilimo, mawasiliano, usafiri, ulinzi na usalama na ushirikiano wa kimataifa.

Misri ni nchi ya pili yenye uchumi mkubwa Barani Afrika. Takwimu za mwaka 2016, zinaonesha kwamba pato la taifa (GDP) la Misri lilikuwa Dola za Kimarekani Billioni 266.213. Sekta kubwa kabisa katika uchumi wa Misri ni sekta ya huduma ( huduma za benki, mawasiliano, usafirishaji na utalii) ambayo inachangia takribani asilimia 52.5 kwenye GDP. Viwanda (manufacturing) inachangia asilimia 36.3, na kilimo asilimia 11.2.

Tanzania na Misri zinashirikiana katika ngazi za taasisi za serikali ambazo ni Taasisi ya Udhibiti wa utawala ya Misri (Administration Control Authority of Egypt) ambayo inashirikiana na Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa ya Tanzania (TAKUKURU), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja zimesaini makubaliano ya Ushirikiano na Hospitali ya El Shatby ya Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kina mashirikiano ya kubadilishana wataalamu na usimamizi wa pamoja wa Shahada za juu za uzamili na uzamivu na Chuo Kikuu cha Azhar cha Misri, Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupitia SUMA JKT wamesaini Makubaliano ya Ushirikiano na Kampuni ya Polyserve ya Misri .

Aidha, kutokana na takwimu za kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesajili jumla ya miradi nane kati ya mwaka 1990 hadi 2017, miradi hii ina jumla ya thamani ya Dola za Kimarekani 887.02 na kutoa ajira zipatazo 953, uwekezaji huo ni katika maeneo ya Kilimo, viwanda(mbao, mbolea, madini, dhahabu na shaba) na sekta ya Huduma.

Hivyo ziara hii ina umuhimu mkubwa sana hasa katika wakati huu ambapo msisitizo wa Serikali ni katika kujenga uchumi wa viwanda.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
11 Agosti, 2017.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA