Saturday 12 August 2017

UHURU KENYATTA ATANGAZWA MSHINDI WA URAIS KENYA

Tume huru ya uchaguzi Kenya (IEBC) imemtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne akipata kura 8,203,290.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati amekabidhi cheti cha ushindi kwa Kenyatta na mgombea mwenza wake William Ruto.

Akihutubia jana mara baada yakutangazwa kuwa mshindi, Rais Kenyatta amewashukuru wananchi kwa kuwa na imani naye na serikali yake.

“Nawaahidi tutaendelea na kazi tuliyoianza. Nawashukuru sana Kenya. Kadhalika, naishukuru tume ya uchaguzi kwa kazi nzuri waliyoifanya,” alisema.

“Nawapongeza wote walioshinda, na kwa walioshindwa pia tutaishi kupambana siku nyingine.”

Kwa upinzani alisema: “Sisi si maadui, ni raia wa nchi moja. Kila shindano, kutakuwa na washindi na wanaoshindwa, lakini tutasalia kuwa Wakenya. Nawapa moyo wa ushirikiano, twafaa kuungana pamoja. Wakenya wanataka sisi tufaulu.”

“Sana kwa Raila Odinga, namuomba yeye, wafuasi wake, wote waliochaguliwa kupitia upinzani, tutafanya kazi pamoja, tutashirikiana, tutakua pamoja na kuendeleza nchi pamoja.”

“Kwa Wakenya wenzangu, uchaguzi huja na kuondoka lakini Kenya itaendelea kuwepo, tukumbuke daima kwamba sisi ni ndugu na dada. Jirani yako bado ni jirani yako. Tuendelee kudumisha amani. Hakuna haja ya fujo, sisi wanasiasa pia huja na kuondoka. Lakini jirani yako atabaki.”

Katika takwimu
  • Bw Kenyatta alipata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 ya kura zilizopigwa
  • Bw Raila Odinga alipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 ya kura zote zilizopigwa
  • Waliojitokeza walikuwa 15,073,662 ambayo ni asilimia 78.91 kati ya 19m waliokuwa wamejiandikisha kupiga kura
  • Siku ya Alhamisi upinzani ulidai  kwamba Raila Odinga alishinda uchaguzi na kuitaka tume imtangaze kuwa mshindi wa urais

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA