YUSUF MANJI KUENDELEA KUSOTA RUMANDE
Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara,Yusuf Manji (41) na wenzake watatu imeahirishwa hadi Agosti 9, mwaka huu.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, aimeiahirisha kesi hiyo leo baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa, kueleza kuwa ingawa kesi ilipangwa kutajwa lakini mshtakiwa wa kwanza, Manji, yupo Mahakama Kuu
Manji aliwakilishwa na Mawakili, Mpaya Kamala, Seni Malimi na Hudson Ndusyepo.
Wakili Kishenyi aliiomba mahakama kesi hiyo itajwe Jumatano ya Agosti 9, 2017 na upande wa utetezi haukuwa na pingamizi. Upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Katika kesi hiyo, Manji na wenzake wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na Usalama wa Taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania vyenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni na mihuri.
Washtakiwa wengine ambao walikuwapo mahakamani ni Deogratius Kisinda (28), Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43).
Awali, akiwasomea hati ya mashtaka inayowakabili washtakiwa hao, Wakili wa Serikali, Tulumanywa Majigo alidai kuwa Juni 30, 2017 katika eneo la Chang’ombe ‘A’ wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na bunda 35 za vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania vyenye thamani ya Sh 192.5 milioni na kwamba mali hiyo ilipatikana kinyume cha sheria.
Katika shitaka la pili, Majigo alidai kuwa Julai Mosi, 2017 huko Chang’ombe ‘A’ washtakiwa hao walikutwa na polisi wakiwa na mabunda nane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania vyenye thamani ya Sh44 milioni mali ambayo ilipatikana isivyohalali.
Katika shtaka la tatu, inadaiwa pia kuwa katika eneo hilohilo, mnamo Juni 30, 2017, washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa na muhuri wa Jeshi la Wananchi Tanzania wenye maandishi ‘Mkuu 121 kikosi cha JWTZ’ bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Katika shitaka la nne, Wakili Majigo anadai kuwa Juni 30, 2017 kwenye eneo hilo la Chang’ombe ‘A’ Manji na wenzake hao watatu walikutwa wakiwa na mhuri wenye maandishi ‘Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma’ wakati hawana uhalali wa kuwa na muhuru huo kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Katika shitaka la tano, Manji na wenzake hao wanadaiwa kuwa Juni 30, 2017 huko Chang’ombe ‘A’ walikutwa na mhuri wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania wenye maandishi ‘Commanding Officer 835 KJ Mgambo P.0. Box 224 Korogwe’ kinyume cha sheria.
Katika shtaka la sita, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Julai Mosi, 2017 katika eneo hilo la Chang’ombe ‘A’ walikutwa na askari polisi wakiwa namba za usajili wa gari SU 383 ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.
Kwenye shtaka la saba washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Julai Mosi, 2017 kwenye eneo hilo la Chang’ombe ‘A’ washtakiwa hao walikutwa na askari polisi wakiwa na namba za usajili wa gari SM 8573 ambayo ilipatikana kwa njia isiyohalali.
0 comments:
Post a Comment