YATAMBUE MAMBO YANAYOFANYA MAISHA YAKO YA KILA SIKU KUWA MAGUMU
Kuna msemo aliwahi kuusema OScar Wilde na katika lugha yake unasomeka hivi; nanukuu,
Life is not complex. We are complex. Life is simple,and the simple thing is the right thing.
Kwa lugha yetu Waswahili msemo huu unatafsiriwa kama ifuatavyo;
Maisha hayana utata. Sisi ndio watata. Maisha ni rahisi,
na mambo rahisi ndio yaliyo sahihi.
Kwa watu wenye umri mkubwa tunafikiri kwamba, tulipokuwa wadogo maisha yalikuwa rahisi, si ndiyo?
Na sasa tunaona mambo yamebadilika na kuna ugumu umeingia katika maisha yetu ya kila siku.Naomba nikwambie kwamba, maisha bado yapo rahisi vile vile kama tulivyokuwa tunayaona utotoni na kila siku yataendelea kuwa hivyo milele.
Tofauti iliyopo ni kuwa tumeongezeka umri na hata maumbo yetu yamebadilika, na jinsi unavyoongezeka umri ndivyo tunavyozidi kuyafanya yawe magumu.
Tulipokuwa wadogo kila kitu tulikangalia katika mtazamo wa matumaini. Tulikuwa tunajua tunachohitaji na hatukuwaza tofauti juu ya mahitaji yetu kama tunaweza kukosa kitu tunachohitaji.
Tuliwapenda watu waliokuwa wanatuonyesha tabasamu. Tuliwakimbia waliotuonyesha nyuso za kisirani. Tulikuwa tunakula pale tunaposikia njaa, na kunywa pale tuliposikia kiu na kulala tulipojisikia kuchoka.
Sasa tunavyozidi kuishi sana mawazo na akili zetu zinatawaliwa na hisia hasi juu ya mahitaji yetu katika maisha kutoka katika nguvu za nje.
Kwa namna moja ama nyingine tunaanza kusita na kuhoji nafsi zetu juu ya mahitaji yetu.Pale kikwazo kipya au maumivu yanapotufika tunaanguka na kukata tamaa.
Jambo hili linatutokea mara kwa mara katika maisha yetu, na mara kadhaa tumeshajiapiza kuwa hatutaki kuanguka tena kama ilivyotokea mwanzo bila kutafuta ufumbuzi wa jambo lililosababisha kuanguka tunaishia kukwepa tatizo.
Badala yake tunatumia vitu kama chakula na pombe kutibu majeraha yetu na kujaza mapengo ya furaha zetu.Wengi wetu tunafanya kazi masaa mengi mpaka usiku wa manane, tukikimbia utatuzi wa tatizo lililotokea katika familia zetu iwe na mke au watoto.
Tunatunza hasira na visasi mioyoni mwetu, tunafanya utapeli na udanganyifu kwetu wenyewe na kwa wenzetu ili tu tusonge mbele.
Na pale mbinu zinaposhindwa kufanya kazi, tunaanza kuishi juu ya uwezo wetu, tunatumia uongo kuficha uongo, na kula na kunywa zaidi ili tu tuyafanye maisha yetu yawe na nafuu.
Katika mfumo huu wa maisha tu nazidi kuyafanya maisha yetu yawe magumu zaidi na zaidi na tunaanza kupoteza muunganiko wa nafsi zetu halisi na mahitaji yetu halisi katika maisha tunayoishi.
Kama kwa utangulizi huu umeshaanza kukuna kichwa na kujiuliza kama na wewe upo humo, hapa nakuletea mambo ambayo ukianza au kuendeleza kuyafanya yatafanya maisha yako kuwa magumu bila sababu za msingi:
1. UNAANGALIA WATU WENGINE KUKUPA MAJIBU YA MASWALI AMBAYO UNGEJIJIBU MWENYEWE.
Wakati tulipokuwa wadogo, uwezo wetu wa kujiamulia mambo yetu ulikuwa mdogo na wakubwa zetu walibeba hilo jukumu la kutuamulia kipi cha kufikiri,kipi ni chema na nini maana ya kufanikiwa.
Sasa ushakua, hupaswi kuendelea kuishi utegemezi wa fikra tena katika maisha yako.
Kuwa huru jivue gamba la utegemezi ili uanze kutumia ubongo wako katika kutoa majibu ya maswali yanayokukabili kila siku katika maisha yako.Anza kutegemea fikra zako, isikilize nafsi yako, vunja kichuguu cha utegemezi nje ya mlango wako. Mpaka sasa unajua jambo gani ni sahihi katika maisha yako.
Usiache wengine wakuamulie nini cha kuchagua kwani mwisho wa siku wewe ndio mwathirika mkuu wa maamuzi yako.Pale utakapoacha kuishi kwa kadri ya maelekezo ya watu wengine na ukaanza kuishi kwa kadri ya majibu yanayotoka kichwani mwako utapata kile kitu unachohitaji katika maisha yako.
2. UNARUHUSU WATU WENGINE WAKUFANYE UJIONE UNA HATIA KWA NAMNA UNAVYOISHI.
Ili mradi haumuumizi mtu kwa mambo unayofanya endelea kuishi kadri upendavyo na katika njia unazoona zinakupa furaha wewe mwenyewe.
Muda mwengine tunapoteza mwelekeo pale tu tunapojaribu kuishi kwa kadri ya mtazamo wa watu wengine, kujaribu kuishi matarajio yao na mambo yanayowafurahisha wao kwetu.
Chukua muda na anza kutafakari juu ya mfumo huo wa maisha. Je, unafanya mambo unayoyaamini au sababu tu uwafurahishe wengine?
Anza kukumbuka matarajio yako mwenyewe ni yapi.Kuna maneno matatu yanayopendwa kutumiwa kurahisisha tafsiri ya maisha: ISHI, FANYA na PENDA ili uwe na furaha katika maisha yako sababu uhusiano waweza kufa muda wowote ila utaendelea kuishi na nafsi yako mpaka pale maisha yako yatakapoishia.
3.UNARUHUSU WATU WABAYA WAHARIBU MAZURI YAKO.
Hata siku moja usijikie hatia kuwaondoa watu wanaokurudisha nyuma katika maisha yako. Haijalishi huyo mtu ni ndugu, mpenzi, mfanyakazi mwenzako, mwanafunzi mwenzako, rafiki wa tangu utotoni au rafiki mpya.
Hutakiwi kuweka chumba kwa ajili ya watu wanaokuletea maumivu katika maisha yako au wanaokufanya ujisikie mnyonge na mdogo.
Labda kama watabadilisha namna yao wanavyoishi na wewe ila kama haonyeshi kujali hisia zako na anaendelea kuvuka mipaka katika maisha yako na kuendelea kukuumiza,fungua mlango watoke nje hupaswi kuendelea kuwalea.
4. UNATAKA KUSHINDANA NA KILA MTU.
Ukitaka kushindana na kila mtu utakuwa mchungu kwa watu wanaokuzunguka. Kwani utaanza kujitengenezea mazingira ya kutojifunza vitu vipya na hata kurekebishwa pale panapohitaji marekebisho.
Mtu anayetaka kuwa bora hashindani na wengine ili awe bora bali anashindana kumzidi yeye wa jana ili yeye wa leo awe bora kuliko wa jana. Na niamini mimi utakuwa bora kuliko unavyodhani.
5.UNANG'ANG'ANIA KUISHI NA MAKOSA YALIYOPITA.
Ni jambo zuri sana unapojisamehe mwenyewe kutokana na makosa uliyowahi kuyafanya siku za nyuma katika maisha yako.Unapaswa uanze kuyatumia makosa yaliyopita kama funzo na ulitumie hilo kusonga mbele katika maisha yako.
Anza kutengeneza mutaskabali wako leo usiache historia ya nyuma iendelee kukutafsiri wakati majira yamebadilika.Muda mwengine malipo mazuri yanayotoka katika kujituma sio kile unachopata kwa muda huo bali kile kipya ulichojifunza ndio faida zaidi.
Usijidanganye kuwa maisha ya furaha ni yale yasiyo na shida, si kweli hata kidogo bali maisha ya furaha ni kuona unavishinda vikwazo kila vinapojitokeza na kusonga mbele.
Kd Mula anasema " MAISHA NI JINSI TUNAVYOYATAFSIRI SISI WENYEWE,IKIWA TUTAAMUA KUBADILI MTAZAMO WA NAMNA TUNAVYOYACHUKULIAAU JINSI WATU WANAVYOTAKA TUYACHUKULIE.
TUNAWEZA KUYAFIKIA MALENGO YETU"
0 comments:
Post a Comment