Tuesday 29 September 2020

UHURU WA KUJIELEZA NI MSINGI BORA WA MAENDELEO






Na Mwandishi wetu

Haki ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ni moja ya haki ya msingi ya kiraia ambayo huwapa watu haki yao ya kupata na kusambaza taarifa, haki ya uhuru wa kujieleza pamoja na haki ya uhuru wa maoni ambazo ni haki za msingi katika mataifa yanayojiendesha kwa misingi ya demokrasia. Haki ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ni chachu katika kukuza misingi ya haki za binadamu, demokrasia na utawala bora kwani husaidia raia na serikali zao kupokea na kutoa taarifa au maoni kuhusu mambo yanaoathiri maisha yao ya kila siku.

Katika maadhimisho ya mwaka huu (2020) yaliyoongozwa na kauli mbiu inayosema “Uandishi wa Habari bila Woga wala Upendeleo”.uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutoa maoni bado unaendelea kukumbana na changamoto kadhaa ambapo miongoni mwa mambo makuu yanayoathiri uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania ni pamoja na;

Uwepo wa Sheria Kandamizi kwa Wanahabari na Vyombo vya Habari; Sheria kandamizi zimeendelea kuwa kikwazo katika utekelezaji na ufurahiaji wa uhuru wa kujieleza nchini Tanzania. Mwezi Machi 2019, Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki ilitoa hukumu yake kuhusu Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, kufuatia kesi iliyofunguliwa na LHRC, Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC). Katika hukumu hiyo, Mahakama ilithibitisha vifungu vya 7(3) (a), (b), (c), (f), (g), (h), (i) na (j); vifungu vya 19,20 na 21; vifungu vya 5,36,37,38,39 na 40; vifungu vya 50 na 54; vifungu vya 52 na 53; na vifungu vya 58 na 59 kuwa vinakiuka haki ya uhuru wa kujieleza na Mkataba unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Sheria nyingine ambazo ziliendelea kuminya uhuru wa kujieleza kupitia baadhi ya vifungu vyake ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Upatikanaji Habari ya mwaka 2016, na Kanuni za Maudhui ya Mtandao. Sheria hizi zinajumuisha vifungu ambavyo havikidhi viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza. Uwepo na utekelezaji wa sheria hizi uliendelea kuchangia upunguaji wa nafasi ya ushiriki wa wananchi kwa mwaka 2019.

Adhabu Kali kwa Vyombo vya Habari; Kwa mwaka 2019 pekee, LHRC imekusanya matukio mbalimbali ya vyombo vya habari kupewa adhabu ya kufungiwa na kulipa faini kwa madai ya kukiuka Kanuni za Maudhui ya Mtandao, ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kutoendana na viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza. Vyombo hivyo vya habari ni Gazeti la The Citizen, na televisheni za mtandaoni za Kwanza

Online TV, Watetezi TV na Ayo TV. Hivi karibuni tumeshuhudia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikisimamisha gazeti la Mwananchi Mtandaoni kutochapa habari kwa miezi sita. Licha ya  kupitia changamoto hizi, hatuwezi kupuuza mchango na juhudi zinazofanya na asasi mbalimbali zikiwemo MISA-Tanzania,MCT,LHRC,TADIO na nyingine nyingi katika uzengezi,utetezi,uwakilishi na hata kusemea masuala ya uhuru wa kujieleza.Vile vile pamoja na yote serikali kwa namna yake inastahili pongezi kwa kutoa nafasi ya kusikilia na usimamizi kwa vyombo vya habari nchini kwani hata katika malezi, adhabu stahiki na za haki ni muhimu sana katika kujenga mazingira ya kuwa na kilicho bora.

Ikumbukwe kuwa vyombo vya mawasiliano ya jamii, havina budi kupewa uhuru wa kutosha pamoja na kulindwa, mintarafu sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa. Lakini, inapaswa kukumbukwa kwamba, kila haki msingi ya binadamu inawajibisha pia. Huu ni ukweli ambao hauwezi kufumbiwa macho.

Uhuru wa vyombo vya mawasiliano ya jamii havina budi kuhakikisha kwamba, vinazingatia kanuni msingi za maadili na utu wema kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na jumuiya ya mwanadamu, kama walengwa na hatima ya mchakato mzima wa mawasiliano ya jamii. Mawasiliano yasaidie kujenga na kukuza mafungamano ya kijamii kati ya watu, ili hatimaye, kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Vyombo vya mawasiliano ya jamii ni nyenzo msingi zinazotumiwa na binadamu kwa ajili ya maendeleo.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA