Monday, 1 April 2024

MAMBO 8 YA KUZINGATIA ILI KUWA BABA BORA


Hayupo mwanajamii asiyekuwepo katika Familia ingawaje wapo baadhi kutokana na mazingira mbalimbali wanajikuta wameingizwa Duniani huku Jamii inayomzunguka ikigeuka kuwa Familia pekee anayoweza kuiita hivyo; ila ni kweli, Jamii ni Familia kubwa yenye kujumuisha Familia zinazoundwa na wapenzi au hata upande mmoja na hasa zile zinazoendeshwa na mwanamke kama mzazi baada ya kuachwa na mwenzake aidha kwa kutelekezwa au namna zingine zozote.

Hivyo inaposemwa Familia ni msingi wa Jamii ni kwakuwa wazazi ni msingi wa Familia iliyojengwa na wapenzi wawili; ila wapenzi hawa wanapofikia hatua ya kuwa wazazi, ndivyo Familia huwa imekua zaidi ikijumuishwa na pande tatu ziitwazo, Baba, Mama, na Mtoto au watoto huku pengine ikijumuisha wengine nje ya hao kama vile wafanyakazi wa ndani au wanandugu au jamaa fulani.

NINI NAFASI YA BABA?
Je, kuwa Baba ni habari ya kutunukiwa? Je, familia za kisasa zahitaji Baba mwenye jukumu la kuongoza shughuli za familia kama sehemu ya mchango wake katika ndoa aliyomo? Au kuwa kwake kichwa cha familia ni tunuku isiyokuwa na jukumu kiuendeshaji mambo (just figurehead he is)? Je, hawapo wakina mama siku hizi wanaoendesha shughuli za Familia kwa ufanisi kama ilivyokuwa kwa ‘Timu ya Baba na Mama’ enzi za zamani? Je, ni sahihi Baba kubakia na jukumu la kutoa nguvu za kiuchumi kwa Familia yake huku habari zingine zikibakia kwa Mama? Ndio, haya ni baadhi ya maswali yanayohitajika katika kuzungumzia wajibu na nafasi ya Baba katika Familia zinazoendeshwa kisasa kwasababu za kuitikia kuwa maisha hayapo jana, bali yapo sasa na yatabakia kuwa hivyo wakati wote huku kinachobadilika ni vile tunavyoyaimarisha kwa mujibu wa mahitaji ya ‘sasa yetu’ katika kujengeka kwetu.


Asilimia kubwa ya kina baba hulaumu wake zao kwa malezi ya deko kwa watoto wao wakitafsiri ni muondoko wa kuwajenga kwa misingi mibovu ambayo itawafanya wawe na haiba zisizowafaa kwa ustawi mzuri wa maisha yao ya baadaye watakapokuwa watu wazima wenye kujitegemea; lakini kwa upande wa mama, nao kwa asilimia kubwa huwalalamikia waume zao kwa kutoona shughuli zote za kifamilia wakizifanya wao bila msaada pengine ukiondoa mchango wa fedha unaotimizwa na baba kwa nafasi kubwa zaidi, lakini hatahivyo, mama hupenda kuona mumewe akiendelea kuimarisha zaidi shughuli zake za kiuchumi iwe ni ajira aliyomo au biashara.

Kwa uchache tutazame  Mambo 8 ya kuzingatia ili kuwa baba bora


 Kama baba, unaweza kuwa mlezi kamili. Unaweza kumpatia mwanao malezi kamili kama mwenza wako afanyavyo. Hivyo akina baba msisite kutimiza majukumu yenu kwa kufanya kazi za kujikimu pamoja na kuwatunza watoto, wenza wenu na wengine ndani ya familia. Usiache imani za kijinsia juu ya malezi ziathiri dhamira na uwezo wako wa kumtunza mwanao, malezi ya mtoto na changamoto zake zimekuwa zikiaminiwa kuwa ni jukumu la mwanamke peke yake jambo ambalo huwanyima wazazi wa kiume nafasi ya kutoa mchango wao katika malezi na makuzi ya mtoto. Tafiti zimeonesha kuwa, ushiriki wa baba kikamilifu katika malezi una mchango mkubwa katika afya na ustawi wa mtoto.

Shiriki sawa na mwenza wako katika shughuli zote za malezi ya watoto wenu. Usiogope kutumia muda wako vizuri na mwanao wa kike au wa kiume na kufanya kazi zote kama vile kunepisha, kupika, kucheza nao na kuwabembeleza wanapolia. Watoto siku zote hukumbuka matendo haya na hivyo kujenga upendo kati yenu na kuzidisha amani kwa familia. Ni vyema kuhamasishana wake kwa waume ili kila mmoja wetu ajione ana uwezo wa kutekeleza majukumu ya malezi na kutafuta pesa kwa pomoja.

Wajengee wanao uwezo wa kutekeleza majukumu bila kujali mipaka ya kijinsia. Wapende wanao na uwakubali walivyo, usitumie nguvu kuwabadli. Jitahidi kuwapa malezi yenye kuondoa mila potofu na kuleta usawa wa kijinsia katika majukumu kwa wewe kuwa mfano.

Jijengee heshima na upendo kwa watoto wako na siyo nguvu na umangi-meza. Kila mtu hufurahia kupenda na kupendwa na unaweza kupata upendo wa watoto wako kwa kuwapenda na si kwa kuwaonesha mabavu na umangi-meza. Ubabe unaambulia nidhamu ya uoga na sio heshima na utii wa kweli. Hivyo ni vyema kwa wazazi wa kiume kuonesha upendo, heshima na uwajibikaji kwa watoto, mwenza wako na familia kwa ujumla. Kumbuka kwa kufanya hivi unajenga msingi wa tabia za mwanao unayemtaka kwa miaka kadhaa ijayo. Yakupasa kuishi kama mfano wa kuigwa kwa watoto wako kwa kupitia malezi unayowapa, matendo unayotenda kwa familia, jinsi unavyotatua migogoro baina yako na mwenza wako, lugha unayotumia n.k. Mabinti na vijana wakimuona baba yao katika hali ya utu, heshima, asiyetumia ukatili na mwenye mahusiano yenye usawa huiga na kurithisha usawa katika vizazi vyao.

Kuna kuteleza na kuanguka katika kutekeleza jukumu la malezi. Usikatishwe tamaa na chanagamioto unazokumbana nazo au makossa yanayojitokeza katika jitihada zako za kulea. Kulea hakujawahi kuwa rahisi lakini tunajifunza siku hadi siku.

Kuwa baba ni zaidi ya kucheza na mwanao. Kuwa baba na kutekeleza jukumu la malezi huanza mtoto angali tumboni. Huhusisha ushiriki wako katika kutunza mimba, kumsaidia mwenza wako katika kipindi hiki na kumuonesha upendo kwa kumsaidia majukumu ya malezi. Ingawa kucheza na mwanao ni muhimu, vivyo hivyo kushiriki kazi za nyumbani na malezi ya watoto, hujenga ari ya kujituma na kuleta usawa wa kijinsia kwa watoto wa kiume na kumjengea mtoto wa kike uwezo wa kujitegemea na kujiamini. Tafiti zimeonesha kuwa mabinti waliolelewa na baba wanaojihusisha na shughuli za nyumbani wana nafasi kubwa ya kuwa wachapakazi na kujikita katika ajira zenye maslahi makubwa.

Mazungumzo na mijadala ya wazi kati yako na mwenza wako ni nguzo ya malezi. Mara zote zungumzeni kuanzia mambo madogo na hata mipango mikubwa katika familia. Namna hii mnawasaidia watoto wenu kujua umuhimu wa kufikia maamuzi kwa mazungumzo. Kukubaliana na kutokukubaliana.

Wasikilize watoto wako, jadiliana nao na wawezeshe kupitia sauti zao. Jambo muhimu ambalo akina baba wengi wanapaswa kuzingatia ni kuwasikiliza watoto wao kwa makini. Kuyapa uzito mawazo yao na kushirikiana nao katika kufanya maamuzi. Walee wanao katika namna ya kujihisi kuwa na uwezo wa kupambana na changamoto na kujiskia wamewezeshwa. Ukiwafunza wanao kuwaheshimu watu wote na kuwatendea usawa basi unawajenga kuwa wanastahili kesho bora yenye fursa na usawa.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA