Monday 21 February 2022

KAMATI YA MIUNDOMBINU YAIPONGEZA SERIKALI MRADI WA BANDARI YA TANGA

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Seleman Kakoso, akisisitiza jambo kwa uongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), wakati kamati hiyo ilipotembelea Bandari ya Tanga
mwishoni mwa wiki.



Sehemu ya mitambo na vifaa vya kuhudumia meli na shehena bandarini iliyonunuliwa ikiwa ni sehemu ya mradi wa maboresho ya Bandari ya Tanga.

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Seleman Kakoso ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha za kuboresha bandari ya Tanga ili kuifanya kuwa na hadhi ya bandari ya Kimataifa. 

Ametoa kauli hiyo jijini Tanga mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa bandari hiyo na kuwataka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuhakikisha idadi ya mzigo inaongezeka zaidi ili kukuza uchumi wa Mkoa. 


“Naipongeza sana Serikali ya awamu ya sita inafanya makubwa kwani Mkoa wa Tanga ulikuwa umepoa sana, ni imani yetu kuwa mradi huu utakapokamilika shehena itaongezeka na kukuza pato la Mkoa na Taifa kwa ujumla", amesisitiza Mwenyekiti Kakoso. 


Mwenyekiti Kakoso ameongeza kuwa Wizara kupitia TPA inapaswa kumsimamia kwa karibu Mkandarasi Kampuni ya China Harbor Engineering Company (CHEC) ili akamilishe mradi kwa wakati na viwango. 


“Mkandarasi ametuhakikishia kuwa mradi huu utakamilika mapema mwezi wa tano lakini sina imani kama utakamilika sababu kasi yake bado haijaridhisha sana, hivyo mkasimamie eneo hili kwa karibu", amesisitiza Mwenyekiti Kakoso 


Mwenyekiti Kakoso ametanabaisha umuhimu wa Sekta ya Uchukuzi kutazama upya mikataba ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha kipengele cha huduma kwa jamii kinakuwepo ili kuwanufaisha wananchi wanaozunguka miradi husika. 


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Atupele Mwakibete, amemuhakikishia Mwenyekiti wa Kamati na Wajumbe kuwa Serikali itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Karim Mataka ameihakikishia Kamati hiyo kuwa maoni yote na maelekezo yaliyotolewa kwa Mamlaka yatashughulikiwa kwa karibu ili kuhakikisha miradi yote ya bandari inakuwa na tija na kuongeza pato la Taifa. 


Mradi wa upanuzi wa bandari ya Tanga utatumia fedha za ndani kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni 400 na unahusisha ujenzi wa gati mbili zenye urefu wa mita 450, ununuzi wa mitambo na vifaa vya kuhudumia meli na shehena, ukarabati wa maghala na sehemu ya kuhudumia shehena na  mradi wa kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia na kugeuzia meli.


(imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA