KWA KIASI KIKUBWA,HAYA NDIO MAMBO YANAYOCHANGIA MTU KUVUNJIKA MOYO
Kuna siku niliwahi kukaa na kujiuliza, ilikuwaje kati ya viungo vyote mwilini,MOYO ndiyo uteuliwe kuwakilisha hisia zote za binadamu (pengine sasa unajiuliza pia).
Ukiwa katili, mpole, mkarimu, mwizi, au jasiri bado utatumika moyo kubeba hizo sifa. Si kitu cha ajabu kusikia mtu anapewa sifa ya kuwa na Moyo mgumu, moyo mwepesi au moyo wa tamaa.
Nilipochunguza kwa kusoma vitabu vya kisayansi nikagundua kuwa Moyo ndiyo kiungo cha kwanza kuishi na cha mwisho kufa kwa binadamu,ndio maana kimepewa nafasi hiyo.
Kutokana na kiungo hiki kubeba matukio mengi muhimu katika maisha yetu ni vyema tukakitunza.
Hivi ni kweli moyo huvunjika?
Kisayansi haiwezekani, lakini amini usiamini, kihisia ni kweli moyo unavunjika.Na mtu ambaye inasemekana moyo wake umevunjika, raha ya maisha kwake haipo.
Kuna matukio yanayoongoza kuvunja mioyo ya binadamu, Hebu tuyaangalie na tuanze kuyakwepa:
1.KURUHUSU WATU WABATILISHE UNAVYOJISIKIA
Kama kuna kitu unajisikia, ni kweli ndivyo kilivyo. Hakuna kingine watu watakachosema chenye uwezo wa kubadilisha hilo. Hakuna anayeishi ndani yako zaidi ya wewe mwenyewe.
Hakuna anayeweza kuelezea hisia zako zaidi ya wewe mwenyewe, usiruhusu mtu akuhukumu kwa ulilofanya kwa kuwa hajui ulikuwa katika hali gani. Usiruhusu watu wakuaminishe tofauti na wewe unavyojisikia.
2.KUJUTIA KILA KOSA
Yaani kama mpaka leo bado unaendelea kujutia kosa ulilofanya muda mrefu uliopita unajivunja moyo wako.Kumbuka katika kipindi ulichokosea, ulifanya kutokana na uelewa na uzoefu uliokuwa nao muda ule na sio sasa.
Yawezekana kabisa, uchanga wa akili ndio ulikufanya ufanye vile ulivyofanya, na ndio maana kama ungepewa nafasi ya leo kufanya maamuzi uliofanya miaka iliyopita usingefanya kama vile hata kidogo.
Muda na uzoefu vinatupa nafasi ya kufanikiwa katika yale tunayoyafanyia maamuzi,kwa hiyo sahau yaliyopita songa mbele.
3.KUWAPOTEZEA WANAOKUPENDA
Unajua kuna kipindi unakuwa na watu wanakuonyesha upendo halafu wewe unashindwa kuwaonyesha shukrani.Hii ni sawa na kujiandalia bomu ambalo litakuja kukulipukia siku ile watakapoondoka kabisa machoni pako.
Na kuna kipindi, utatamani angekuwepo karibu yako umueleze unavyojisikia au akikusaidia shughuli fulani.Unatakiwa umuonyeshe shukrani yule anayekufanyia upendo kila muda utakaopata.
4.KURUHUSU MATAMANIO KUKUTAWALA
Kuna kipindi tunafanya uamuzi mbaya, sio kwasababu ni wabaya ila ni kwasababu tumejali zaidi kuwafurahisha wengine kuliko fahari yetu.Unapokubali kufanya uamuzi wa tamaa ya kutaka uonekane mtu fulani ni kujitengenezea uasi wa ndani.
5.KUTAKA KUBISHANA KILA HOJA
Kuwa shujaa sio kupigana kila vita inayokuja mbele yako, au si kujibu kila shutuma dhidi yako.Kama unaona hilo jambo litakushushia heshima na utu wako, ni heri ukaachana nayo ili yasiweze kuzaa mengine mapya na mabaya zaidi.
6.KUHARAKISHA UHUSIANO
Uhusiano mzuri ni wa watu ambao kila mmoja amempokea mwenzake kwa hali yake aliyonayo, na kumsaidia atoke hapo alipo kwenda katika hali iliyobora zaidi ya aliyomkuta nayo.
Usikimbilie kuwa katika uhusiano na mtu kwa kuwa, mazingira au nafasi imetokea tu.Tafuta mwenza ambaye atakuhimiza kukua,asiyeng'ang'ania ufanye anachopenda yeye kila wakati,atakayekuruhusu uchangamane na watu wengine, na atakayekuamini.
7.KUMNG'ANG'ANIA ANAYETAKA KUONDOKA
Ni uchungu sana, kumuaga mtu unayetaka abaki,lakini ni maumivu zaidi kumng'ang'ania anayetaka kuondoka.
Kama unayemuonyesha upendo na, hataki kurudisha upendo kwako usikae kulazimisha kwani utaendelea kujiumiza tu na kuwa mtumwa kwake.Mtu pekee unayepaswa kuwa naye ni yule anayekuheshimu na anatambua umuhimu wako katika maisha yake.
8.KUKATAA KILA USHAURI
Si kila ushauri utakao pewa utakuwa sahihi sawa,lakini si kila ushauri utakuwa mbaya kwako.
Kubali kupokea marekebisho kutoka kwa watu wengine.Usijitengenezee mazingira ya kuja kuuvunja moyo wako siku zijazo kwa kujuta.
Kd Mula anasema: Tukiwa tunaelekea mwisho wa mwaka 2017 huenda umekutana au umepitia baadhi ya niliyoyajadili na kuwa miongoni mwa waliovunjika moyo. Nikueleze tu ukweli maadam unaishi hapa duniani utakutana na mengi yatakayo kuumiza kwa namna moja au nyingine Lakini nikutie moyo kuwa unayo nafasi ya kushinda na Kuifufua furaha na amani moyoni :::RAHA YA MAISHA NI KUISHI KWA AMANI NA FURAHA,
KAMA UTAENDELEA KUJIWEKA KATIKA MAZINGIRA YA KUJA KUUVUNJA MOYO WAKO, HAUTAONA LADHA YA MAISHA KAMWE , AMUA SASA 2018 KWAKO UWE MWAKA WA TOFAUTI.
ANZA LEO KUUTUNZA MOYO WAKO.
Usisite kuniandikia maoni yako na pia ni vyema ukamshirikisha na mwingine nakutakia wakati mwema.
0 comments:
Post a Comment