HII NDIO TOFAUTI KATI YA WAONGOZAJI WA NDEGE NA WAEGESHAJI WA NDEGE
Waegeshaji wa ndege ni wataalamu wanaofanya kazi katika maeneo ya maegesho ya ndege viwanjani. Mara nyingi huonekana wakiwa wamevaa mavazi maalum ya usalama na kutumia vijiti vya mwanga au ishara za mikono kumwelekeza rubani wakati ndege inapokaribia sehemu ya maegesho au inapojiandaa kuondoka.
Jukumu lao ni kuhakikisha ndege inaelekezwa kwa usahihi katika eneo lililotengwa bila kuhatarisha usalama wa ndege, vifaa vya uwanja, majengo au watu waliopo katika mazingira ya karibu. Ishara wanazotumia hutambulika kimataifa na humsaidia rubani kufanya maamuzi sahihi hasa katika maeneo ambayo mwonekano kutoka ndani ya ndege unaweza kuwa na mipaka.
Historia ya kazi ya uegeshaji wa ndege inaanzia katika miaka ya mwanzo ya maendeleo ya usafiri wa anga, ambapo mawasiliano kati ya marubani na wahudumu wa ardhini yalitegemea zaidi ishara za mikono. Pamoja na maendeleo ya teknolojia katika viwanja vya ndege, kazi ya Aircraft Marshaller bado inaendelea kuwa sehemu muhimu ya shughuli salama za ndege ardhini.
Kwa upande mwingine, Waongozaji wa Ndege, au Air Traffic Controllers, wana jukumu la kusimamia na kuratibu mwendo wa ndege angani na katika maeneo maalum ya viwanja vya ndege. Hutumia mifumo ya mawasiliano, ufuatiliaji na taratibu za uongozaji wa ndege kuhakikisha ndege zinatenganishwa kwa umbali salama na kupewa maelekezo wakati wa kuruka, kutua na kujiendesha katika maeneo wanayoyasimamia.
Tofauti kubwa kati ya wataalamu hawa ni kwamba Air Traffic Controllers huongoza na kuratibu mwendo wa ndege kupitia mawasiliano ya redio na mifumo ya uongozaji, wakati Aircraft Marshallers humwelekeza rubani kwa ishara za kuona katika eneo la maegesho ya ndege.
Pamoja na tofauti hiyo ya majukumu, wataalamu hawa wote ni sehemu muhimu ya mfumo wa usalama wa usafiri wa anga na huchangia kuhakikisha shughuli za ndege zinafanyika kwa mpangilio, usalama na ufanisi.
Nchini Tanzania, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ina jukumu la kusimamia na kudhibiti usalama wa usafiri wa anga kwa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vinavyotambuliwa kitaifa na kimataifa, ikiwemo miongozo ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga, ICAO.

.jpg)


0 comments:
Post a Comment