TCAA YAPONGEZWA KWA MABORESHO YA HUDUMA NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA SEKTA YA ANGA
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imepongezwa kwa kuendelea kusimamia sekta ya usafiri wa anga kwa ufanisi na kuimarisha utoaji wa huduma kupitia mifumo ya kisasa ya kidijitali.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Uchukuzi Mh. Prof.Makame Mbarawa aliyekuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Nne la Kimataifa la Sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji, linalofanyika tarehe 20 na 21 Agosti 2026 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ambalo TCAA imeshiriki, pindi alipotembelea banda la TCAA.
Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), Aristid Kanje akimuelezea Mhe. Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb) alipotembelea wakati wa Kongamano la Nne la Kimataifa la Sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji, linalofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam
Awali akiwa katika banda la TCAA, Prof. Mbarawa alipokewa na Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), Aristid Kanje, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Dkt. Jabiri Bakari, ambaye alimweleza kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Mamlaka katika kusimamia na kuendeleza sekta ya usafiri wa anga nchini, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma.
Kanje pia alimweleza Mh. Waziri kuhusu mfumo wa huduma za kielektroniki unaofahamika kama "Civil Aviation Services Portal (CASP)" unaowawezesha wadau wa usafiri wa anga kupata huduma kwa haraka na kwa ufanisi zaidi, pamoja na Dawati la Huduma kwa Wateja linalowezesha kupokea na kufuatilia maoni na changamoto za wadau.
Kongamano hilo limeandaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na limewakutanisha wadau kutoka sekta ya umma na binafsi kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, maarifa na kujadili fursa na changamoto katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji nchini.



0 comments:
Post a Comment