Kifo cha meneja wa Ewura utata mtupu
Dar/Dodoma. Wakati kukiwa na utata wa kifo cha Meneja wa Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imebainika kuwa tofauti ya takwimu kati ya mamlaka hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliyotolewa kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti ni Sh25 bilioni.
Meneja huyo, Julius Gashaza alikuwa akihudhuria kikao kilichokuwa kikijadili tofauti hiyo bungeni Dodoma na baadaye aliporudi Dar es Salaam akakutwa amejinyonga hotelini huku ikielezwa kuwa alirudi akiwa amejawa hofu na kukosa amani.
Vyanzo vyetu ndani ya kamati hiyo vimeeleza kuwa tofauti iliyobainika katika hesabu za taasisi hizo za Serikali ni lita 11,755,161, ambazo zingeuzwa kwa bei ya sasa ya petroli mkoani Dar es Salaam ya Sh2,200 zingepatikana Sh25.86 bilioni.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, takwimu za
TRA zinaonyesha kuwa kati ya Julai 2013 hadi Machi mwaka huu, kiasi cha
mafuta kilichoingizwa nchini kilikuwa lita 2,189,240,000 wakati Ewura
ilionyesha ni lita 2,177,484,839.
Hata hivyo, baada ya utata huo na
Kamati ya Bajeti chini ya Andrew Chenge kuitaka Serikali itoe ufafanuzi
wa tofauti hizo, Serikali iliwasilisha taarifa yake Jumapili ikisema
takwimu zote ni sawa.
Katika ufafanuzi wake, Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba alisema uhakiki wa takwimu hizo ulibaini kuwa
zote zilikuwa 'sahihi' na kwamba tofauti iliyopo inatokana na upimaji wa
mafuta.
Nchemba alikaririwa akisema TRA hupima
mafuta kwenye meli mara inapoingia na kukadiria kodi wakati Ewura
hupima mafuta yanapopokewa kwenye matanki.
"Kwa kuwa wakati mwingine meli hutumia
muda mrefu tangu zinapoingia hadi zinapoteremsha mafuta, sehemu ya
mafuta ambayo TRA huhesabu kama yameingizwa katika mwezi mmoja wakati
Ewura hupata takwimu za kiasi cha baadhi ya mafuta hayo katika mwezi
unaofuata na hiyo ndiyo iliyosababisha kuwapo kwa tofauti hiyo ambayo
hata hivyo ni ndogo."
Kulingana na takwimu hizo, kiasi cha
mafuta kilichoonyeshwa na TRA kilikuwa juu kuliko kile kilichoonyeshwa
na Ewura na haijajulikana iwapo kutofautiana huko kwa takwimu kuliifanya
Serikali kumweka kitimoto Gashaza.
Alikuwa na hofu
Sintofahamu imeendelea kugubika kifo
cha Gashaza na sasa imeelezwa kuwa alirudi kutoka Dodoma akiwa amejawa
hofu na kukosa amani.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix
Ngamlagosi alisema jana kuwa ingawa hakuzungumza na Gashaza baada ya
kurudi kutoka Dodoma, taarifa za polisi na kutoka kwa mkewe zinaeleza
kuwa alirudi akiwa na hofu na ndiyo sababu ya kuondoka nyumbani kwake na
kwenda kulala hotelini
"Tumepata mshtuko mkubwa kuhusu msiba
huu. Ndiyo maana tunataka kujua alikuwa na hofu ya nini na kwa nini.
Kama alitishiwa maisha ni watu gani walimtishia maisha. Ndiyo majibu
tunayoyataka kutoka kwa wanausalama," alisema Ngamlagosi.
Mkurugenzi huyo alisema si kweli kuwa
marehemu Gashaza alikwenda bungeni kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya
Bajeti, bali alikwenda kuhudhuria mkutano wa kawaida ambao haukuwa
ukihusisha Ewura na tuhuma zozote.
"Gashaza alikwenda kuniwakilisha,
hakwenda kwa minajili ya kuhojiwa, Ewura iliitwa kushiriki mkutano wa
kawaida, ambao ni miongoni mwa taratibu za kawaida za kazi," alisema.
Ngamlagosi alisema kifo cha Gashaza
bado ni kitendawili kikubwa ambacho kinaweza kufumbuliwa na watu wa
usalama pekee, kwa kuwa meneja huyo alikuwa mwadilifu na tegemeo kubwa
kwa mamlaka hiyo.
"Tunamfahamu kama mtu ambaye si
mwepesi kurubuniwa kwa lolote lile, hakuwahi kukumbwa na kashfa yoyote
ile tangu aanze kazi hapa mwaka 2007," alisema na kuongeza:
"Ameleta mabadiliko makubwa kwenye mamlaka. Mpaka sasa hatujui nini au nani amemkwaza."
Alisema Gashaza alikuwa mwadilifu kwa
kiasi kikubwa licha ya kuwa alikuwa akifanya kazi kwenye kitengo nyeti
cha ukaguzi wa mafuta ambako majukumu yake makuu yalikuwa ni kuangalia
ubora, miundombinu, biashara, bei na ununuzi wa mafuta, kusimamia
uingizwaji wa mafuta nchini, utoaji wa leseni na kuangalia jinsi
wafanyabiashara wanavyofanya kazi.
Mhudumu wa gesti
Mhudumu wa gesti ya Mwanga Lodge
ambayo Gashanza alipanga kabla ya mauti kumkuta, Ngina Riwa alisema
mteja wake huyo alifika Jumamosi saa 3:00 usiku na kupanga chumba namba
113.
Alisema baada ya muda mfupi walifika
watu watatu, wanawake wawili na mwanamume mmoja na kuonana na mteja wao
na baada ya kushauriana kidogo wakaingia naye chumbani.
"Huko chumbani hawakukaa sana na
haikuzidi hata nusu saa na baadaye yule mteja akatoka nao kuwasindikiza.
Hakufika mbali, akarudi tena na kuingia chumbani.
Riwa alisema wakati mteja wake anaingia chumbani kulala ilikuwa takribani saa nne usiku na hakutoka tena.
Alibainisha kuwa asubuhi kati ya saa
12:30 na 1:00 asubuhi alikuja tena yule rafiki yake mwanamume kumulizia
mteja wake kama alikuwa ameamka.
"Alikwenda kumgongea lakini
hakufungua, akarudi kwangu tukaenda naye tukagonga hakufungua, ndipo
tukashirikiana na mlinzi kufungua dirisha kwa nje na kumwona akiwa
amelala chini.
"Tukawapigia simu polisi kutoka Kituo
cha Ali Mboa ambao hawakuchukua muda wakaja. Baadaye wakaja polisi wenye
vyeo vya juu wakapimapima wakaondoka na mlinzi na bosi wetu kama saa
tatu asubuhi hivi," alisema mhudumu huyo.
Uchunguzi wa polisi
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke,
Engbert Kiondo alisema uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho unaendelea kwa
kuangalia maeneo matatu.
Alisema utajielekeza kubaini kama
kulikuwa na mgogoro wowote wa kifamilia au iwapo alikuwa na tatizo
lolote kazini kwake kabla ya kifo chake na mazingira kilipotokea kifo
hicho na baada ya kujiridhisha watatoa taarifa kamili kwa vyombo vya
habari.
"Kuna maswali mengi ya kujiuliza kwa
nini hakutaka kulala nyumbani kwake usiku ule badala yake akaamua kulala
hotelini, tunafanya upelelezi kubaini nini hasa kilimsukuma
kujinyonga," alisema.
Alisema pia wanasubiri ripoti ya uchunguzi ya daktari ambayo wataitumia katika upelelezi wao kubaini chanzo.
Alisema polisi watachunguza kama Gashaza alijinyonga kweli au aliuawa na kutengenezewa mazingira ya kujinyonga.
Ampigia simu rafiki yake
Kiondo alisema Gashaza alipofika
katika nyumba ya kulala wageni, alimpigia simu rafiki yake wa karibu
anayeitwa Sibitwango na kumweleza kuwa mambo yamekuwa magumu na
hakujisikia vizuri.
Usiku huo, Kiondo alisema Sibitwango
pamoja na mke wa marehemu Judith walimfuata katika hoteli aliyofikia na
kumsihi arudi nyumbani akapumzike lakini yeye (Gashaza) alisisitiza
kulala hapo kwa sababu tayari alikuwa ameshalipia chumba hicho
Kiondo alieleza kuwa siku iliyofuata Sibitwango mwenyewe ndiye aliyetoa taarifa polisi na kueleza mazungumzo yao kabla ya kifo.
Utata bungeni
Wakati inaelezwa kuwa kulikuwa na
tofauti ya takwimu kati ya zile za TRA na Ewura kuhusu kiwango cha
mafuta kilichoingia kwenye soko, taarifa zaidi zimeeleza kuwa katika
kikao cha Kamati ya Bajeti, Gashaza hakuulizwa swali hata moja.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo
alisema marehemu hakuhojiwa labda kilichomfanya ajiue ni hofu
iliyotokana na mahojiano baina ya kamati hiyo na watendaji wa Wakala wa
Nishati Vijijini (Rea).
Alisema kamati hiyo iliwaita viongozi
wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Nishati na Madini ili kuwahoji kwa nini
Sh50 zilizoongezwa katika mafuta ya petroli na dizeli hazikwenda Rea?
Mjumbe huyo alisema kati ya zaidi ya
Sh100 bilioni zilizotakiwa kwenda Rea ni Sh17 bilioni tu zilizopelekwa
na fedha nyingine zilielekezwa kwenye matumizi mengine ambayo
hayakuidhinishwa na Bunge.
Imeandikwa na Daniel Mjema, Sharon Sauwa na Fidelis Butahe, Florence Majani, Nuzulack Dausen na Peter Elias
0 comments:
Post a Comment