MAMA MJAMZITO AFARIKI DUNIA KWA KUNYWA SUMU
MAMA mjamzito
aliyekuwa na mimba ya miezi tisa, Anjela Domiano (42), mkazi wa
Nanenane katika Manispaa ya Morogoro, amefariki baada ya kunywa sumu ya
panya.
Tukio hilo lilitokea juzi, saa 2.30 asubuhi, katika eneo la Kichangani katika Manispaa ya Morogoro.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alisema jana kuwa, marehemu
Angela alifia katika hospitali ya mkoa, ambako alipelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Alisema siku ya tukio, Angela alikutwa akiwa ameanguka huku akitapatapa katika eneo la Kichangani.
Alisema
polisi walipata taarifa na kufika katika eneo la tukio na kumchukua
mama huyo na kumfikisha katika hospitali hiyo, ambapo alifariki wakati
akipatiwa matibabu.
“Wasamaria
wema walipomwona mama huyo kaanguka chini, walitoa taarifa polisi na
walipofika eneo la tukio, walimkuta akiwa anatapatapa na kuamua
kumkimbiza hospitali ili kuokoa maisha yake,” alisema.
Alisema
Angela alikutwa na sumu ya panya katika pochi yake na uchunguzi wa
awali umeonyesha kuwa, alifariki kutokana na kunywa sumu hiyo.
Kamanda huyo alisema hawakuweza kumhoji Anjela kutokana na hali yake kuwa mbaya na wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.(E.L)
0 comments:
Post a Comment