Siri ya watoto kupotea, kuibwa yabainika
Mkazi wa Kyela mkoani Mbeya, Mboka Mwakikagile (20) akiwa na mtoto
wake Godluck Mwangosi katika Hospitali ya Rufaa Meta ya jijini Mbeya
baada ya polisi kumkamata mtu anayedaiwa kumwiba mtoto huyo. Picha ya
Maktaba
Dar es Salaam. Kwa
muda mrefu kumekuwapo na taarifa za watoto kupotea katika mazingira
tofauti, huku baadhi yao wakipatikana na kuunganishwa tena na wazazi
wao, lakini wengine hawajaonekana hadi leo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika mikoa mbalimbali nchini
kubaini sababu za watoto hao kupotea, umebaini kuwa baadhi ya watoto
huondoka nyumbani baada ya kutokea ugomvi kati ya wazazi au walezi wao.
Sababu nyingine ni kuibuka kwa biashara ya watoto wanaouzwa kwa watu
ambao hawana watoto, nchini na nje ya nchi na imani za kishirikina
zinazochochewa na waganga wa jadi.
Taarifa kutoka polisi zinasema kuwa baadhi ya watoto walioripotiwa
kwenye vituo vya polisi kupotea au kuibwa, walibainika kuchukuliwa na
mmoja wa wazazi wa mtoto kuto
Zaidi ya watoto 61 waliripotiwa kuibwa Dar es Salaam katika ya mwaka 2012 na 2013, kati yao wa kiume 28 na wa kike 32.
Taarifa kutoka Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inaeleza kuwa mwaka
2012 kulikuwa na kesi 29 za wizi wa watoto, ambapo kati yake watoto
wanne wa kiume waliibwa hospitalini na watano wa kike walichukuliwa
wakiwa nyumbani. Watoto saba pekee kati ya wote walioibwa ndiyo
walipatikana.
Mwaka jana kulikuwa na kesi za wizi wa watoto 31, kati yao wa kiume
wawili walichukuliwa na watu wasiofahamika wakiwa hospitalini na 17
wakiwa nyumbani. Pia watoto wa kike 12 walipotea mwaka huo. Hadi kufikia
Desemba 2013, watoto 21 walikuwa wamepatikana, ambapo kati yao wa kiume
11 na wa kike 10.
Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Camillius Wambura anasema watoto
wachanga ndio wanaoibwa huku wenye umri mkubwa kidogo hupotea kutokana
na sababu mbalimbali zikiwamo uzembe wa wazazi. Wambura anasema baadhi
ya wazazi waliiba watoto wachanga kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa
kuzaa, tabia iliyokomaa kutokana na wazazi wa aina hiyo kushindwa
kukubali hali waliyonayo.
Akitoa mfano anasema kuwa mama mmoja aliiba mtoto mwenye umri wa wiki
mbili Dar es Salaam, lakini alikamatwa siku chache baadaye mkoani Rukwa.
“Huyu mama alikuwa akiishi Rukwa, alimrubuni mume wake kuwa ana
ujauzito, hivyo kwa kuwa siku za kujifungua zilikuwa zimefika alimwambia
mumewe anataka kuja Dar es Salaam kujifungua kumbe alikuwa anakuja
kuiba mtoto,” anasema.
Mama huyo alipomwiba mtoto alimpa rafiki yake atangulie naye Morogoro
ambapo alikwenda kumchukua na kwenda naye Rukwa, hata hivyo mtoto huyo
alifariki dunia baadaye. Wambura anazitaja sababu za watoto kupotea kuwa
ni pamoja na watoto kutoroka nyumbani baada ya kukithiri kwa migogoro
kwenye ndoa na wazazi kutokujali watoto wao.
“Ndoa nyingi zipo kwenye migogoro ambayo haiwahusu watoto, lakini
wanaishi kwenye mateso. Usiombe kuishi kwenye nyumba yenye mateso,”
alisema.
Anasema baadhi ya watoto wapo tayari kuishi kwenye vituo vya kulelea
watoto kuliko kukaa na wazazi wao, ambao wanagombana kila siku.
Anaongeza kuwa baadhi ya wazazi hawawajali watoto wao, kisha anatoa
mfano huu: “Tuliwahi kukaa kituoni na mtoto wa miaka mitatu kwa wiki
mbili, hakuna mtu yeyote anayekuja kumuulizia. Tukaja kubaini alikuwa
anatoka karibu kabisa na kituo, tulipowauliza wazazi mtoto wenu yuko
wapi? Walituambia tulijua akiokotwa ataletwa.”
Kamanda huyo anasema dawa ya watoto kutokupotea ni wazazi kuwapenda
watoto wao, kusimamia michezo yao, kujua wanakula nini na wanakwenda
wapi.
“Tuwafanye watoto wetu watuone sisi ni wazazi bora kuliko wengine,” alisisitiza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime anasema jumla ya matukio
24 ya kupotea kwa watoto yaliripotiwa Polisi katika kipindi cha kuanzia
Januari 2013 hadi Aprili 2014.
Misime anasema kuwa watoto wote waliopotea walipatikana kwa nyakati
tofauti ingawa hakueleza walikuwa katika hali gani na kwamba waliohusika
walichukuliwa hatua gani.
“Taarifa hizo zimekuwa zikiletwa na wazazi na walezi wa watoto hao, na
sababu za kupotea kwao tumebaini zinatokana na watoto hao kwenda mbali
na maeneo ya makazi wanayoishi,” anasema.
Alitaja maeneo yenye matukio mengi ya kupotea kwa watoto kuwa ni machungani, shuleni na katika maeneo ya uwindaji.
Taarifa kutoka Tanga zimeeleza kuwa kati ya mwaka 2012 hadi Aprili 2014
jumla ya watoto 63 waliripotiwa kupotea katika mazingira tofauti.
Watoto waliopotea na wilaya zao kwenye mabano ni 31 (Handeni), wawili
(Pangani), Saba (Korogwe), tisa (Tanga Mjini), wanne (Muheza), watano
(Lushoto), wawili (Kilindi) na mmoja (Mkinga).
Alisema watoto wote waliopotea walionekana kwa nyakati tofauti wakiwa hai na kwamba umri wao ulikuwa kati ya miaka mitano na 13.
Pia, baadhi ya watu waliohojiwa walibainisha kuwa kuna watoto wanaoibwa
na kupelekwa kwenda kutumikishwa nje ya nchi katika nchi za Mashariki ya
Kati na Ulaya kutokana na kushamiri kwa biashara ya usafirishaji watu.
Ahmed Sheikh ambaye awewahi kufanya kazi za ndani katika nchi za
Mashariki ya Kati, anasema baadhi ya watu huwalaghai wazazi kuwa
wanakwenda kuwasomesha watoto wao Uarabuni au Ulaya, lakini hali huwa
kinyume chake kwani wakifika huko hutumikishwa kwa kufanya kazi zilizo
juu ya umri wao ikiwamo kuhusishwa na biashara na ngono.
Ushirikina watajwa
Baadhi ya watu wamewanyooshea kidole waganga wa jadi kwa madai kuwa
wameshiriki kupotea kwa watoto kwa imani za kishirikina. Wamesema yapo
matukio ambayo watu walikamatwa wakijaribu kuwatorosha watoto na
kuwapeleka kusikojulikana.
“Kama utakumbuka yule mtoto aliyekamatwa na kichwa cha mtoto utaelewa
kuwa ushirikina nao unahusika hapa. Sasa kama yule mtoto asingekamatwa,
wazazi wake hadi leo wangekuwa wanasema mtoto wao alipotea au
alichukuliwa na mtu wasiyemjua,” anasema Vero Msemwa mkazi wa Temeke
Mwisho.
Mganga wa jadi, Dk Ameir anayeishi Mkuranga, Pwani anasema baadhi ya
watu huenda kwake wakitaka awasaidie kuwatafuta watoto wao waliopotea
katika mazingira anayoyataja kuwa ya kutatanisha.
Anasema waganga wanatumia nafasi hiyo kuwaibia wateja wao fedha, kwani
siyo rahisi wakasema hawawezi kumpata mtoto aliyepotea, badala yake
hubadilisha sababu kila siku huku wakizidi kujiingizia fedha.
“Mtu anaweza kukwambia anaweza kumvuta mtu wako aliyepotea au kuibwa
hata kama yupo mbali namna gani, lakini utamngoja ndugu yako huyo hadi
uchoke, na kama ukimsumbua anaweza kukufanyia kitu chochote kibaya,”
anasema.
Waziri aliahidi kuwalinda watoto
Akisoma hotuba ya makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2013/14,
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alisema
kuwa Serikali imeanzisha timu maalumu za kusimamia ulinzi wa watoto
katika mikoa 24 Tanzania Bara.
Alisema kutokana na kuendelea kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto,
imeanzisha mikutano ya kuongeza uelewa wa ukatili dhidi ya watoto katika
mikoa ya Mara, Shinyanga na Singida.
“Wizara yangu itaendelea kuwatambua na kuwapongeza wadau wanaoshiriki
kikamilifu na kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa
haki za mtoto na kuzuia ukatili wa watoto,” alisema.
Mwanaharakati wa haki za watoto, Usu Mallya anasema watoto wengi
wanaopotea wanatoka katika familia duni, ambazo zinashindwa kumpa mtoto
ulinzi wa kutosha. Usu anasema watoto wanaoishi uswahilini wanapotea kwa
sababu ya kukosa maeneo ya kucheza yaliyotengwa kwa ajili yao.
“Watoto watengewe maeneo maalumu yenye ulinzi, najua ni suala la kisera
na kijamii na kama mambo haya yote yatajumlishwa kwa pamoja watoto
watakuwa salama,” anasema.
Pia, anawanyooshea kidole wanaume wanaowapa mimba wasichana kisha
wanazikana, kuwa wanahitaji kulaumiwa kwa kushiriki kuwaweka watoto
kwenye mazingira hatarishi ya kupotea.
“Wanaume wanasababisha mama anakuwa na watoto wengi baba tofauti halafu
baadaye anashindwa kuwalinda wote, haya wanaume wabanwe wawalee watoto,”
anasema.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment