TAARIFA KUHUSU MWANAFUNZI ALIYELIWA NA MBWA KARIBU NA IKULU
Jeneza la Mwili wa Marehemu Iblahim Faraja Chipungahelo likiteremshwa makaburini kwa ajili ya mazishi.
Mchungaji akiendesha ibada ya mazishi ya Marehemu Iblahim Faraja Chipungahelo
Waomboleaji wakiuzika mwili wa marehemu Iblahim Faraja Chipungahelo
Mmoja wa Mbwa wanaodaiwa kumuua marehemu Iblahim Faraja Chipungahelo ameuwawa.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio hilo.
…………………………………………………………………………………………………………….
Na Bazil Makungu Ludewa
MWANAFUNZI wa shule ya msingi Ludewa mjini katika mkoa wa Njombe Iblahim Faraja Chipungahelo ameuawa na kisha kuliwa nyama na mbwa wanaosadikika kuugua kichaa kwa kukosa chakula kwa muda mrefu.
Tukio hilo la kusikitisha na lililoleta simanzi kubwa kwa wakazi wa Ludewa mjini lilitokea August 8 mwaka huu majira ya saa saba mchana katika eneo la Ikulu ambapo marehemu Chipungahelo pamoja na wenzake walikuwa wakipita njia karibu na nyumba ya mtu aliyejulikana na kwa jina la Bosco Lingalangala kwenda kuchuma mapera kama ilivyo destuli yao.
Mashuhuda wa tukio hilo mama Kumba na mama Haule wakazi wa kitongoji cha Ibani katika kata ya Ludewa kwa pamoja walieleza kuwa wakiwa nyumba walisikia kelele za watoto jirani huku wakimwita mwenzao marehemu bila mafanikio.
‘’’’ Tulipowauliza walisema kuwa mwenzao Ibrahim amekamatwa na mbwa na ndipo tulipokusanyika na kwenda kumwokoa mtoto lakini tulipofika eneo la tukio tulimkuta mbwa wakiendelea kumla marehemu huku amelala kifudifudi lakini tulishindwa kumwokoa na ndipo tukakimbia kutoa taarifa kituo cha polisi.””” walisema akina mama hao kwa uchungu
Kwa mujibu wa taarifa ya daktari Sira Rajabu wa Hospitali ya wilaya ya Ludewa aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu alisema mtoto Ibrahim alikuwa na majeraha makubwa mwili mzima huku paja la mguu wake wa kulia likiwa limeliwa na kuondolewa nyama.
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi Fulgensi Ngonyani alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwahoji watu mbalimbali akiwemo mmiliki wa mbwa hao ambaye inasadikika kuwa ananishi jijini Dar es salaam.
Akizungumza na mwandishi wetu mganga wa mifugo Simoni Haule alisema kuwa mbwa hao wa bwana Bosco Lingalangala hawajapata chanjo zaidi ya miaka miwili sasa kwa hiyo tayari mbwa hao wanaugua ugonjwa wa kichaa ambacho hawawezi kupona tena na dawa iliyobaki ni kuuawa tu.
Mmiliki wa mbwa hao Bosco lingalangala hakupatikana ili kuzungumzia suala hilo kwa sababu simu yake ya mkononi haikupatikana.
Hata hivyo akiwa makaburini diwani wa Kata ya Ludewa Monica Mchiro aliwaambia na kuwatahadharisha waombolezaji na wananchi waliohudhuria mazishi kuwa mawasiliano yamefanywa kati yake na mmiliki wa mbwa hao lakini majibu aliyoyatoa hayana ushirikiano kwa sababu ameahidi kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakaye husika kuwadhuru mbwa wake.
Hata hivyo habari kutoka kwa majirani ambao hawakupenda kutaja majina yao walisema mbwa hao hufungiwa kwenye banda na hupewa nyama mbichi kwa kurushiwa na wahudumu lakini siku hiyo walifunguliwa na kuanza kuzagaa kwa nia ya kujitafutia chakula wenyewe baada ya kukosa kwa muda mrefu.
0 comments:
Post a Comment