Wednesday 13 August 2014

WALIOPATA UFADHILI CHINA WAAGWA


picha moja
Watanzania waliopata ufadhili wa masomo nchini China katika ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu katika fani ya mafuta na gesi wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi (wa nne kutoka kushoto mstari wa nyuma) pamoja na watendaji wengine wa Wizara ya Nishati na Madini mara baada ya kuagwa rasmi katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini.Wengine katika picha (mstari wa mbele) ni Kamishna Msadizi Nishati anayeshughulikia Umeme, Eng.Innocent Luoga (wa kwanza kulia), Kamishna wa Madini, Eng.Paul Masanja (wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi Utawala – Bi. Caroline Musika (wa kwanza kushoto).

picha mbili
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi (wa tano kutoka kushoto waliosimama), akiwatambulisha wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo nchini China (baadhi hawapo pichani) waliofika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini na kukabidhiwa nyaraka zitakazowawezesha kujiunga na masomo nchini China.Wanaowatazama wanafunzi hao ni Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Caroline Musika (wa kwanza kushoto, waliokaa), Mkurugenzi Msaidizi-Rasilimali Watu, Lusius Mwenda (wa kwanza kulia),Kaimu Kamishna Msaidizi,Maendeleo ya Nishati, Eng. Juma Mkobya (wa pili kutoka kulia), Kamishna wa Madini, Eng. Paul Masanja (kushoto kwa Mhe.Waziri).Wengine katika picha ni watumishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na waandishi wa habari.
piccha tatu
Bi. Erasma Rutachura, ambaye amepata ufadhili wa masomo nchini China,ngazi ya shahada ya uzamivu katika mafuta na gesi akipokea nyaraka zitakazomwezesha kujiunga na masomo yake mwaka huu.Anayempa nyaraka hizo ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kutoka kulia).Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.
Serikali ya China kupitia Wizara ya Nishati na Madini imetoa ufadhili wa nafasi kumi (10) za masomo kwa watanzania katika ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu katika fani ya mafuta na gesi.
Katika shahada ya uzamili wamechaguliwa watanzania 9 kati ya 46 walioomba ufadhili ambapo katika shahada ya uzamivu amechaguliwa mtanzania mmoja kati ya wanne waliowasilisha maombi.
Msaada huu wa masomo umetolewa na Serikali ya China kwa Tanzania kufuatia juhudi za Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha kuwa Serikali inakuwa na rasilimaliwatu ya kutosha katika kusimamia Sekta za Nishati na Madini hasa sekta ndogo ya mafuta na gesi inayokua kwa kasi hapa nchini.
Ufadhili huu ni wa pili kupitia Wizara ya Nishati na Madini ambapo wa kwanza ulitolewa katika mwaka wa fedha 2013/14 kwa nafasi 10 katika ngazi ya shahada ya uzamili kwenye fani za nishati na madini ikiwemo uhandisi migodi, uhandisi wa nishati katika mafuta na gesi. Wanafunzi hao wanatarajia kuingia mwaka wa pili wa masomo mwezi septemba, 2014.
Nafasi hizi zimepatikana kwa ushindani baada ya kutangazwa kwenye vyombo vya habari ambapo vigezo vilivyotumika kupata ufadhili ni aina ya kozi aliyoisoma mwombaji katika Shahada ya kwanza au Uzamili,  Chuo alichosoma shahada ya kwanza,   kiwango cha ufaulu katika shahada ya kwanza kuanzia GPA 3.0 na Uwiano wa jinsia.
Faida ambazo Tanzania itapata kutokana na ufadhili huu ni kuongeza wataalam katika fani za sekta za nishati na madini na hasa sekta ndogo ya mafuta na gesi, kuongeza fursa za masomo kwa watanzania hasa kwa kuzingatia kuwa wengi hukosa elimu kutokana na kutomudu gharama, na kuzidi kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na China.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA