HUYU NDIYE MFUNGWA ALIYERUHUSIWA KUOA NCHINI MAREKANI
Mtu aliyeua watu wengi nchini Marekani na kufungwa kifungo cha maisha Charles Manson, mwenye umri wa miaka 80, ameripotiwa kupewa hati ya kuoana na mwanamke mwenye umri wa miaka 26 ambaye amekuwa akimtembelea gerezani.
Hati hiyo ya ndoa ilitolewa siku 10 zilizopita kwa Manson na Afton Elaine Burton, limeripoti shirika la habari la Associated Press.
Bi Burton alihamia Corcoran, California, miaka tisa iliyopita ili kuwa karibu na gereza la Manson.
Manson anatumikia kifungo cha maisha jela kwa kuua watu saba na mtoto mmoja ambaye hakuwa amezaliwa huko Los Angeles Marekani mwaka 1969.
Waliouawa ni pamoja na mwigizaji aliyekuwa mjamzito Sharon Tate, mke wa mwongoza sinema Roman Polanski.
"Wote mtajua kuwa ni kweli... Itatokea," ameliambia shirika hilo.Bi Burton, ambaye anajiita nyota, ameliambia shirika la Associated Press kuwa ataoana na Manson mwezi ujao. Hati hiyo imeripotiwa kudumu kwa siku 90.
"Nampenda," ameongeza kusema.
Kiongozi huyo wa kidini na wafuasi wake, wakijulikana kama Familia ya Manson, aliwachoma visu na kuwaua kwa kuwapiga risasi watu saba huko Los Angeles katika siku mbilimwezi Agosti 1969 katika jaribio la kutaka kuanza vita vipya vya matabaka ya rangi.
Manson na wanawake watatu washirika wake walihukumiwa adhabu ya kifo kutokana na mauaji hayo, lakini hukumu hiyo ilitolewa mwaka 1972 wakati jimbo la California lilipositisha kwa muda adhabu ya kifo.
Mwaka 2012, Manson alinyimwa parole yaani msamaha wa kuachiliwa na jopo la gereza la California - ilikuwa mara ya 12 kwa Manson kuomba kuachiliwa huru.
Kwa matokeo hayo, Manson hastahili tena kuomba parole hadi mwaka 2027.
-BBC