Friday, 9 January 2015

YANGA NJE MAPINDUZI CUP.CHEKI WALIVYOFANYWA


???????????????????????????????
YANGA SC imetupwa nje ya kombe la Mapinduzi 2015 kufuatia kutandikwa bao 1-0 dhidi ya JKU katika mechi ya mwisho ya robo fainali iliyomalizika uwanja wa Amaan usiku huu.
Bao pekee la Amour Omar ‘Janja’ lililofungwa katika dakika ya 72 limetosha kuwatumbukiza Wanajeshi hao katika hatua ya nusu fainali.
Kipindi cha kwanza timu zote ziliuanza mchezo kwa makani na kupata nafasi kadhaa za kufunga, lakini washambuliaji wa timu zote hawakuwa makini.
Yanga walianza kwa kutawala mchezo huo wakipigiana pasi za uhakika kuanzia katikati, lakini hesabu zao hazikuwa nzuri kila walipofika eneo la hatari la wapinzani wao.
Dakika ya 24 kipindi cha kwanza, Amiss Tambwe aliendeleza maajabu yake ya kukosa mabao ya wazi katika michuano ya kombe la mapinduzi kwani alipata nafasi nzuri ya kufunga kufuatia mabeki wa JKU kuchanganyana na kipa wao Mohammed Abdallah, lakini Mrundi huyo alipiga mpira nje.

Dakika ya 35 kwa mara nyingine tena Tambwe alishindwa kuifungia goli Yanga kufuatia kupata mpira wa kona, lakini alipaisha juu.
Katika dakika ya 42, Saimon Msuva aliingiza krosi murua kutoka winga ya kushoto, Tambwe alipiga kichwa cha kudundisha mpira chini akimchanganya kipa, lakini gozi hilo la Ng’ombe likapaa juu ya lango.
 Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.
???????????????????????????????
Kipindi cha pili Yanga walianza kwa kasi wakilishambulia lango la JKU na katika dakika ya 46 Andrey Coutinho alipiga shuti kali, lakini halikulenga lango. Ndani ya sekunde kadhaa Msuva naye alipata nafasi na kupiga shuti ambalo halikulenga lango pia.
Dakia ya 49 Coutinho alipiga mpira wa adhabu ndogo uliobabatiza ukuta wa JKU na kumkuta Kpah Sherman aliyezamisha mpira nyavuni, lakini kibendera cha mwamuzi msaidizi, Mbaraka Haule kilikuwa juu kuashiria mfungaji wa goli pamoja na Msuva waliotea.
Yanga waliendelea kushambulia kwa dakika zote, lakini kama ilivyokuwa katika mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Shaba, walikuwa wanakosa nafasi za wazi.
???????????????????????????????
Licha ya Yanga kushambulia muda mwingi, JKU walionesha ukomavu hasa katika ukabaji wa nafasi na mtu kwa mtu, hivyo kuwafanya Yanga washindwe kuliona lango lao kirahisi.
Wakati Yanga wakitafuta bao la kuongoza, katika dakika ya 72, Amour Omar ‘Janja’ aliachia shuti kali lililomshinda kipa wa Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’ na kuzama nyavuni akiiandika JKU bao la kuongoza.
Kufungwa kwa bao hilo kuliwaamsha hasira Yanga na kushambulia kama nyuki, lakini uwezo wa golikipa wa JKU na nidhamu ya ukabaji ya mabeki iliwasaidia kuzuia ‘presha’ ya Yanga.
Mpaka dakika 90 zinamalizika Yanga walikuwa nyuma kwa bao 1-0.
Hata hivyo, kamati ya mashindano ya kombe la Mapinduzi wamemtangaza Ismail Khamis wa JKU kuwa mchezaji bora wa mechi.
JKU ambao ni vinara wa ligi kuu ya Zanzibar wamefuzu kucheza hatua ya nusu fainali ambapo watachuana na vinara wa ligi kuu Tanzania bara Mtibwa Sugar.
Hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo itatimua vumbi januari 10 mwaka huu uwanja wa Amaan Zanzibar.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA