Monday, 2 March 2015

Mamia ya watoto watekwa Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umesema kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto wa kiume waliotekwa hivi karibuni huko Sudan Kusini walichukuliwa na kundi lililo upande wa serikali.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto, UNICEF, limesema idadi ya watoto waliochukuliwa na wapiganaji wa Shilluk wa Johnson Oloni walikuwa mamia, na sio themanini na tisa kama ilivyodhaniwa hapo awali.
Mhariri wa BBC wa masuala ya Afrika, Mary Harper anasema kwa zaidi ya mwaka mmoja, jeshi la Sudan Kusini na wapiganaji wanaowaunga mkono wamekuwa wakipambana na makundi ya waasi yanayomtii aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar. Bwana Oloni pia ana cheo cha meja jenerali katika jeshi la Sudan Kusini.
Afisa wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, Claire McKeever ameiambia BBC kwamba shirika hilo limekuwa likijaribu kuiomba serikali kuwatafuta wavulana lakini muda unazidi kuyoyoma:
"Jibu tulilopata wakati fulani ni kwamba kundi hili la wapiganaji liko nje ya udhibiti wa serikali lakini tumesema kwa nguvu kwamba maadam wamejumuishwa katika jeshi la serikali, serikali ina jukumu la kuhakikisha watoto hawa wanaachiliwa. Serikali ilionyesha ishara nzuri kwamba wangetafuta kuachiliwa kwa watoto hawa lakini hadi sasa hakuna mtoto aliyeachiliwa. Kwa hiyo muda ni jambo muhimu sana kwa sasa kwa sababu watoto hawa wanapelekwa kuelekea maeneo ambako mapigano yanatokea. Tumewaona watoto katika maeneo haya wakiwa na bunduki mpya na watoto wengine wamehusishwa katika mafunzo karibu kabisa na maeneo walikochukuliwa", anasema McKeever.
UNICEF imesema vijana hao wamegawanywa makundi mawili. Baadhi wamepelekwa kwenye kambi ya mafunzo. Huku wengine wamepelekwa sehemu inayoitwa Melut pembezoni mwa White Nile iliyopo kaskazini mwa nchini. Baadhi ya watu katika eneo hilo la Melut wanasema wameona vijana wenye umri chini ya miaka kumi na mbili wakiwa wamebeba bunduki.
UNICEF imeendelea kusema kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba wapo katika mchakato wa kupelekwa kupambana na waasi. Kwa upande wake, serikali imesema haina mamlaka juu ya wapiganaji waliowateka watoto hao. Nchi ya Sudan Kusini ambayo imejipatia uhuru wake miaka mitatu iliyopita, kwa miongo kadhaa imekuwa na mpasuko mkubwa unaotokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wakati huo huo, makundi ya kupigania haki za binadamu yamezituhumu pande zote mbili kwa kutumia watoto kama wanajeshi.
-BBC

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA