Saturday 9 May 2015

KLABU,WACHEZAJI WAWE MAKINI MSIMU WA USAJILI


MSIMU wa Ligi Kuu ya Bara 2014-2015 utafikia tamati kesho Jumamosi. Timu mbili zitakazoshuka daraja zinatarajiwa kufahamika baada ya mechi za kesho. Hii ni tofauti na walivyofahamika mapema mabingwa wa msimu huu na wawakilishi wa michuano ya kimataifa wa mwakani.
Yanga ilitwaa taji mapema na Azam juzi ilijihakikishia nafasi ya pili na kuungana na mabinhwa hao kuiwakilisha Tanzania kama ilivyokuwa kwa miaka miwili mfululizo iliyopita. Yanga itacheza Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwapokea Azam ambao mwaka huu waliicheza michuano hiyo na Azam itawapokea Yanga ushiriki wao wa Kombe la Shirikisho waliyoicheza mwaka huu. Tunaamini kila timu imevuna ilichokipanda katika msimu huu na ni vema kwa zile zitakazosalia kwa msimu ujao zikiungana na timu nne zilizopanda daraja kujipanga mapema kwa msimu ujao.
Ni wazi kumalizika kwa ligi hiyo siku ya kesho ni mwanzo wa maandalizi ya msimu ujao kwa maana ya kufunguliwa kwa dirisha jipya la usajili kwa msimu wa 2015-2016. Tayari baadhi ya klabu zimeshaanza kupiga vikumbo kusaka saini za wachezaji wapya kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao hata kabla dirisha la usajili halijafunguliwa. Siyo jambo baya kuanza kujipanga mapema, ila Mwanaspoti lilikuwa likizikumbusha timu zote sambamba na wachezaji kuwa makini katika kipindi hiki. Hawatakiwi kukurupuka hasa kwa klabu katika kufanya usajili, watulize vichwa na kulifanya jambo hilo kulingana na mapendekezo ya makocha wao na mahitaji ya klabu. Pia, klabu ziache kufanya usajili wa kishabiki, kwani ndiyo ambao umekuwa ukiziumiza. Klabu zenye utamaduni wa kusajili wachezaji wa kigeni ni lazima ziwe makini na wachezaji wanaoletewa na watu wanaojiita mawakala na hata baadhi ya wadau wa klabu zao kwa lengo la kuepuka kuingizwa mkenge. Katika msimu huu tulishuhudia baadhi ya klabu zilivyouziwa mbuzi kwenye gunia kwa kuletewa wachezaji ambao waliishia kuwa mizigo bila kuzinufaisha.
Yanga iliingizwa mkenge na aliyekuwa kocha wake kwa kuletewa Wabrazili Jaja na mwenzake Emerson kwa kuaminishwa kuwa ni wachezaji wakali na wangeisaidia. Kilichotokea kila mtu anakifahamu. Simba nao sio msimu mmoja au miwili wameshalizwa na usajili wa sifa na kujikuta wakibeba gharama zisizo na sababu. Inapaswa makosa ya mwisho kuwa funzo kwa klabu hizo kama ambavyo wachezaji wanavyopaswa kujifunza kwa wenzao ambao walikurupuka kukimbilia kusajili kwa tamaa ya fedha na kujikuta wakiua vipaji vyao.
Wachezaji, hasa chipukizi ni lazima wajitathimini uwezo wao na klabu wanazotaka kwenda kuzichezea kama wanalingana nazo na zitaweza kuwasaidia kuendeleza vipaji vyao au wanaenda ili kuvizika vipaji na mwishowe kuwa maveterani katika umri mdogo.
Kipindi cha usajili ni msimu wa mavuno siyo kwa wachezaji, bali hata wapambe na makocha wa klabu, lakini tunasisitiza, mambo yafanywe kwa weledi wa hali ya juu kwa manufaa ya pande zote kwa maana ya wachezaji na klabu husika, ili mwishowe soka la Tanzania lipae.
Hatutarajii vituko kama vilivyotokea kwenye dirisha dogo kwa Simba kumtema Mfungaji Bora ili tu kuwafurahisha mashabiki na kushindana na watani zao, na mwishowe kuja kuumizwa kama ambavyo Amissi Tambwe anavyowaumiza kwa kuchanua kwenye ufungaji akiwa Yanga.
Klabu zihakikishe wachezaji wa kigeni wanaowasajili katika vikosi vyao wanakuwa wenye viwango na ubora kuliko walichonacho wazawa, ili kuzisaidia timu hizo ndani na nje ya nchi. Tumekuwa tukishuhudia klabu kama TP Mazembe, Etoile du Sahel, El Merreikh na nyinginezo zinazotamba Afrika zikibebwa kwa kiasi kikubwa na wageni sambamba na wazawa, tofauti na klabu zetu. Wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa ni wachache mno wenye ubora unaoridhisha na kutoa msaada wa klabu husika, lakini wengi wao ni mizigo mitupu na kuvuna mishahara ya bure bila sababu za msingi.
Tunaamini mambo yakifanyika kwa tahadhari na umakini mkubwa kwa pande zote mbili kwa viongozi na makocha wa klabu ni wazi tunaweza kushuhudia ligi tamu zaidi kwa msimu wa 2015-2016 pengine kuliko ilivyokuwa msimu wa 2014-2015 unaofikia tamati kesho.
Mwisho tunawaomba wachezaji wawe makini katika kuingia mikataba na kama itawezekana wawe na mawakili wao wa kuwasimamia.
-MWANASPOTI

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA