MBUNGE LEMA ACHAFUA HALI YA HEWA WAKATI WA ZOEZI LA UANDIKISHAJI BVR
Mbunge wa jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema (mwenye shati la drafti ), akiongea na Mkuu wa Kituo cha Polisi Kati jijini hapo, Thomas Maleko kuhusu kitendo cha Polisi kuwaandikisha majina ya wananchi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura (BVR) katika kituo kilichopo shule ya Sekondari Mkombozi, Kata ya Sinoni. Picha na Diana Saria
Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema jana alichafua hali ya hewa katika Kituo cha Uandikishaji Wapigakura, Kata ya Sinoni baada ya kutaka shughuli ya uandikishaji wa majina isitishwe akidai kuna njama za polisi kuvuruga mchakato huo.Ilidaiwa kuwa kituo hicho kilibadili mfumo wa uandikishaji kwa kuweka utaratibu wa kushika namba kazi hiyo ikisimamiwa na polisi ambao walidaiwa kuwa badala ya kutoa ulinzi walikuwa wakiandikisha majina kinyume cha sheria hali iliyozua mgogoro baina yao na mbunge huyo.
Mzozo uliibuka baada ya Lema kutaka daftari hilo lifutwe ikiwa ni pamoja na kusitisha uandikishaji huo haraka hatua iliyojibiwa na askari hao kutaka Lema aondoke kwenye eneo hilo mara moja kabla hatua hazijachukuliwa dhidi yake. Hata hivyo, alikaidi amri hiyo akisema anafuata sheria na haogopi lolote.
“Huu ni ubatili inawezekanaje polisi ahusike kuandikisha majina ya watu tena kwenye daftari lisilo la Serikali na bila muhuri wowote wa Serikali? Huu ni mpango na mkakati uliopangwa kufanya uhuni kwa kutaka kuandika majina ya watu na kuyatumia kwa njia nyingine isiyofaa,” alidai Lema.
Alisema utaratibu huo uko kinyume cha sheria za uandikishaji na utaratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Alisema Tume na wadau wa siasa kupitia mkurugenzi wa jiji walikubaliana mfumo ambao hauruhusu mtu kuandika jina wala kushika nafasi isipokuwa kila mmoja anatakiwa kuwahi kituoni na kusubiri zamu yake ya kujiandikisha.
“Huu mfumo waliotunga hapa ni wa kimafia na wanachotaka ni kuwaondoa watu kijanja ili wasijiandikishe, haiwezekani mtu akaamka saa 10 usiku kuja kujiandikisha halafu akaambiwa arudi mpaka jioni kwa kuwa kuna watu waliojiandikisha majina. Kazi ya polisi ni kulinda usalama wa raia na mali na si kuandikisha majina ya wapigakura nasema waache zoezi hili haraka kwa kuwa tutasema wanatumika,” alisema Lema.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Kituo cha Polisi Kati, Thomas Mareko alisema utaratibu uliofanyika kituoni hapo ulikuwa wa wananchi na ulikuwa wa amani kabisa hivyo kutaka wanasiasa kutouingilia.
Hata hivyo, utaratibu huo ulilalamikiwa na wananchi ambao walisema ni ukiukwaji wa taratibu na kuwapotezea muda wa kufanya kazi zao.
Mmoja wa wananchi hao, Bruno Joel alisema amesikitishwa na hali hiyo kwa kuwa aliamka saa 10 alfajiri kuwahi nafasi ya kujiandikisha lakini alipofika kituoni aliambiwa ajiandikishe badala ya kusubiri muda mwafaka wa kuingia kujiandikisha kwa mawakala hali aliyodai ni usumbufu.
“Kuanzia jana saa 12 asubuhi nahangaika kupata huduma hii, nimeandikisha jina mara mbili na sijapata huduma yoyote,” alisema Joel.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment